Madaktari wa
mafunzo kwa vitendo (Interns) ambao walikuwa nguzo kubwa katika mgomo wa
madaktari ambao umetikisa sekta ya afya tangu Juni 23, mwaka huu,
wameanza kuripoti Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kujua hatima yao
kama walivyotakiwa kwenye barua za kuwarejesha wizarani.
Akizungumza katika ofisi za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Godbless Charles, alisema wamefika wizarani hapo ili kujua sababu za serikali kuwaita.
Hata hivyo, Charles, alisema wao wako tayari kwa lolote watakaloambiwa na serikali.
“Tumekuja ili tujue wanachotaka kutuambia…tuko tayari kutimiza masharti yoyote watakayotuambia, yawe ya kisheria au vinginevyo, ilimradi tu yasitukandamize,” alisema Charles, aliyekuwa amefuatana na baadhi ya viongozi wenzake.
Viongozi hao pamoja na madaktari wenzao ambao walikuwa wamesimama nje ya lango la wizara hiyo, jana walifika wizarani hapo kufuatia wito wa serikali wa kuwataka wote waliohusika kwenye mgomo nchi nzima, kufika mara moja kwenye ofisi hizo kupewa tamko la serikali dhidi yao.
Hata hivyo, msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja, akizungumza na waandishi wa habari wizarani hapo jana alisema tamko rasmi la nini serikali imeamua litatolewa kesho Ijumaa.
Juzi wizara hiyo ilitoa tangazo la kuwataka madakatari wote wa mafunzo kwa vitendo ambao walipewa barua za kurejea Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wanatakiwa kuripoti kwa katibu mkuu wa wizara hiyo Ijumaa (kesho).
Aidha, msemaji huyo alipingana na kauli ya madaktari kuripoti kwenye vyombo vya habari kuhusiana na kukosekana kwa mashine za CT Scan kwenye hospitali za serikali, akidai kwamba zipo za kutosha kwenye hospitali zote za rufaa.
Alizitaja baadhi ya hospitali kuu za serikali nchini ambazo zina mashine hizo kuwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hospitali ya magonjwa ya akili ya Mirembe, hospitali ya magonjwa ya kifua kikuu ya Kibong’oto, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), KCMC, Bugando, Mbeya na hospitali ya magonjwa ya saratani ya Ocean Road.
MOI HUDUMA ZAREJEA
Utoaji huduma katika Hospitali ya Taasisi ya Mifupa (MOI), imerejea katika hali ya kawaida licha ya kuwepo kwa idadi ndogo ya wagonjwa hospitalini hapo huku madaktari bingwa 18 na madaktari 61 wameripoti kazini na kuendelea na kazi.
Akitoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Balozi mstaafu Charles Mutalemwa, alisema mpaka sasa taasisi hiyo imerudi katika hali yake ya kawaida na madaktari wote wanaendelea na kazi kama kawaida.
Mutalemwa alisema tangu madaktari watangaze mgomo Juni 23, mwaka huu, pamoja na kutokea kwa tukio la kupigwa Dk. Stephen Ulimboka, hali ya utoaji huduma katika taasisi hiyo ilikuwa mbaya sana.
Aliongeza kuwa kufuatia hali hiyo, Bodi ya Wadhamini ya Moi iliitisha kikao na madaktari hao Juni 29, mwaka huu ili kuwasihi kuacha mgomo na kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.
Alisema ulipofika Julai 2, mwaka huu, madaktari wote waliitikia wito huo na kurudi kazini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence Museru, alisema awali huduma ya kuona wagonjwa wanaotoka nje pamoja upasuaji usio wa dharura, ilikuwa imesitishwa hospitalini hapo, lakini kwa sasa huduma hizo zinapatikana.
“Jana tulikuwa na wagonjwa watano tu katika chumba cha dharura, kwa kawaida tunakuwa na wagonjwa 35, hivyo tunawataarifu wananchi kuwa huduma MOI imerejea katika hali yake ya kawaida,” alisema.
