Monday, July 2, 2012

JK: Hatuhusiki unyama aliofanyiwa Ulimboka




Rais Jakaya Kikwete
ASEMA MADAKTARI WASIOKUBALI MSHAHARA WA SERIKALI WAFUNGASHE VIRAGO
Boniface Meena
WAKATI Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya pande hizo mbili.

Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwezi, ambapo mbali na suala hilo, pia alizungumzia sababu za mgomo wa madaktari na usafirishaji wa wahamiaji haramu.

Dk Ulimboka ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, anatibiwa figo na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita.

Tangu kutokea kwa unyama huo uliofanywa na watu wasiojulikana, baadhi ya wananchi na wanaharakati wamekuwa wakiilaumu Serikali kuwa inahusika na utekaji huo na wengine wakienda mbali zaidi, kuwa watekaji walikuwa wanamlazimisha kueleza nani yuko nyuma ya mgomo wa madaktari.

Rais Kikwete, kama awali alivyosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walisema wanatambua kuwa, Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini yeye ameshangazwa na hisia hizo, kwani haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.

"Dk Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.  Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali," alisema Rais Kikwete.

Alisema Serikali haina sababu ya kumdhuru Dk Ulimboka kwa sababu suala la mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kuusitisha, hivyo anayekaidi amri hiyo atakuwa ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola, ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu.

"Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dk Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?" alihoji na kuongeza:

"Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali," alisema Rais Kikwete.

Alisema alichofanyiwa Dk Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.

Alisema Watanzania hawajazoea mambo hayo na kwamba ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.

"Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa," alisema.

Alisema anatoa mkono wa pole kwa Dk Ulimboka na kumwombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.

Rais Kikwete pia alimpongeza Juma Mgaza ambaye alimsaidia Dk Ulimboka kumtoa katika pori alikotupwa na kumpeleka kituo cha polisi kwa moyo wake wa huruma.

Kuhusu mgomo
Kuhusu mgomo unaoendelea Rais Kikwete alisema, kiwango cha mshahara cha Sh3.5 milioni wanachokitaka madaktari Serikali haina uwezo wa kukitoa, hivyo daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara huo, awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho.

Rais Kikwete alisema, kwa sasa Serikali haiwezi kuwaahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa Sh3.5 milioni na posho zote zile, kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi, kitu ambacho haitakiweza.

"Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari. Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha. Nasi tutamtakia kila la heri,"alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema, madaktari hawana sababu ya kugoma ili washinikize kulipwa mshahara huo kwani uwezo haupo.

"Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe," alisema.

Alisema mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria za kazi na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.

Alisema anajua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa yatajitokeza, lakini ni bora kufanya hivyo ili ijulikane Serikali haina daktari.

"Mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo anayekuja awe na mahali pa kuishi."

Kutokana na hali hiyo amewasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini, kwani Watanzania wanateseka na kupoteza maisha.

Sababu za mgomo
Rais Kikwete alisema kwamba, kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na mwafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo kati ya madaktari na Serikali.

Alisema suala la kwanza ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi ambalo Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.

Pia alisema Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili na utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yapi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.

Rais Kikwete alisema kuwa, madaktari wamekataa suala hilo la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.

Alisema suala la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi ambalo Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia nyumba za kuishi.

Rais Kikwete aliongeza kwamba, kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango, Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.

Alisema jambo hilo limekataliwa na madaktari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba.

Rais Kikwete alisisitiza kwamba, Serikali kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa kama wafanyakazi wengine wote wa umma.

Alisema suala lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu na pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma, hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao.

Kuhusu posho, alisema Serikali imekubali kuwapo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.

Alisema madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.

"Tofauti hapa si posho hiyo kuwapo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo," alisema.

Alisema kuna mambo mawili ambayo hayakuwa na mwafaka kabisa kati ya pande hizo mbili na la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance).

Rais Kikwete alisema, Serikali ilishaongeza posho hizo tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa daktari bingwa, Sh20,000 kwa dakari mwenye usajili wa kudumu na Sh15,000 kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).

Alisema hata hivyo, madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara.

Rais Kikwete alisema ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini na kwamba ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.

Alisema jambo la pili ambalo mwafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari ambao madaktari wanataka uwe Sh3.5 milioni wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.

Alisema Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.

Rais Kikwete alisema, kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya Sh1.1 milioni na Sh1.2 milioni kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.

"Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania Sh3.5 milioni," alisema.

Alisema ni muhimu madaktari wakatambua kuwa wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili kuwapo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.

Alisema viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza madaktari katika mgogoro na mahakama na waajiri wao isivyostahili.

Rais Kikwete alisema ni vyema viongozi wa madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana mahakamani kuwa hahusiki nao.

Rais Kikwete alisema madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini kwani mfanyakazi hana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria.

"Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao, kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari kwa hayo wafanyayo," alisema.

Hoja za madaktari
Rais Kikwete alisema katika mambo 12 ambayo madaktari waliyawasilisha pande zote mbili zilifikia mwafaka na kukubaliana kwa pamoja kwa mambo saba.

Alitaja la kwanza ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini ambalo limeshashughulikiwa.

Alisema jambo la pili, ni madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya ambalo Serikali na Wizara ya Afya zimechukua hatua za utekelezaji wake.

Jambo la tatu, alilitaja Rais Kikwete kuwa ni hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya ambalo tayari Serikali imechukua hatua.

"Uongozi wa juu wa wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajabisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona.  Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio," alisema.

Rais Kikwete alisema kuwa, jambo la nne walilokubaliana ni viongozi kuwalazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje suala ambalo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewaeleza madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi.

Alisema jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa.

"Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili," alisema.

Rais Kikwete alisema jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya ambalo Serikali imeliafiki.

Rais Kikwete alisema jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.

Alisema jambo hilo jipya halikuwepo mwazoni, hata hivyo, Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka Sh 10,000 hadi kufikia Sh100,000 kwa daktari na Sh50,000 kwa wasaidizi wake,” alisema.