SERIKALI imesema imeweka kiwango cha pointi 26 watu waliomaliza
kidato cha nne na kutaka kujiunga na vyuo vya ualimu, lengo likiwa ni
kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Elimu ya
Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo wakati alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Manyovu (CCM) Albert Ntabaliba aliyetaka kujua kwa
nini wizara hiyo imeweka kigezo cha pointi 27 katika vyuo vya ualimu
licha ya baadhi ya vijana 78,000 wa Kasulu wenye pointi 28 tayari
walishatuma maombi yao.
Mbunge huyo alitaka kujua Wizara hiyo ilipanga walimu kwa kuzingatia
mahitaji ya walimu na inatoa kauli gani kwa wale ambao wana pointi 27
wakati kuna uhaba wa walimu?
Akijibu swali hilo Mulugo alisema Mwaka jana jumla ya vijana 78,000
waliomba nafasi ya kujiunga na ualimu, lakini Wizara hiyo ilikuwa
inahitaji jumla ya vijana 7000 na Mwaka huu ni mahitaji ya walimu 6800.
“Lengo hapa ni kuweza kuboresha Sekta hii ya Elimu na kwa mwaka ujao
tunaweza kuhitaji Walimu wenye pointi 26 ili tuweze kuwa na elimu yenye
ubora wa hali ya juu,” alisistiza Mulugo.
Aidha alisema asilimia 54 ya Walimu ambao walipangiwa katika Wilaya ya
Kasulu hawakuripoti ila baada ya Wizara hiyo kutoa agizo la kuwataka
walimu hao waripoti kwani iliwaambia wasipofanya hivyo wangelifukuzwa
kazi na hivyo walimu hao waliripoti mara moja.
Katika swali la Msingi la Mbunge huyo ambalo lilikuwa na vipengele
viwili ambapo kipengele (a) alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka
walimu wakutosha katika Vijiji vya Wilaya Mpya ya Buhigwe? Wakati
kipengele (b) kilikuwa kinauliza kama Serikali itakubali zitengwe nafasi
katika Vyuo vya Ualimu vya Kabanga na Kasulu ili kupunguza tatizo hilo
la walimu.
Akijibu Swali hilo Naibu Waziri huyo alisema ni kweli kuna upungufu wa
Walimu katika baadhi ya shule hapa nchini zikiwemo shule za Wilaya mpya
ya Buhigwe na kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wilaya ya Kasulu
ilipangiwa walimu wa cheti 222, stashahada 73 na shahada 94.
Mulugo alisema kwa kuwa wakati huo Buhigwe ilikuwa sehemu ya Wilaya ya
Kasulu ilipata mgawo wake kupitia Wilaya hiyo na katika mwaka huu wa
fedha Wilaya mpya ya Buhigwe zitapewa mgawo wa Walimu waliohitimu
kupitia Halmashauri husika