Alisema kwa sasa vifaa vya kutolea tiba katika hospitali hiyo siyo vya kuridhisha sana, lakini wanajitahidi kutoa huduma kwa wagonjwa.
MADAKTARI 112 WAREJESHWA MUHIMBILI
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), uongozi wa hospitali hiyo umewarudisha kazini madaktari 112 wanaofanya kazi kwa vitendo ambao waliendelea na kazi wakati wa mgomo na kutakiwa kuripoti katika idara zao.
Majina ya madaktari yalibandikwa katika ubao wa matangazo ikiambatana na tangazo lililotolewa na Mkurugenzi wa Utumishi, Makwala Makani.
Waliorudishwa katika sehemu zao za kazi ni pamoja na Idara ya Maabara madaktari 20, waliopo kazini mpaka jana 41, waliokuwa likizo sita, idara ya famasia madaktari 45.
Sehemu ya tangazo hilo lilisomeka: "Yahusu kuendelea na kazi kwa baadhi ya interns ambao waliendelea na kazi wakati wa mgomo...uongozi wa hospitali katika uhakiki wake wa mahudhurio baada ya kuanza kwa mgomo ulibaini kuwepo kwa baadhi ya interns walioendelea na kazi...interns waliopo kwenye orodha iliyoambatanishwa na tangazo hili, hawajaandikiwa barua za kufutiwa ‘rotation’ na wanatakiwa kuripoti kwenye idara zao na kuendelea na kazi.”
Baadhi wa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili walisema wamepata matibabu na madaktari wamewaona wakifanya kazi.
Zainabu Uliza (40), aliyelazwa wodi namba mbili Jengo la Mwaisela, alisema alipata huduma za matibabu pamoja na upasuaji wa mguu.
Cosmas Rwezaura, mgonjwa aliyelazwa katika wodi namba nane Jengo la Sewahaji, alisema alipata huduma baada ya kufikishwa hospitalini hapo jana.
MWANANYALA, AMANA KAZINI
HALI ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, imerejea katika hali ya kawaida huku kukiwa na idadi ndogo ya wagonjwa tofauti na ilivyozoeleka.
Katibu wa Afya wa hospitali hiyo, Dk. Edwin Bisakala, alieleza kuwa madaktari bingwa na madaktari wa vitendo 24, wanaendelea kutoa huduma kama kawaida.
Hata hivyo, Dk. Bisakala alisema kasi ya wagonjwa kufika hospitalini hapo imepungua kutokana na wananchi kudhani mgomo bado unaendelea.
"Wagonjwa waje madaktari tuliopo tuko makini na hakuna anayekufa kwa kukosa huduma hapa,” alisema Dk. Bisakala.
Aidha, Dk. Bisakala alikiri kuwepo kwa upungufu wa vifaa hospitalini hapo na alisema Manispaa ya Kinondoni imeandaa mpango wa kupunguza tatizo hilo ili huduma nyingine zipatikane ngazi ya wilaya.
“Upungufu wa vifaa ni kwa taifa zima, lakini madai ya madaktari ni kwamba huduma zinazopatikana hospitali kubwa kama Muhimbili zipatikane katika hospitali za wilaya, hivyo tatizo hilo linashughulikiwa,” alisema Dk. Bisakala.
HOSPITALI YA AMANA
Katika baadhi ya wodi za Hospitali ya Amana ikiwemo ya watoto ambayo mara nyingi imezoeleka kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, vitanda vya hospitali hiyo viliomekana kuwa tupu.
Mmoja wa daktari katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliishutumu serikali kwa kusema kuwa inatoa vitisho badala ya kutatua matatizo ya msingi ambayo madaktari wanayadai.
Aliongeza kuwa madai yote ya madaktari ni ya msingi na yana faida kwa Taifa zima, lakini mara nyingi watu wamekuwa wakigusia suala moja tu la maslahi kwa madaktari wakati kuna madai kadha kwa kadha yalioainishwa na Jumuiya ya Madaktari kwa faida ya hospitali za taifa zima.
