Tuesday, July 3, 2012

Kamati ya Bunge: Baraza la Mawaziri lipunguzwe

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete ni kubwa.
Pamoja na wingi huo, kamati hiyo imesema hata idadi ya makatibu wakuu na manaibu wao, ni wengi na kwamba kuna haja kwa serikali kupunguza idadi ya viongozi hao, ili kupunguza gharama za matumizi ya Serikali.

Kauli hiyo, ilitolewa bungeni jana na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Paul Lwanji, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012, pamoja na maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2012/2013.

Maoni ya Lwanji, yalilenga Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora pamoja na Mahusiano na Uratibu.

‘‘Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Serikali kwa kujiunga na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa uwazi uitwao Open Government Partnership (OGP).

“Kamati imefuatilia kwa makini utendaji wa Serikali na kugundua, upo uwezekano wa kuunganisha baadhi ya wizara na idara, ili kupunguza ukubwa wa Serikali na hivyo kuleta ufanisi na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali kama ilivyo kwa hivi sasa.

“Mheshimiwa Spika, idadi ya Mawaziri 30, Manaibu Waziri 25, Makatibu Wakuu 26 na Manaibu Katibu Wakuu 26 ni kubwa mno kwa nchi inayoendelea kama yetu.

“Kwa hiyo, kamati inashauri kwamba, Serikali iangalie uwezekano wa kupunguza kwa kuunganisha baadhi ya wizara na idara zinazoshabihiana bila kuathiri utendaji wa shughuli za Serikali,” alisema Lwanji.

Lwanji ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), alisema kamati yake inapendekeza uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu serikalini, uendane na uwezo wao ili kuepuka tatizo la viongozi kushindwa kutimiza wajibu wao, pindi wanapopewa nafasi zisizolingana na uwezo wao kiakili.

“Pia kamati inapendekeza nadharia ya Peter Principle, itumike wakati wa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali, kwani tunapozungumzia uwezo wa mtu wa kumudu majukumu yake, tusisahau kwamba, uwezo huo una ukomo wake kutokana na uwezo wa kiakili yaani IQ, sifa na uzoefu.

“Hivyo basi, mamlaka ikikosea na kumteua mtu kushika madaraka asiyostahili, ni wazi kuwa mhusika atashindwa kumudu madaraka aliyopewa,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema kuna haja kwa Serikali kuangalia namna ya kurekebisha Sheria na Kanuni za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili ifanye kazi kisayansi zaidi.

“Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda kurejea ushauri wake ilioutoa mwaka jana, kwamba ni vema Serikali ikafikiria kurekebisha Sheria na Kanuni za Sekretarieti ya Viongozi wa Umma, ili iweze kufanya kazi kisayansi zaidi na ikibidi kuweka utaratibu wa kuwabana watumishi wengine wa umma ambao siyo viongozi.

“Kamati inashauri Sekretarieti, ifikirie uwezekano wa kuweka taarifa za mali za viongozi wazi kwa umma, kwenye mitandao kama wanavyofanya kwa nchi nyingine duniani ikiwamo Kanada,” alisema Lwanji.

Sambamba na hayo, mbunge huyo aliishauri Serikali kuipa Sekretarieti fedha zote zinazoidhinishwa kwenye bajeti, ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Alisema kuna haja kwa Serikali kuongeza bajeti ya Sekretariti, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ofisi zake za kanda kwa vile njia hiyo, itaifanya ifanye kazi kwa ufanisi zaidi tofauti na sasa, ambapo kazi zinafanyiwa katika ofisi zake kuu za Dar es Salaam.

“Kamati inaishauri, Serikali kuongeza bajeti zaidi, kwa ajili ya Sekretarieti hii ikiwa ni pamoja na kuimarisha ofisi za kanda, ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi kuliko hivi sasa, ambapo Sekretarieti inafanyia shughuli zake kwa kutumia ofisi za makao makuu, Dar es Salaam tu na hivyo kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Ushahidi wa hilo ni kwamba, mwaka 2011 Sekretarieti iliweza kushughulikia mashauri 23 tu ya viongozi wote walioshindwa kutekeleza sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

“Pia mwaka 2011 ni madiwani 1,032 tu ndiyo waliotekeleza Sheria ya Sekretarieti na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya madiwani 1,844 ambao hawakutekeleza sheria,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), aliitaka Serikali iache tabia yake ya kuhamisha fedha za mafungu ya miradi pindi yanapojitokeza mahitaji ya fedha yaliyo nje ya bajeti.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali inatakiwa kuweka utaratibu na mfumo utakaohakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinalindwa.

Chenge aliyasema hayo jana, alipokuwa akitoa taarifa ya kamati yake kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.