Ikulu
imekanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari , kuwa juzi msafara wa Rais Jakaya Kikwete ulirushiwa mawe na
kulazimika kusimama kwa muda katika eneo la Namanga, Tegeta jijini Dar
es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana, imesema taarifa hizo ni uzushi na
upotoshaji wa makusudi na makosa makubwa ya taaluma ya uandishi wa
habari.
"Msafara wa Mheshimiwa Rais haukusimama, wala kusimamishwa ama kutupiwa mawe katika tukio hilo la Tegeta," ilisema taarifa hiyo.
Ilisema ni bahati mbaya kuwa upotoshaji
huo wa makusudi bado umeendelea hata baada ya tukio hilo kutolewa
maelezo mazuri ya kutosha na ya kina na maofisa waandamizi wa Jeshi la
Polisi Tanzania akiwemo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Kamanda Suleiman Kova na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni,
Kamanda Charles Kenyela.
"Ni kweli kuwa jana (juzi), majira ya saa
nne asubuhi, msafara wa Mheshimiwa Rais Kikwete ulipitia katika eneo la
Namanga, Tegeta, Dar es Salaam, ukienda Bagamoyo ambako Mheshimiwa Rais
alizindua Hosteli ya kisasa ya Stella Maris ya Shirika la Holy Ghost
Congregation la Kanisa Katoliki katika eneo la Msalabani, mjini
Bagamoyo.
Aidha, baada ya kuzindua Hosteli hiyo,
Rais Kikwete alifungua Mkutano wa 20 wa International General Chapter wa
Shirika hilo ambao ni wa kwanza kufanyika Barani Afrika katika miaka
309 iliyopita tokea Shirika hilo lilipoanzishwa mwaka 1703 nchini
Ufaransa na Claude Poullart des Places.
Hakuna wakati wowote, ama wakati wa kwenda
Bagamoyo ama kurudi kutoka Bagamoyo msafara wa Mheshimiwa Rais
ulisimama, hata kwa sekunde moja, kwenye eneo la Namanga, Tegeta, ama
eneo jingine lolote isipokuwa nyumbani kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Mahusiano na Uratibu) Mheshimiwa Steven M. Wassira ambako Mheshimiwa
Rais alipitia kuhani msiba wa mama yake Mheshimiwa Wassira katika eneo
la Masaki, Dar es Salaam." ilifafanua taarifa hiyo.
Imesema hakuna jiwe hata moja lililorushwa
kuelekezwa kwenye msafara wa Rais ambao baada ya kuona vizuizi
vimewekwa barabarani ulipitia pembeni mwa barabara hiyo ya Bagamoyo na
kuendelea na safari yake.