NAIBU Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, ameitaka
serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwachunguza na kuwachukulia hatua
zikiwemo kuwataja, kuwashtaki na kuwafilisi mafisadi wanaodaiwa kupora
fedha za miradi ya gesi, madini na petroli na kuzihifadhi kwenye
akaunti nchini Uswisi.
Aliyasema hayo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) na kuongeza kuwa kuna wizi wa fedha za serikali zaidi ya
sh bilioni 300 ambazo baadhi ya watumishi wa serikali wamepewa kama
hongo na wawekezaji wa sekta hiyo.
Wakati Zitto akisema hayo, Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Mambo ya Nje na Usalama, Edward
Lowassa, ameitaka serikali kutolea maelezo madai ya kufichwa kwa
shilingi bilioni 300 katika benki mbali mbali nchini Uswisi ambazo
zinadaiwa kuwekwa na wanasiasa na watu wa kada mbalimbali nchini.
Akizungumza Bungeni jana Zitto aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, vyombo
vya usalama na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)
kuchunguza na kuchukua hatua mara moja.
Zitto aliitaka serikali kuiga mfano wa India ambayo ilipata mkasa
kama huo na kuwataja watuhumiwa, kuwachunguza na kuzirudisha serikalini
pesa zilizoonekana kuwa zilipatikana kinyume cha sheria.
Alitaka serikali ihakikishe kuwa watuhumiwa hao wanatajwa,
wanachukuliwa hatua na pesa zinarudishwa nchini huku akionya kuwa
inashangaza hata kabla ya miradi kuanza watu wameanza ufisadi na
kupora mali za umma.
Gazeti la The Guardian la Jumamosi iliyopita lilichapisha taarifa za
ufisadi huo uliofanywa na Watanzania sita waliopokea hongo kutoka
makampuni yanayotafiti gesi, madini na petroli na kuweka pesa zao
Uswisi.
Kwa upande wake Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu maswali
ya waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wa kamati ya ulinzi na
usalama juu ya kuwepo kwa fedha hizo katika mabenki hayo ya Uswisi huku
Watanzania wakiendelea kutaabika kwa mfumko mkubwa wa bei.
Akizungumzia kuhusu hilo, Lowassa ambaye hakutaka kuzungumzia kwa
kirefu alisema hata wao kama kamati wamesoma taarifa hizo kwenye
magazeti na kwamba wenye majibu mazuri kuhusiana na suala hilo ni
serikali.
Hoja ya Zitto
Aidha Zitto katika hoja yake hiyo pia akizungumzia mjadala wa
mafuta na gesi alishauri suala hilo lisiwe la Muungano kila upande
uachiwe jukumu la kutafuta na kuchimba nishati hizo.
“Kila upande wa Muungano ushughulikie gesi na mafuta yake hakuna sababu ya kuchelewesha suala hili,” alisema.
Akiunga mkono hatua hiyo mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy,
aliitaka serikali kutoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya
Watanzania walioingia mikataba ya rada.
Alisema Waingereza waliwashtaki watuhumiwa wake na kurudisha fedha ya
rada kwa Tanzania na kuhoji serikali nayo imefanya nini kwa
watuhumiwa walioingia mikataba mibovu ya rada humu nchini?
Alitaka waliofilisi mashirika ya umma kama Shirika la Ndege –ATC,
Reli na Bandari wakamatwe, washtakiwe, kufilisiwa na kunyongwa hata
kama walifanya hivyo miaka 20 iliyopita.
Aliliambia Bunge kuwa hata kama walioua mashirika wamekufa pingu
zipelekwe kwenye makaburi yao na kusisitiza kuwa dawa ya walioua
mashiriki ya umma ni kuuawa.
Alipendekeza wauliwe kwani wamewaua Watanzania kwa kuwaibia stahili
zao kama dawa zilizokuwa ziwatibu na kusababisha vifo vyao.
Aliongeza kuwa sheria za Tanzania ni mbaya kwani zinawalinda wezi na
kuwatetea mafisadi na kuiponda serikali kuwa ina masikio lakini
haisikii ina pua lakini hainusi.
