Tuesday, July 3, 2012

Mtoto azaliwa bila kichwa, kifua - Singida

MTOTO wa ajabu amezaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida huku akiwa hana baadhi ya sehemu za mwili wake kuanzia kifuani hadi kichwani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Joseph Malunda amesema tukio hilo ni la mara ya kwanza katika Hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo mama wa mtoto huyo alikuwa amejifungua watoto wawili pacha wote wa kike wakiwa na miezi saba huku mmoja akiwa na viungo vyote.
Dk.Malunda alidai mama wa watoto hao Amina Bilau baada ya kujifungua mtoto wa kwanza, alifuatia mtoto mwingine ambaye hakuwa na mikono, kifua na kichwa.
Hata hivyo, mtoto wa kwanza aliweza kuishi kwa saa sita tu na kufariki.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Malunda alitumia fursa hiyo kuwashauri akina mama wanapopata ujauzito wasisite kuhudhuria kliniki na kuacha kutumia madawa makali yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa watoto wenye upungufu wa viungo.
Akizungumzia tukio hilo, Amina Bilau mkazi wa Kijiji cha Mtamaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida alisema wakati wa ujauzito wake yeye aliona tumbo lake likiongezeka, na baada ya kupata matibabu katika zahanati ya Kijiji bila mafanikio na akaamua kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kisha kujifungua watoto hao.
Baba wa watoto hao, Maulidi Mkuki alisema hata yeye anashangaa kuona mkewe amejifungua mtoto wa aina hiyo wakati wana watoto wengine watatu waliozaliwa bila matatizo yoyote yale.
‘’Kwa kweli naona ni ajabu kwa mama kujifungua mtoto na ‘mdoli’ alisema Mkuki akiwa na masikitiko.