WATU watatu wamekufa na wengine 17
kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka katikati ya
Mlima Kitonga, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
Aidha mkoani Pwani imetokea ajali
nyingine ambayo abiria 11 waliokuwa wakisafiri kwa kutumia mabasi ya Dar
Express na Simba Mtoto walijeruhiwa baada ya mabasi hayo yaliyokuwa
yakisafiri kutoka Arusha na Dar es Salaam kugongana uso kwa uso eneo la
Wami mkoani Pwani.
Kuhusu ajali iliyotokea mlima wa
Kitonga, Iringa, mmoja wa majeruhi wanaohitaji msaada wa haraka ni
Vedastus Benjamin (11), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya
Msingi Minazini, Kurasini Shimo la Udongo, Dar es Salaam.
Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisafiri peke
yake kutoka Lusaka, Zambia alikokwenda kumsalimia baba yake mdogo,
amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa sambamba na
majeruhi wengine na anaomba wasamaria wafikishe taarifa hiyo kwa baba
yake mzazi, Vedastus Benjamin.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter
Kakamba alisema ajali hiyo ya gari aina ya Isuzu namba T 218 ACH mali ya
Kampuni ya Mwashi Express ya Dar es Salaam ilitokea juzi saa 11.30
jioni.
Alisema basi hilo likitoka Tunduma
kwenda Dar es Salaam liliacha njia na kugonga gema na kupinduka na
kusababisha maafa hayo. Kakamba alitaja waliokufa kuwa ni Clara Dili
(32) mfanyabiashara na mkazi wa Lusaka, Abel Nelson (32) mkazi wa Dar es
Salaam na Danny Kawin (43), mfanyabiashara na mkazi wa Zambia.
Alisema dereva wa basi hilo, Benjamin
Enock ambaye pia amelazwa katika hospitali hiyo yuko chini ya ulinzi wa
Polisi akisubiriwa apate nafuu ili ahojiwe kwa sababu uchunguzi wa awali
unaonesha ajali hiyo ilitokana na uzembe binafsi uliomfanya ashindwe
kuchukua hadhari.
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald
Guninita jana alifika katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kufariji
majeruhi hao. Pamoja na kutoa pole, Guninita alitoa msaada wa fedha na
vifaa vya tiba kwa baadhi ya majeruhi waliokosa ndugu wa kuwasaidia
wakiwamo wa Zambia.
Katika ajali ya mkoani Pwani, Kamanda wa
Polisi wa mkoa huo, Ernest Mangu alimwambia mwandishi kuwa ilitokea
kati ya Wami na Msata jana saa 7 mchana wakati dereva wa basi la Dar
Express akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake.
Kamanda Mangu alisema dereva wa Dar
Express namba T316 ANS lililokuwa likitoka Arusha kwenda Dar es Salaam,
Juma Lyimo alijaribu kulipita gari la mbele bila uangalifu na kukutana
uso kwa uso na Simba Mtoto namba T901 ASL lililokuwa likiendeshwa na
Khalifa Makame likienda Tanga kutoka Dar es Salaam.