ASKARI saba wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakiwamo Luteni Kanali
watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuhamisha na kupitisha Sh
bilioni 3.8 kwa ajili ya ununuzi wa mali chakavu.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi na Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakiwa kwenye gari aina ya
Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T529 ASM lenye vioo vyeusi
wakisindikizwa na gari lenye namba DFP 8763.
Walisomewa mashitaka saba na mawakili kutoka Takukuru, Donasian Kessy na Ben Linkolin mbele ya Hakimu Mkazi Aloye Katema.
Washitakiwa wenye cheo cha Luteni Kanali ni Mkohi Kichogo, Paul Mayavi na Felix Samillan ambaye ni Mkuu Miradi wa Suma JKT.
Wengine ni Kanali Ayoub Mwakang’ata, Sajini John Laizer, Meja Peter
Lushika na Meja Yohana Nyuchi. Wakili Kessy alidai kuwa, Machi 5, 2009
katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirika la Suma JKT, washitakiwa wakiwa
wajumbe wa Bodi ya Suma JKT, walijifanya wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya
Takopa inayoundwa kwa ubia kati ya Serikali ya Korea Kusini na Suma JKT.
Alidai lengo la kujifanya wajumbe wa Bodi ya Takopa, lilikuwa
kupitisha fedha kutoka kampuni hiyo kwenda Suma JKT kwa ajili ya ununuzi
wa magari na mitambo ya ujenzi chakavu bila idhini ya Bodi ya
Wakurugenzi wa kampuni hiyo.
Wakili Kessy alidai kuwa washitakiwa walitumia vibaya ofisi kupitisha
fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa magari pamoja na mitambo hiyo bila
kufuata kifungu cha 58 (3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Aliendelea kudai katika mashitaka ya tatu yanayowakabili Luteni
Kanali Samillan na Luteni Kanali Kichogo kuwa, Machi 16, 2009
walihamisha Sh bilioni 2.8 kupitia hundi namba 000010 kutoka akaunti ya
Takopa namba 0111030331753 kwenda akaunti ya Suma JKT 01110307094 katika
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Ilidaiwa kuwa Aprili 3, 2009, wakijidai wajumbe wa Bodi hiyo ya
Takopa walihamisha Sh milioni 489.7, Aprili 4 walihamisha Sh milioni
269.5, Mei 4, mwaka huo walihamisha Sh milioni 350 kutoka akaunti ya
Takopa kwenda akaunti ya Suma JKT bila kuzingatia Kanuni ya 156 ya
Sheria ya Fedha za Umma.
Katika mashitaka ya saba yanayowakabili washitakiwa wote, ilidai kuwa
kati ya Machi na Mei mwaka 2009 jijini Dar es Salaam, washitakiwa
walipanga njama za kuhamisha fedha kutoka katika taasisi ya Takopa
kwenda kwenye akaunti ya Suma JKT bila kufuata Kanuni 156 ya Sheria ya
Fedha za Umma.
Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na upande wa mashitaka
ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuwa hawana pingamizi
la dhamana endapo washitakiwa watakidhi masharti yatakayotolewa na
Mahakama.
Hakimu Katemana aliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa
kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni 25 kila mmoja. Washitakiwa
walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana hadi Agosti mosi, mwaka huu.
Hata hivyo, baada ya washitakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo,
hawakuwekwa mahabusu kama ilivyo kawaida kwa washitakiwa wengine,
walikaa kwenye gari hadi saa 7 mchana waliposomewa mashitaka yao.