Wednesday, July 11, 2012

Dk. Slaa agoma kuhojiwa na polisi.Asema amepoteza imani na vyombo vya usalama.



KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema hayuko tayari kuhojiwa na polisi kuhusu tishio la yeye na viongozi wenzake kuwindwa na vigogo wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Amesema msimamo huo unatokana na ukweli kwamba yeye na viongozi wenzake wa CHADEMA hawana imani na polisi katika mchakato huo.
Vile vile, wanatilia shaka dhamira ya serikali, ambayo imejikanganya katika kauli za viongozi waadamizi watatu – Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora).
Juzi, baada ya CHADEMA kutoa taarifa kwamba imegundua mkakati wa wana usalama kuwadhuru Dk. Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, zilitoka kauli tatu tofauti kutoka serikalini.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alikanusha habari hizo akisema serikali haihusiki. Alisema, “Hii inaweza kuwa mbinu ya kisiasa tu. Sisi serikalini hatuna mambo ya vyama… sasa kwa nini wauawe? Wana nini hasa, hadi idara ya usalama ifanye hivyo?”
Naye Waziri wa Nchi anayehusika na Utawala Bora, George Mkuchika, aliahidi kutoa tamko kwa maandishi, lakini hakulitoa.
Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi ndiye aliagiza polisi wafanye uchunguzi huo kwa kuwahoji Dk. Slaa, Mnyika na Lema.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kauli hizo zinazojikanganya kutoka kwa viongozi wa serikali ni ishara kwamba hawawezi kuaminiwa katika sakata hili.
“Tunataka waelewe hali tuliyonayo sasa kiusalama hapa nchini ni mbaya, na jukumu la Nchimbi na watu wake ni kufanya uchunguzi wa madai yetu na kuyatolea taarifa. Kama watu wengine wanafikia hatua ya kuomba ulinzi wa maisha yao Umoja wa Mataifa, serikali inataka tusemeje ili ielewe hatari tuliyonayo?” Dk. Slaa alihoji.
Vile vile, Dk. Slaa alisema amepata taarifa kwamba baada ya mpango huo kujulikana, viongozi ndani ya idara hiyo wameanza kulumbana na kulaumiana.
Alisema kitendo cha Dk. Nchimbi kukimbilia katika vyombo vya habari na kutoa kauli hiyo pasipo kufanya uchunguzi kinadhihirisha wazi kuwa alikuwa anajua mkakati huo, na sasa anatafuta ulinzi kwa wananchi baada ya kuona mpango wao umejulikana.
Katika mkutano huo wa jana, Dk. Slaa alisema Kamati Kuu ya CHADEMA iliyoketi juzi jijini Dar es Salaam, imelaani hatua hiyo ya serikali kutumia vyombo vya usalama kutishia usalama wa wananchi wake.
Alisema hatajieleza kwa polisi, bali kama itabidi, atajieleza mbele ya mahakama, kwa sababu ameshapoteza imani na vyombo vya usalama, tangu walipokalia taarifa yake ya kuchunguzwa alipokuwa mbunge mjini Dodoma.
Alisema mazingira ya Jeshi la Polisi kukalia taarifa mbali mbali za hatari bila kuzitolea ufafanuzi ni kielelezo kuwa hata kama viongozi hao watakutana na polisi, hakuna jipya litakalojitokeza kuhusu madai yao.
Alisisitiza kuwa dhamira ya wazi ya Jeshi la Polisi kuficha ukweli wa matukio mbalimbali yanayowakabili viongozi wa CHADEMA imeonekana katika tukio la kushambuliwa kwa wabunge wa chama hicho mkoani Mwanza. Alisema polisi walipewa taarifa za tukio hilo wakati wabunge hao wakiwa wamezingirwa, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
“Leo asubuhi nimepigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Mgonja au Chigonja sikumbuki vema jina lake, akiniomba tukutane; nilichomweleza nikamwambia hapaswi kuniomba juu ya hilo zaidi ya kufanyia kazi kwanza yale yaliyojiri kabla ya taarifa hizi za sasa,” alisema.
Alisema Kamati Kuu ya CHADEMA imelaani kitendo hicho na kueleza kuwa hizo ni dalili za wazi za serikali inayokaribia kuanguka; lakini imeitaka serikali kuepukana na matendo yatakayohatarisha zaidi amani na usalama wa nchi.
Alisema historia inaonyesha utawala wowote unapofikia mwisho wake, viongozi walio madarakani hutumia vyombo vya dola kuhalalisha uwepo wake wa kuendelea kutawala.
Alisema vile vile chama hicho kimejipanga kwa Operesheni Sangara ya Pili, itakayohusisha majimbo 44, kata 806 na vijiji 4000 katika mikoa mitano, katika ziara itakayodumu kwa muda wa siku 40 kuanzia wiki ijayo.
Mikoa itakayofikiwa ni Manyara, Iringa, Morogoro, Dodoma na Singida.
Waanzisha mfumo wa kujitathmini
Dk. Slaa alisema kamati kuu iliazimia kutathmini kazi ya kila kiongozi wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa ndani ya chama hicho kama inaendana na maazimio ya chama kuwatumikia wananchi.
Alisema tathmini hiyo itaanzia katika mchango wa wabunge, madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa, kama watakuwa wamefikia malengo ya kuwakomboa wananchi kwa nafasi zao walizopata.
Kuhusu rushwa katika uchaguzi Dk. Slaa alisema chama hicho kimefuta kanuni za kampeni ndani ya chama na kuboresha nyingine lengo likiwa ni kupambana na suala zima la rushwa ambalo alisema serikali imeshindwa kukabiliana nalo.
“Tunataka tuwe chama cha mfano kwa kukemea na kupambana na vyanzo vyote vya rushwa kwa kuanza na chama chetu na atakayebainika tutamshughulikia,” alisema Dk. Slaa.
CHADEMA pia imebaini mbinu chafu zinazotumiwa na wakuu wa wilaya katika kuwaelekeza wananchi namna ya kutoa maoni juu ya upatikanaji wa Katiba mpya.
Dk. Slaa alisema kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa maoni yatakayopatikana yasiwe ni maoni halisi ya Watanzania.
Alisema tangu mwanzo CHADEMA ilikuwa inafuatilia mienendo mbalimbali ya viongozi wa serikali, hususani wakuu wa wilaya, juu ya wajibu wao wa kuhakikisha wananchi wanatoa maoni yao pasipo kuingiliwa kwa namna yoyote.
“Tunafuatilia kila hatua ya ukusanyaji wa maoni juu ya Katiba mpya kwa ukaribu, na tumebaini baadhi ya wakuu wa wilaya wanaenda siku moja kabla katika eneo linalokusudiwa na kuwapanga watu watakaotoa maoni, na kipi wazungumzie,” alisema Dk. Slaa.
Alisema wakuu hao wa wilaya wakishawapanga wananchi watakaotoa maoni wanawaelekeza wenyeviti wa vijiji au mitaa kuwachagua pindi wanaponyoosha vidole, na kuwanyima fursa wale ambao hawajapangwa kuchangia maoni yao katika Katiba hiyo.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, CHADEMA itaongeza nguvu ya kufuatilia vitendo hivyo, na kisha kutoa taarifa kwa umma juu ya kunyimwa haki yao ya msingi ya kuchangia upatikanaji wa Katiba mpya.