Tuesday, July 3, 2012

JK apigwa kombora

BAADHI ya wabunge jana walimtupia makombora, Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na mwenendo wa utawala nchini, likiwemo sakata la mgomo wa madaktari na kutekwa na kupigwa kwa Dk. Steven Ulimboka.
Aidha, Kikwete pia alishambuliwa kwa kuunda baraza kubwa la mawaziri, huku akitakiwa kutambua kuwa yeye ni rais wa nchi na siyo waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
Wa kwanza kumrushia kombora Rais Kikwete, alikuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Mbilinyi, ambaye alisema serikali haiaminiki kwa wananchi kuhusiana na sakata hilo, huku akithubutu kusema kuwa waliomteka nyara Ulimboka wanafanana na kundi la kigaidi la Janjaweed ambalo linatuhumiwa kuhusika na kufanya vitendo vya kikatili huko Sudan.
Mbilinyi alisema serikali haina sifa ya kuchunguza kutekwa Dk. Ulimboka kwani inataja kuhusika, na kuhusisha kundi hilo na lile lililowavamia na kuwacharanga wabunge wawili wa CHADEMA huko Mwanza.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mbilinyi iliibua mzozo mzito Bungeni, huku Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba, akionekana kushindwa kumudu kiti cha Spika.
“Mh Mwenyekiti, ndugu yangu Ulimboka katekwa, kapigwa, kang’olewa meno na koleo, kucha na watu wenye silaha. Isijekuwa kama Rais wa Sudan alivyokuwa akitumia Janjaweed kuwaua watu na sisi tukatumia Janjaweed kumteka Ulimboka...,” alisema Mbilinyi.
Wakati akiendelea, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, alisimama kutaka mwongozo wa Spika na kumbana Mbilinyi athibitishe kauli yake.
Hata hivyo Waziri Nagu hakusema jambo gani la uongo alilotaka Mbilinyi athibitishe.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema kwa sasa serikali haiaminiki tena katika suala zima la mgogoro wa madaktari, na hivyo kumtaka rais kukubali kuunda chombo kingine huru kitakachosimamia mgogoro huo kikamilifu.
Mnyika alisema suala hilo ni zito, na serikali haiwezi kudai kuwa inachunguza wakati pande hizo mbili kila moja linatoa taarifa zake.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imeponda ukubwa wa Baraza jipya la Mawaziri aliloliunda, likielezwa kuwa kubwa na halina tija na linaongeza gharama za uendeshaji.
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pamoja na maoni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013, Makamu Mwenyekiti, Paul Rwanji, alisema Baraza la Mawaziri na idadi ya makatibu wakuu ni kubwa mno.
“Mheshimiwa Mwenyekiti idadi ya mawaziri 30, manaibu waziri 25, makatibu wakuu 26 ni kubwa mno kwa nchi inayoendelea kama yetu,” alisema Rwanji.
Alisema kamati yake inashauri kuwa serikali iangalie upya uwezekano wa kuunganisha baadhi ya wizara na idara zinazoshabihiana bila kuathiri shughuli za utendaji wa Serikali.
Pia Kmati hiyo ilipendekeza uteuzi wa watendaji wa Serikali uzingatie uwezo wa kiakili sifa na uzoefu.
Kwa mujibu wa Rwanji, Kamati hiyo iliitaka Serikali kuweka utaratibu ambao ni endelevu wa kupima utendaji wa viongozi na watendaji utakaoendelezwa hadi ngazi ya chini.
Kamati hiyo pia ilihoji mpango uliowahi kuzungumzwa mara nyingi na Rais Kikwete wa kutenganisha biashara na siasa.
“Kamati inapenda kupata ufafanuzi ni kwa kiasi gani dhana hiyo ya kutenganisha uongozi na biashara imetekelezwa hadi sasa?” alihoji.
Hata hivyo kumbukumbu zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mpango huo ulikwama baada ya kubaini kuwa idadi kubwa ya viongozi wa siasa kuanzia ngazi ya juu kwa maana ya mawaziri, wabunge, madiwani na wengine, wengi ni wafanyabiashara na wengine walikuwa watu wa karibu na Rais Kikwete.
Kuhusu tuhuma za ubadhirifu, Rwanji alisema kumekuwa na mtindo wa kuhamisha watumishi wa umma pindi wanapokumbwa na kashfa au tuhuma za ubadhirifu katika eneo lingine.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha ubadhirifu kuendelea katika maeneo mengine ambayo watumishi hao wamehamishiwa.
“Kamati inaagiza Serikali kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu mara moja kwa watumishi wote wanaovunja sheria na kanuni za ajira zao na siyo kuwahamishia maeneo mengine.
Akizungumzia rushwa na utendaji wa TAKUKURU, Rwanji aliitaka taasisi hiyo kufanya kazi zaidi ili kuziba mianya ya rushwa. Aliitaka kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya rushwa na ikithibitika kuwepo hata ushahidi wa mazingira, sheria ichukue mkondo wake.