Mufti alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, na kusisitiza lengo ni kukamilisha shughuli hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.
“Katika nchi yetu zimefanyika sensa nyingi miaka ya nyuma na hazikuhusishwa na dini wala ukabila, ni jambo lililozoeleka na kukubalika na Waislamu wote kutoa ushirikiano kwa watumishi wa Serikali watakaopita kuwahesabu,” alisema Mufti.
Mufti Simba alisisitiza kuwa sensa ni utaratibu wa kisheria pia ni suala la maendeleo kwa Watanzania wote hivyo hakuna haja ya kususia.
“Mimi ni kiongozi wa Waislamu wa Tanzania natoa, mwito kwa Waislamu wote kushiriki kikamilifu katika sensa hii pia wasisite kuiuliza Serikali ili iwape ufafanuzi kama hizo takwimu za Waislamu kadhaa na Wakristo wapo kadhaa inazitambua,” aliongeza.
Sensa hiyo inatarajiwa kufanyika kwa siku saba mfululizo kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu, ambapo makarani wa sensa watapita katika nyumba zote kuhesabu watu.
Makarani hao watafanya kazi hiyo kwa siku saba mfululizo na katika kila kaya au nyumba watakayopita, watataka kujua idadi ya watu waliolala katika nyumba au kaya husika usiku wa kuamkia Agosti 6 mwaka huu.
Mbali na kuulizwa idadi ya watu waliolala katika nyumba husika zikiwemo hata nyumba za kulala wageni, pia makarani hao watauliza maswali mengine kuhusu hali ya maisha ya kiuchumi, kijamii na kielimu na taarifa hizo zitakuwa siri, hazitatolewa kwa mtu yeyote.
Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa, makarani hao kabla ya kufanya kazi hiyo wataapishwa kutunza siri na taarifa watakazokusanya kutokana na maswali hayo, zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu.
Mkanganyiko wa dini Pamoja na Mufti Simba kuwataka Waislamu kushiriki katika sensa, pia aliitaka Serikali iwafafanulie kuhusu takwimu za sensa zilizoonesha idadi ya Waislamu na Wakristo.
Kauli hiyo imetokana na madai yaliyopo kuwa baadhi ya mitandao ya jamii na hata ofisi za Serikali zimekuwa zikitoa takwimu zinazopingana kuhusu idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani nchini.
Mufti Simba alisema suala lililowakera Waislamu siyo nafasi ya sensa katika maendeleo ya nchi, isipokuwa jambo lililowafanya kuweka msimamo wa kususa ni takwimu za sensa zilizotolewa hivi karibuni na watu wasio na dhamana ya suala hilo.
Alisema kwa niaba ya Waislamu wote nchini, anaiomba Serikali itunge sheria itakayoainisha mtu au chombo chenye dhamana ya kutoa taarifa za sensa ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza.