Kampuni
ya Wallis Trading Inc ya Lebanon, iliyoikodisha Kampuni ya Ndege ya
Taifa (ATCL) ndege ya A320, imeanza tena kuibana Serikali kuishinikiza
kulipa deni la Dola milioni 40 (Sh bilioni 60).
Deni hilo linajumuisha mkopo na riba fedha
zinazotokana na ATCL kukodi ndege ya kampuni hiyo mwaka 2007 ambayo
hata hivyo haikufanya kazi.
Ndege hiyo A320-214 muda mfupi baada ya
kukodi iligundulika kuwa na matatizo makubwa ya kiufundi hivyo kubaki
kwenye matengenezo baada ya kushindwa kuruka.
Wallis inataka kulipwa mara moja bila
kupewa visingizio kuwa Serikali haina fedha ama Hazina inahitaji idhini
ya Baraza la Mawaziri.
Katika waraka wa kampuni hiyo ulioandikwa
Mei 16, mwaka 2012 kwa Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
ATCL, Wallis inaikumbusha serikali kuwa mwanzoni mwa mwaka huu
ilipanga jedwali la jinsi ya kuanza kulipa mkopo huo kwa utaratibu wa
awali unaoanzia na malipo ya Dola milioni 10.67.
Barua hiyo inaibana serikali kuwa
ililiandaa jedwali la malipo kwa awamu nne kuwa Januari italipa Dola
3,000,000 na riba ya Dola 90,000 hivyo kuweka kwenye akaunti ya Wallis
Dola 3,090,000.
Malipo mengine yangefuata Februari kwa
kulipa Dola nyingine 1,590,000 wakati pia Machi ingelipa kiwango hicho
hicho na kumalizia na Dola 3,090,000 mwezi Aprili.
“Hadi kufikia Aprili 26, 2012 hakuna pesa
iliyolipwa huku deni na riba vyote vikifikia Dola 10,672,895.57. Kwa
kuzingatia ushahidi huu wa kutosha wa makubaliano dhidi ya deni la Dola
milioni 39 tunarudia tena ombi letu kuwa tafadhali utulipe mara moja
deni letu kwa mkupuo,” ilisema sehemu ya barua hiyo, ambayo nakala yake
imetumwa Wizara ya Ujenzi, Hazina, ATCL na Shirika Hodhi la Serikali
(CHC).
“Tunataka kulipwa bila visingizio kuwa
serikali haina fedha na maelezo mengine yanayotolewa kuwa utahitaji
idhini ya Baraza la Mawaziri kwani serikali ndiyo mdhamini wa ATCL
anayewajibika kulipa Dola milioni 39 na riba inayotozwa katika mkopo
huu,” ilisema barua hiyo ya kurasa mbili.
Kampuni hiyo ililalamika kuwa kuchelewesha
malipo kunaisababishia Wallis gharama zaidi za ushauri wa sheria na
usafiri ambazo ATCL italazimika kuzilipa.
Baadhi ya wajumbe wanaotajwa na waraka huo
kuwa walishiriki kuandaa jedwali la malipo mwanzoni mwa mwaka huu ni
pamoja na Katibu Mkuu wa Hazina, Ramadhani Khija, Geoffrey Mkilla ofisi
ya Msajili wa Hazina, Ezamo Mapunda kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na
Esmail Kassimu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Hata hivyo, walipotafutwa wahusika kuzungumzia deni hilo ilijibiwa na kiongozi mmoja kwa sharti la
kutotajwa jina lake kuwa kama serikali imeahidi kuwalipa, itawalipa
hakuna haja ya kulalamika.
Aliitaka kampuni hiyo kuwa na imani kwani si wao peke yao wanaoidai serikali.