Monday, July 30, 2012

NIDA yaongeza muda wa kujiandikisha Dar



MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza muda wa wiki moja wa kujaza fomu za kuomba vitambulisho vya uraia kwa wakazi wa Dar es Salaam na sasa zoezi hilo ambalo lilikuwa likamilike leo, litakamilika Jumatatu ijayo.

Taarifa iliyotolewa jana na NIDA iliwataka wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kujaza fomu hizo katika kipindi hicho kilichoongezwa kwani hawataongeza tena siku za uandikishaji.

Wakati NIDA ikiongeza muda huo, agizo la mamlaka hiyo ya kuwataka waandikishaji kuwagawia fomu wananchi ili wazijaze wenyewe limeendelea kukiukwa, hali ambayo imefanya vituo vingi vya uandikishaji viendelee kuwa na misururu mirefu ya watu.

Taarifa ya jana ya NIDA ilisisitiza tena suala hilo na kuwa waombaji wasiojua kusoma na kuandika watasaidiwa kujaza fomu na wananchi wanaojua kusoma na kuandika watapewa fomu ili wajaze wenyewe katika vituo vya usajili chini ya wasimamizi walioko katika kila kituo.

Kabla ya kutoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Jackson Mwaimu aliliambia gazeti hili jana kuwa mamlaka yake tayari imeshawataka waandikishaji hao kuwapa wananchi wenyewe wajaze fomu na akashangaa inakuwaje hawazingatii tamko hilo.

“Unajua tunashughulika na binadamu, sisi tumetoa maagizo lakini wao bado wanang’ang’ania kuwajazia fomu kwa kweli wamesababisha usumbufu mkubwa…yaani hawa watendaji wetu ni wagumu kuelewa,” alisema Mwaimu.

Gazeti hili pia lilibaini kuwa katika baadhi ya vituo watu wanaoenda kuandikishwa hawana taarifa juu ya tarehe walizozaliwa wazazi wao hali inayowalazimu wasimamizi wa vituo kuwajazia tarehe za bandia.

Lakini taarifa ya NIDA ya jana ilisisitiza kuwa ni marufuku kutoa taarifa ambazo sio sahihi ikiwemo ya uraia na watakaobainika watashitakiwa na wanaweza kutozwa faini au kuhukumiwa miaka mitatu jela ama vyote kwa pamoja.

Jana hali iliendelea kuwa ya sintofahamu katika vituo vingi. Katika kituo cha Kitunda waandikishaji walikuwa wanatumia utaratibu wa kukusanya nakala za nyaraka kama vyeti na vitambulisho na baadaye wanawaita mtu mmoja mmoja kuingia ndani ambako anaenda kuandikishwa kwa ofisa.

Utaratibu huo ulilalamikiwa na wananchi kuwa unachelewesha na kufanya eneo hilo kuwa na wananchi wengi ambao hawajajiandikisha.

Baadhi ya waandikishaji walipoulizwa na mwandishi kwa nini wasiwagawie wananchi fomu ili wajaze wenyewe walisema hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Lakini walipobanwa kuwa tayari NIDA kupitia kwa mkurugenzi wake mkuu Mwaimu ameshatoa ruhusa wananchi wanaojua kusoma na kuandika wagawiwe fomu hizo, mmoja wa maofisa wanaoandikisha alisema eneo hilo lina watu wengi ambao hawajui kusoma wala kuandika.

“Huku kuna watu wengi hawajui kusoma wala kuandika ndio maana tunalazimika kuwaandikisha,” alisema ofisa huyo jambo ambalo wananchi wengi waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo walikanusha madai hayo ya kuwa hawajui kusoma wala kuandika.

Lakini baada ya mwandishi kushauri waandikishaji watumie busara wawaruhusu wananchi wajaze wenyewe fomu walikubali na kuwafanya wananchi wengi kwa kipindi kifupi kujiandikisha kwa wingi badala ya ilivyokuwa hapo awali.

“Unaona kumbe walikuwa wanakiuka utaratibu, walikuwa wanaweka mazingira ya rushwa,” alisema mwananchi mmoja baada ya kuona katika kipindi kifupi wananchi wanajiandikisha.

Katika kituo cha Masaki cha kujiandikisha, pamoja na kwamba kulikuwa hakuna foleni kubwa ya watu kama vituo vingine, ujazaji fomu hizo ulichukua muda kutokana na wahusika kuwajazia fomu watu wote hata wale wanaojua kusoma na kuandika.

Alipoulizwa mmoja wa waandikishaji kwanini hawapatii fomu wanaojua kusoma na kuandika na kujijazia wenyewe fomu hizo ili kuepuka makosa kama vile majina, alijibu kwa ukali kuwa, huo ndio utaratibu uliowekwa.

Katika kituo cha Msasani, mwananchi mmoja alidai fomu yake iliyopewa namba 90 aliichukua Ijumaa na hadi jana alikuwa hajafikiwa kuandikisha na akalalamika kuwa uandikishaji unaenda kwa kasi ndogo.

Katika kituo hicho pia kwa mujibu wa mwananchi huyo, waandikishaji hawaruhusu wananchi kupewa fomu na kuzijaza wenyewe hali ambayo imesababisha kasi ya uandikishwaji iwe ndogo.

Katika kituo cha Mogo kilichoko eneo la Majumbasita Ukonga kulikuwa na misururu mirefu huku watu wakiwa wamefika tangu saa kumi na moja alfajiri kutaka kujiandikisha huku baadhi wakiwalalamikia waandikishaji wasaidizi kwa kutowapa ushirikiano.