BAADHI
ya wasomi nchini wamelaani kitendo cha kupigwa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, wakisema kuwa kimechukua sura
ya usalama wa taifa badala ya mgogoro wa madaktari. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ally, alisema suala hili sasa limevuka hatua ya mgogoro wa madaktari na limechukua sura ya usalama wa nchi. Alisema mahali ambapo suala hili limefikia wananchi wanataka kuona hatua zinachukuliwa na siyo masuala ya kuambiwa kuwa mihimili inaingiliana. “Jana (juzi) Waziri Mkuu alisema atatoa tamko la Serikali leo (jana), akisema liwalo na liwe, huku watu wakisubiri tamko hilo, Bunge linasema haliwezi kufanya hivyo kwa sababu mihimili inaingiliana,” anasema na kuongeza: “Wanasema hivyo huku watu wanakufa, watu hawajui wala kutaka kusikia mambo ya mihimili, sijui tulibeba kamati kwa ndege, wanataka kupata majibu ya hali hii kutoka kwa Serikali.” Mhadhiri huyo alisema kuwa, watu wengi akiwamo yeye mwenyewe anaogopa hata kutoka ndani kwani, kama siyo Serikali iliyohusika, basi hata kikundi hicho hakijulikani kina orodha ya watu wangapi wanaotakiwa kufanyiwa unyama huo. Alisema kuwa, mgogoro huu umeanza tangu Desemba mwaka jana ambapo madaktari wa mafunzo kwa vitendo waligoma wakidai fedha za chakula na vifaa vya kufanyia kazi, lakini mpaka sasa Serikali imeshindwa kupata ufumbuzi. “Wanasema udaktari ni wito, nani anaweza kufanya kazi akiwa na njaa, kwa nini wao Wabunge wasijitolee kwenda bungeni bila kulipwa posho, waache kutuambia mambo ya separation of power ‘(mgawanyo wa madaraka); watu wanakufa hospitali, wanataka majibu ya Serikali,” alisema Bashiru. Alisema kuwa kuwa, lugha zinazotolewa sasa hivi juu ya mgomo wa madaktari, ni lugha za viongozi walioshindwa kutawala. Kwa upande wake Profesa Abdallah Safari, anasema unyama aliofanyiwa Dk Ulimboka unaonyesha kuwa, sasa Tanzania imefikia katika Siasa za Kimafia. “Tumezoea kusikia wanauliwa wanasiasa, lakini kwetu Tanzania tumeanzisha historia mpya ya kutaka kuuwa Professionals (wataalam) kitu ambacho kwa Afrika hakijawahi kutokea,” alisema Safari. Alisema kuwa, suala hili lisichukuliwe kwa mzaha na kutaka Tume Huru ilichunguzwe kwa kuwa, Serikali inadaiwa kuhusika katika tukio hilo. “Polisi hapa wanasema wanalichunguza, lakini wao ndio wanatuhumiwa, hapa hayatapatikana majibu sahihi, ni lazima kuwe na tume huru,” alisema Profesa Safari. Aidha Dk Benson Bana, aliwataka Watanzania waungane kulaani tukio la kupigwa kwa Dk Ulimboka, kwa kile alichosema siyo utamaduni wa Watanzania. “Lakini nawataka madaktari wajiangalie upya, huwezi kudai haki huku watu wakiwa wanakufa, wakae meza moja na Serikali wajadiliane,” alisema Dk Bana. |