SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kutumia hospitali za Jeshi na
madaktari wastaafu kunusuru afya za wagonjwa kufuatia mgomo wa madaktari
nchini, juhudi zaidi zimechukuliwa na sasa itatumia pia hospitali
binafsi.
Hospitali za awali zilizotajwa kukubali kushirikiana na Serikali
kuokoa maisha ya Watanzania watakaohitaji tiba ya haraka na walio katika
tiba isiyoweza kusitishwa ni pamoja na TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu
Mandal, CCBRT na Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Aidha, nguvu zimeongezwa katika hospitali za Mwananyamala, Amana na
Temeke za Dar es Salaam kunakodaiwa hakuna mgomo, ili kutotoa rufaa
nyingi kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kunakodaiwa kuwa
na mgomo.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja
aliliambia gazeti hili jana ofisini kwake kuwa, utekelezaji wa agizo la
Waziri Mkuu kuhusu kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu
limeanza na sasa nguvu imeongezwa kwa kuhusisha hospitali binafsi.
“Pamoja na Lugalo kuwa tayari, tulikuwa katika mazungumzo na
hospitali za binafsi ikiwa ni juhudi hizo hizo za Serikali, hospitali
kadhaa zimeshakubali ambazo ni CCBRT, Aga Khan, Hindu Mandal, Regency na
TMJ na tunaendelea kuzungumza na nyingine,” alisema Mwamwaja.
Pamoja na hilo, Mwamwaja alisema nguvu kubwa pia imeelekezwa katika
hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana kuhakikisha kuwa wagonjwa
wanatibiwa kikamilifu.
Akifafanua kuhusu namna ya wagonjwa watakavyotibiwa katika hospitali
hizo za binafsi, Mwamwaja alisema;” Kutakuwa na fomu maalumu ambayo
daktari wa Amana, Mwananyamala au Temeke atakayeona mgonjwa anahitaji
tiba zaidi, atamjazia ili apokewe ama kupelekwa katika hospitali hizo”.
Pia alisema wagonjwa watakaohitaji rufaa, kwa utaratibu huo huo,
watatibiwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo ambayo imekuwa tayari
muda mrefu ikishirikiana na hospitali nyingine chini yake.
Alisema mgomo wa awali madaktari walipelekwa Muhimbili kutoa huduma,
lakini baadhi ya madaktari wenyeji mgomo wa awali walidaiwa kuwakwamisha
makusudi kufanya huduma na Serikali ililiona hivyo na kuona ni bora
wagonjwa wapelekwe huko ili kupata tiba vizuri zaidi.
Alisema madaktari wastaafu na wa Wizara kama alivyosema Waziri Mkuu
Pinda, ndio watakaohusika Muhimbili. Pinda alieleza hayo juzi bungeni
akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
aliyetaka kujua hatua za Serikali kukabili mgomo huo.
Jana gazeti hili lilifika Muhimbili kufuatilia mgomo, lakini
ilishindikana baada ya ofisi za wasemaji na lango la Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (MOI) kufungwa ili waandishi wasiingie.
Mlinzi wa MOI ambaye hakufahamika jina, aliwaeleza waandishi kuwa,
amepewa agizo kuwa mwandishi yeyote asiingie kupata taarifa za mgomo au
za Dk Steven Ulimboka.
Mmoja wa wagonjwa Lydia Rwechungura kutoka Chamwino, Dodoma, akiwa
nje ya lango la MOI alisema, alifika hospitalini hapo Juni 25 mwaka huu
baada ya kupewa rufaa ya Hospitali ya Mkoa Dodoma na sasa hajui
afanyeje.
“Pingili za uti wa mgongo zinasigana, nilikuja wakaniambia nije leo
(jana) tarehe 29 ili nianze mazoezi, nimeingia humo ndani, mapokezi
wameniambia niondoke maana hakuna huduma.
Eti niangalie vyombo vya habari mgomo ukiisha ndio nije, sijui niende
wapi, kwa nini madaktari hawana huruma jamani,” alisema Rwechungura
huku akilia.