Aliishangaa miradi ya usafiri jijini Dar es Salaam iliyotangazwa na
Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli ya kujenga vituo saba vya usafiri wa
boti kutoka Bagamoyo hadi Feri na kusema huo ni ubadhirifu wa fedha za
umma.
Aliitaka serikali kuwashughulikia watuhumiwa wanaodaiwa kuhifadhi
fedha za rushwa ya gesi na petroli kwenye benki za Uswisi na yenyewe
kukaa kimya.
Aliongeza kuwa Takukuru imeshindwa kazi na inashangaza kuona kuwa
inawaambia wananchi wawaletee majina ya wala rushwa wakati wanawajua na
watu wanaiba fedha za umma na kujenga maghorofa na kumiliki mali za
wizi.
Alisema maofisa wa Takukuru wanawachuuza wananchi wanaowapa majina ya
wala rushwa kwa kutoa taarifa kwa watuhumiwa waliotajwa kisha kuwaomba
rushwa.
Alikataa kuunga mkono bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maelezo
kuwa inaifanya mikoa mingine kuwa peponi na mingine kuwa motoni.
Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia taarifa yake
kilirudia kutoa wito kwa Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba
kuagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa rada ambao iliwataja
kwa nyakati mbalimbali ikiwemo katika orodha ya mafisadi (list of
shame) Septemba 15 2007 katika Uwanja wa Mwembeyanga.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na
Mkurugenzi wa Mambo ya Habari wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kutokana
na sheria za usiri za Uswisi, wanaitaka serikali inayoongozwa na CCM
kuwasiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuanza mchakato wa kuwezesha
mahakama za nchi hiyo kutoa ruhusa kutolewa kwa taarifa zote kuhusu
wenye akaunti hizo na makampuni yaliyoweka kiasi hicho cha fedha ili
hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na
Sheria za Kimataifa.
“CHADEMA inatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua
kamili za kisheria na mali zao kufilisiwa kunafanya taifa kuendelea na
ufisadi ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na sasa
tuhuma mpya za ufisadi kwamba kuna vigogo wenye kiasi cha bilioni 303
kwenye akaunti Uswisi ambazo zinadaiwa kuwekwa na makampuni ya madini,
mafuta na gesi asili,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha chama hicho kimekumbusha kuwa katika orodha yake ya mafisadi
iliwataja pia kwa majina viongozi wa serikali ambao waliingia mikataba
ya kifisadi ya madini na rasilimali nyingine za taifa kutolewa kwa
taarifa hizo za benki za nje kutathibitisha ukweli na pia kubainisha
watuhumiwa wengine zaidi.
Pamoja na hilo imeitaka serikali inayoongozwa na CCM kuzingatia mpango
kati yake na serikali ya Uingereza kupanga matumizi ya fedha kiasi cha
shilingi bilioni 72.3 za rada zilizorejeshwa baada ya kubainika
zilizochotwa kifisadi na kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.
Wakati huohuo, CHADEMA imeshangazwa na uamuzi wa serikali inayoongozwa
na CCM kubadilisha mpango wa kujenga nyumba za walimu kinyume na mpango
huo wakati huu ambapo serikali iko katika mgogoro na walimu kutokana na
kutowatimizia madai yao ya msingi ikiwemo nyongeza ya mishahara, kulipa
madeni na kupunguza kodi kwenye mishahara.
Chama hicho kimeitaka serikali kukumbuka kwamba mpango huo ulikuwa
moja ya ushahidi muhimu uliotolewa mahakamani kumshawishi jaji kutoa
uamuzi wa kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE kwamba fedha hizo
zingetumika kununua vitabu 4.4 milioni kwa ajili ya wanafunzi, vitabu
192,000 Kwa ajili ya walimu kufundishia, madawati 200,000, kujenga
nyumba 1,196 za walimu wa shule za msingi vijijini, kujenga vyoo 200,000
kwenye shule za msingi.
Kadhalika imeonyesha kuguswa na taarifa kwamba zabuni ya kuchapa
vitabu hivyo imetolewa kwa kampuni ya Kiingereza ya Oxford University
Press hali ambayo itafanya sehemu kubwa ya fedha hizo kurejea hukohuko
Uingereza.
source: Tanzania Daima.