AGIZO la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na mgomo kuacha kazi limechukua sura mpya baada ya madaktari bingwa ambao awali hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi huyo wa nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini. Badala yake, madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao juzi, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka, walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapowarejesha kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa. Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura jana na kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi wa mabingwa hao Dk. Catherine Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao. “Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu… kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi. “Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo. Alisema hata wao hawana sababu ya kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na kuwaona Watanzania wakifa kwa kukosa vifaatiba na dawa. Dk. Mng’ong’o alisema madaktari hapa nchini wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa muda mrefu hivyo wakati wa kubadili hali hiyo umefika na kuwasaidia Watanzania maskini wanaotibiwa kwenye hospitali hizo. Jumuiya yasema JK kadanganywa Kwa upande wao viongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini wameelezea masikitiko yao, ya namna Rais Kikwete alivyopewa taarifa za uongo na wasaidizi wake. Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la watoto kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Katibu wa Jumuiya hiyo Dk. Edwin Chitage alisema wako tayari kumweleza ukweli rais kwa kuwa wasaidizi wake wameshindwa kufanya hivyo. “Rais hajapata taarifa sahihi… tuko tayari kumweleza ukweli kwa sababu wasaidizi wake wanamdanganya, tunasikitika kuona watanzania wakidanganywa. “Wanaelezwa hoja dhaifu za kuonyesha kwamba madaktari hatuna uzalendo wakati madai yetu pia ni kwa maslahi ya wagonjwa wote hasa pale tunapodai mazingira bora ya kazi. Katibu huyo alisema moja ya madai yao yalikuwa kuomba kila hospitali ya wilaya ipate mashine moja ya X-ray kwa vile, haiwezekani nchi nzima kukosa mashine ya CT-Scan wakati bei yake ni sawa na gari aina ya shangingi moja la kiongozi wa serikali,” alisema Dk. Chitage. Katibu huyo alikiri kwamba posho ni sehemu ya madai yao huku akisisitiza kwamba hawang’ang’anii nyongeza hiyo badala yake kuwepo kwanza na mazingira bora ya kazi ili kutoa tiba sahihi kwa mgonjwa. Dk. Chitage alisema hawapendi kubishana na mamlaka ya rais huku akisisitiza uwezo wa kumaliza hili ni Kikwete kukaa nao meza moja kwa ajili ya kuzungumza badala ya kutoa vitisho. Waomba kukutana na Rais Madaktari hao walisema kuwa sasa wanaomba kukutana na rais ili kujadili hatima ya mgomo huo. “Tunamheshimu rais na mamlaka zote ila tunachoamini ni kuwepo kwa meza huru ya majadiliano kati yetu na yeye kwa sababu nafasi ya kumaliza kero hii anayo,” alisema. Naye Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Dk. Godbless Charles alihoji sababu za kuwepo kwa taarifa tofauti kuhusu ongezeko la mishahara wakati waliishauri serikali kuwa wazi kuhusu nyongeza hiyo. “Kumekua na majibu tofauti mfano Waziri wa Afya na UStawi wa Jamii aliliambia Bunge kwamba nyongeza ya mishahara ni asilimia 15. Hotuba ya rais Kikwete inasema nyongeza hiyo ni asilimia 20 wakati ripoti ya wataalam iliyokutana na kamati ya Waziri Mkuu ilipendekeza asilimia 25 je, nia ya serikali iko wapi? “Wakati viongozi wa serikali wakitoa taarifa zinazotofautiana ripoti ya ufafanuzi wa madai na hoja za madaktari iliyotokana na majadiliano ambapo tulikuwa wajumbe hatukutoa pendekezo lolote juu ya ongezeko la mshahara,” alisema Dk. Godbless. Alisema tangu kuanza kwa mgogoro kati ya