Monday, July 2, 2012

Mgomo uliotangazwa na CWT wapingwa

Mgomo uliotangazwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) dhidi ya Serikali unaokusudia kufanyika hivi karibuni umeingia katika sura mpya baada ya walimu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kuupinga kuwa hauna maana wala tija bali umetangazwa na viongozi wa chama hicho kutokana na maslahi yao binafsi.
Katika taarifa yao waliyoisambaza kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa walimu waliojitoa CWT, Sabidi K. Sabidi, walisema mgogoro huo ni kati ya viongozi wa chama hicho na serikali na siyo walimu kama inavyoelezwa.
Kabidi alisema viongozi wa CWT Taifa lazima watambue kuwa mgomo siyo suluhisho la kumaliza tatizo bali kinachotakiwa kufanyika ni mazungumzo na serikali kwani kumekuwa na migogoro mingi kati ya chama hicho na serikali lakini haijaweza kuzaa matunda.
Alisema walimu katika Manispaa ya Ujiji hawaoni umuhimu wa kujiingiza katika mgogoro huo kwasababu bado serikali inaendelea kuyatafutia ufumbuzi madai ya walimu kwa awamu hivyo kugoma hakutasaidia badala yake kutakwamisha jitihada zinazofanywa na serikali.
Alisema viongozi wa CWT wamalize kwanza kushughulikia matatizo yaliyopo ndani ya chama chake yanayolalamikiwa na wanachama badala ya kukimbilia migomo kana kwamba wao ni wasafi ndani ya chama.
Chama cha Walimu Tanzania kimetangaza mgomo wa walimu nchi nzima utakaoanza Julai 7, mwaka huu ikiwa ni shinikizo la madai ya nyongeza ya mishahara na posho za kujikimu na kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Katika mkutano uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, baraza la CWT liliagiza kuwa Juni 5, mwaka huu viongozi wa CWT, ngazi zote kutekeleza matakwa ya kutangazwa mgogoro kwa mujibu wa sheria za Ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004.
Baraza hilo liliidhinisha kuwepo kwa mgomo ikiwa serikali itashindwa kutekeleza matakwa ya walimu ya kutaka kuongezewa mshahara kwa asilimia 100. katika mgomo huo.