Eneo la Hospitali ya Muhimbili tofauti na siku nyingine, jana
lilikuwa kimya, hakukuwa na pilikapilika za wagonjwa wala wahudumu na
baadhi ya wagonjwa walionekana kuingia na kutoka huku wengine
wakisikitika kwa kuelezwa kuwa hakuna huduma.
Simu za Jumaa Almasi, Ofisa Uhusiano wa MOI ziliita bila majibu na
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaeshi alikataa kuzungumza na
waandishi akidai hajui kama mgomo upo au haupo na kuwataka wamtafute
jana jioni. Alipotafutwa simu haikuwa hewani.
Bugando, Sekou Toure zatimua 63
Wakati hali ya huduma ikizorota Muhimbili, Mkoa Mwanza madaktari 63
waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo kazini katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando na ya Sekou Toure wametimuliwa kutokana na mgomo na kurejeshwa
wizarani, anaripoti Grace Chilongola.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk. Charles Majinge
alisema inawarejesha wizarani madaktari 47 baada ya kukataa kurejea
kazini.
“Hospitali ya Bugando ina jumla ya madaktari 47 walio katika mafunzo
kazini ambao tumewarudisha wizarani wamegoma kurejea katika mafunzo
kazini, na sasa kwa kuwa walitoka wizarani kuja hapa kwetu kwenye
mafunzo, basi tunawarejesha huko walikotoka,” alisema Dk. Majinge.
Alisema kuwa kuondoka kwa madaktari hao, waliokuwa katika mgomo
kutaathiri utendaji wa utoaji huduma, kwa muda mpaka baadaye
watakapojipanga na kupata ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, madaktari
16 waliopo kwenye mafunzo kazini wamesimamishwa pia kwa agizo la Wizara
ambao waliamuliwa kuchukua barua zao na kuondoka katika eneo la
Hospitali ya Sekou Toure.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Valentine Bhangi akielezea kutimuliwa kwa
madaktari hao alisema kwa vile madaktari hao waliletwa na wizara hapo
kwa ajili ya mafunzo kazini, wamerejeshwa huko walikotoka kwa hatua
zaidi.
Dodoma mgomo baridi
Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wameingia kwenye mgomo
baridi hali ambayo inasababisha wagonjwa kutopata huduma kwa wakati huku
wengine wakitaka Serikali itazame hatima ya wananchi wa kipato cha
chini ambao hawana uwezo wa kwenda hospitali za kulipia, anaripoti Sifa
Lubasi.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel
Mpuya alisema kuwa hakuna mgomo hospitalini hapo na wanaendelea na kazi
kama kawaida.
Mwandishi wa habari hizi alifika hospitalini hapo jana na kushuhudia
msululu mrefu wa wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya kumuona daktari ambapo
ni daktari moja tu alikuwa akitoa huduma huku vyumba vingine vya
madaktari vikiwa havitoi huduma yoyote.
Mmoja wa wananchi hao, Zakaria Daudi ambaye ni mkazi wa Chamwino
katika Manispaa ya Dodoma alisema kuwa, hali ya huduma sio nzuri kwani
wanalazimika kusubiri kuingia kwa daktari muda mrefu bila ya mafanikio.
“Tangu juzi namleta hapa mke wangu bado hajapata huduma napigwa tu
kalenda bila huduma yoyote kama wamegoma waseme ukweli,” alisema. Kwa
upande wake, mkazi wa Nkuhungu, Kunze George alimtaka Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma kuwa mkweli kuwa kuna mgomo na si kusema hali shwari
wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma.
Wakati huohuo, afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari wanaoongoza
mgomo, Dk Steven Ulimboka, imeelezwa kuwa inaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jopo la Madaktari wanaomtibu daktari huyo,
Profesa Joseph Kahamba, wanaendelea kumtibu akiwa chini ya uangalizi wao
katika kitengo cha wagonjwa mahututi.