madaktari na serikali jumla ya vikao sita viliketi kati ya hivyo vikao vinne vilijadili juu ya uboreshaji wa huduma za afya kwa watanzania. “Ni masikitiko yetu kuwa ripoti ya ufafanuzi wa hoja na madai yetu iliyotolewa Juni 31 mwaka huu, taarifa ya waziri wa afya, taarifa ya waziri mkuu ndani ya Bunge na hotuba ya rais haikuzungumzia kwa jinsi gani serikali itaboresha huduma za afya kwa watanzania,” alisisitiza Dk. Godbless. Katika hotuba yake kwa wananchi rais Kikwete aliwataka madaktari wote waliogoma kuchakazi kwa kuwa viwango vikubwa vya mishahara wanaoitaka serikali haiwezi kuilipa. Kipigo cha Dk. Ulimboka Akizungumzia kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande alikofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania Dk. Steven Ulimboka alisema wameshtushwa na kauli ya rais Kikwete. Kwa mujibu wa Dk. Godbless kauli ya rais Kikwete kwamba serikali yake haihusiki na kitendo hicho kimeingilia uhuru wa tume hiyo ambayo tangu awali madaktari na wanaharakati waliipinga. “Tume imeundwa kuchunguza suala hilo na mpaka sasa hakuna mwenye uwezo wa kudhibitisha kwamba serikali inahusika… je ni sahihi kwa rais kutangaza waziwazi kwamba serikali yake haihusiki? “Kauli hiyo haitoi uhuru kwa tume kueleza ukweli wa tukio kwa sababu tume hiyo imeundwa na serikali yenyewe,” alisema makamu mwenyekiti huyo na kuongeza kwamba madaktari hawana imani na tume hiyo. Awali alisema madaktari wana hasira kwa kitendo cha kinyama alichofanyiwa mwenzao hali inayowafanya waishi kwa hofu huku wengine wakiandika barua za kuacha kazi na wengine wakiendeleza mgomo. Bunge lachafuka, kupigwa Ulimboka Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, hali ndani ya bunge jana jioni ilichafuka, baada ya mwenyekiti wa bunge, kushishwa kabisa kuongoza kikao hicho kufuatia kuzuka kwa malumbano makali baada ya Mkuu wa mkoa wa Iringa, Stella Manyanya kukituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa vinara wa mgomo wa madaktari. Manyanya alisema kuwa, CHADEMA wamebainika kuchochea mgogoro huo, hali iliyomfanya Mbunge wa Ubungo kusimama na kuomba mwongozo akimtaka Manyanya kuthibitisha ama kukanusha tuhuma hizo. Lakini katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Iramba mashariki Mwigulu Mchemba alisimama na kunukuu hotuba ya kambi ya upinzani, ambayo ilitamka bayana kuwa inaunga mkono madai ya watumishi wa serikali, na kwamba kwa kauli hiyo inadhihirisha bayana kuwa ndio wakuu wa mgomo huo. Badala ya kutoa mwongozo, Mabumba hakumtaka Manyanya kukanusha ama kuthibitisha alimruhusu Mchemba kuendelea kurusha makombora mazito dhidi ya CHADEMA, safari hii akidai kuwa ni vimbelembele kutoa matamshi ya kulaani kupigwa kwa Ulimboka huku, wakimwacha mmoja wa viongozi wake bila kumhudumia wala kumjulia hali. Katika kujichanganya kwa wabunge hao wa CCM, wakati Mchemba akidai kuwa CHADEMA ndio wachocheaji wakubwa wa mgogoro huo kwa kuwatumia madaktari, mwenzake Manyanya alitoa hoja safari hii akidai kuwa, ndio waliohusika na tukio la kumvamia na kumteka na kisha kumpiga Dk. Ulimboka. Hata pale Mnyika aliposimama na kuomba tena mwongozo wa mwenyekiti, huku akiweka bayana jinsi inavyoelezwa ushiriki wa maafisa wa polisi, na hata Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja wengine kwa majina, alimtaka mchangiaji kuthibitisha ushiriki wa CHADEMA kumjeruhi ama siyo afute kauli yake. Lakini kwa mara nyingine tena, Mabumba hakumtaka Manyanya wala Mchemba kuthibitisha kauli ama kufuta kama inavyofanywa kwa wabunge wa upinzani, badala yake alimruhusu mkuu huyo wa mkoa wa Iringa kuendelea na mchango wake bila kufuta kauli wala kuithibitisha. Kushindwa huko kwa waziwazi kwa Mwwenyekiti wa kikao hicho cha bunge, kuliwachefua wabunge wengi wa upinzani, huku wale wa CCM wakionekana kufurahia jambo hilo. |