WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema hawezi kujiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kutatua matatizo ya madaktari.
Pinda amelieleza Bunge kuwa, hadhani
kama ni busara kujiuzulu kwa sababu ya matatizo ya madaktari na kwamba
suala hilo ni la muda mrefu na ni changamoto.
Waziri Mkuu ametoa msimamo huo wakati
anajibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema)
ambaye alisema, kwa kuwa matatizo ya madaktari ni ya muda mrefu, na
Pinda ameshindwa kuyamaliza, kwa nini asijiuzulu.
Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa, amefanya kila aliloweza kumaliza mgogoro kati ya Serikali na madaktari.
Lissu alimuuliza Pinda kuwa, kama amefanya kila aliloweza kumaliza tatizo hilo na ameshindwa kwa nini asijiuzulu.
Waziri Mkuu amemjibu kwamba, anamuheshimu sana, na hadhani kama hiyo ni namna nzuri ya kumuuliza.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amefunga
mjadala kuhusu mgogoro wa Serikali na madaktari kwa kuwa Mahakama
imelalamika kwa kuwa, suala hilo lipo mahakamani lakini wabunge
wameendelea kuuliza, kudadisi na kutoa taarifa.
Kutokana na msimamo huo wa Bunge,
Serikali leo haitatoa msimamo wake kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea
katika hospitali nyijngi nchini zikiwemo hospitali za rufaa.
Makinda ametoa msimamo huo wakati anatoa
mwongozo alioomba Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye alimuomba aagize
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii itoe taarifa bungeni kuhusu
waliyoyaona walipotembelea hospitali na kuzungumza Serikali, madaktari,
na wadau wakati wa mgomo uliopita wa madaktari.
Makinda amewaeleza wabunge kuwa, yeye
ndiye aliyeituma kamati kufanya kazi hiyo, na ilitoa taarifa kwenye
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi hivyo taarifa hiyo haitawasilishwa
bungeni.
“Sasa suala hili lipo mahakamani na huo mjadala umefungwa”amesema Makinda.