MBUNGE CCM: BUNGE LIJADILI MGOMO
Madai ya wabunge kutaka mgomo wa madaktari unaoendelea hivi nchini ujadiliwe na Bunge, yamezidi kupamba moto, baada ya jana Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola, kuungana na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kudai suala hilo.
Lugola aliungana na wabunge hao jana baada ya kusimama bungeni na kuomba mwongozo wa spika kwamba, kuendelea kuzuia mkutano wa sasa wa Bunge kujadili suala la madaktari iwapo inaruhusiwa au la.
Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilikwishatoa uamuzi wa kuwaamuru madaktari watangaze kumaliza mgomo.
Lugola alisema pia Rais Jakaya Kiwete hivi karibuni alipata fursa kwenye mhimili wa serikali kuzungumzia jambo hilo kwa wananchi.
Kutokana na hoja hizo, alisema ni wakati muafaka kwa Bunge kujadili mgomo huo sababu matatizo kwenye hospitali bado yanaendelea na kwamba, bado migomo ya chini kwa chini inaendelea.
“Hatutawatendea haki Watanzania endapo Bunge hili, ambalo ni chombo cha wananchi halitatunza heshima yake ya kujadili matatizo yanayowakabili Watanzania na kuweza kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu,” alisema Lugola na kuongeza:
“Kwa hiyo nilikuwa naomba mwongozo wako Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuendelea kuzuia Bunge hili kujadili suala la madaktari haliruhusiwi au linaruhusiwa. Naomba mwongozo wako Mwenyekiti.”
Hata hivyo, akitoa Mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba, alisema suala hilo lilikwishatolewa maelezo na Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivyo akaomba wabunge wasubiri hadi mahakama itapotoa uamuzi wake.
“Mimi kama Mwenyekiti kwenda kinyume cha maagizo ya bosi wangu na kwa kuzingatia mihimili hii mitatu, naomba tukubaliane kwamba, suala hili tuliache kuzingatia kwamba, mahakama bado haijatoa ruling (uamuzi). Tutalizungumza baada ya mahakama kutoa ruling yake,” alisema Mabumba.
Juzi Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, aliwasilisha rufaa kwa Katibu wa Bunge, akipinga uamuzi wa Spika wa Bunge, kuzuia mgomo wa madaktari kujadiliwa na Bunge.
Mnyika alichukua hatua hiyo siku chache baada ya kumwandikia Katibu wa Bunge, kutaka Bunge liruhusu suala hilo pamoja na kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, lijadiliwe na Bunge.
Katika barua hiyo, Mnyika pia alitaka ripoti ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, iliyochunguza mgomo huo wa madaktari, ijadiliwe na Bunge.
Mnyika alisema kuwa hadi kufikia jana Ofisi ya Katibu wa Bunge ilikuwa bado haijajibu barua yake.
MUHIMBILI WATOA TAARIFA
Taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana jioni ilieleza kuwa huduma katika hospitali hiyo zimerejea katika hali yake ya kawaida na madaktari walifika sehemu zao za kazi.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha ,alisema huduma za tiba katika hospitali hiyo zimeendelea kuimarika katika maeneo mengi.
MBEYA, DODOMA SAFI
Huduma katika hospitali za serikali katika mikoa ya Mbeya na Dodoma, imerudi katika hali yake ya kawaida ambapo wagonjwa wameendelea kupatiwa kupata huduma kama kawaida.
Katika Hospitali ya Wilaya Dodoma na ya Mkoa, madaktari waliendelea na utoaji wa huduma kama kawaida baada ya kugoma wiki mbili zilizopita.
Mkoa wa Mbeya madaktari waliokuwa katika mafunzo wamefukuzwa na kutakiwa kurudi wizarani baada ya kubainika walijihusisha na mgomo na hivyo wanajeshi kushika nafasi zao.
Uchunguzi uliofanywa katika mikoa hiyo jana ulibaini kwamba hospitali zote jana ziliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa