PRESS RELEASE- taarifa ya Jumuiya ya madaktari
TAARIFA YA JUMUIYA YA MADAKTARI KUHUSU MAAMUZI YA SERIKALI KUFUATIA
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YAWA TANZANIA TAREHE 1 JULAI 2012 JUU YA
MGOGORO KATI YA SERIKALI NA MADAKTARI
Utangulizi
Jumuiya ya madaktari imepokea kwa masikitiko hotuba ya Serikali kuipitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaina
Ifahamike kuwa mgogoro huu umedumu kwa takribani miezi saba bila kupatikana kwa suluhu ya dhati baina ya pande mbili.
Kutokana na Hotuba iliyotolewa na Mhe Rais ya tarehe 01.07.2012 kwa
wananchi wa Tanzania kupitia vyombo vya habari, Kamati ya Jumuiya ya
Madaktari inapenda kutoa ufafanuzi katika mambo yafuatayo;
Ni
wazi ikafahamika kuwa mjadala juu ya hoja/madai ya Madaktari kwa mara
kadhaa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa
ukizuiwa na Mhe. Spika wa Bunge kwa kigezo kuwa suala hilo liko
mahakamani, je ni sahihi Serikali kutoa maamuzi juu ya suala hilo?
Pia, kuhusu suala la kutekwa, kupigwa na kuumizwa kikatili kwa Dr.
Ulimboka Stephen, Serikali kupitia Jeshi la polisi lilitangaza kuwa Tume
imeundwa ili kuchunguza suala hilo mpaka sasa hakuna mwenye uwezo wa
kuthibitisha kuwa Serikali haijahusika moja kwa moja, je ni sahihi kwa
Mhe. Rais kutamka waziwazi kuwa Serikali haihusiki kwa namna yoyote ile
hata kabla ya tume kutoa ripoti yake ya uchunguzi? Hii itatoa uhuru kwa
tume ambayo kimsingi imeundwa na Serikali?
Nini dhamira ya Madaktari katika kusuluhisha Mgogoro huu
Kwa kuamini kuwa Madaktari ni upande muhimu katika kufikia suluhu ya
dhati, tulishiriki katika meza ya ya Majadiliano kwa takribani miezi
mitatu na jumla ya vikao sita vilifanyika, katika vikao hivyo takribani
vikao vine kati ya vikao sita (asilimia 66% ya vikao na muda wa vikao)
tulijadiliana juu ya Uboreshaji wa huduma ya afya kwa Watanzania, ni
masikitiko yetu kuwa Ripoti ya Ufafanuzi juu ya Hoja/Madai ya Madaktari
ya tar 31 Juni 2012, Taarifa ya Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Taarifa ya Waziri Mkuu ndani ya Bunge na hata hotuba ya Rais
haikuzungumzia chochote ni kwa jinsi gani serikali itaboresha huduma za
afya kwa Watanzania.
Pia tulijadiliana kuhusu Uboereshaji wa
Mazingira ya Kazi, ambapo tuliishauri Serikali kupitia kamati ya
Majadiliano kuwa ni muhimu kurejesha motisha kwa watumishi wa sekta ya
afya kwa kurudisha posho mbalimbali ambazo ziliondolewa.
Kuhusu
suala la mshahara, tulishauri serikali iwe wazi kuhusu uwezo wake wa
kulipa mishahara, cha kushangaza ni kwamba Serikali imekuwa ikitoa
taarifa tofauti juuya ongezeko hilo mfano: Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii amelihutubia Bunge kuwa ongezekoni 15%, Hotuba ya Mhe. Rais
ametoa ongezeko la 20%. Ripoti yaWataalamu iliyotokana na Kamati ya
Waziri Mkuu ilitoa pendekezo la 25%. Je, nia ya Serikali iko wapi?
Wakati viongozi wa Serikali wakitoa taarifa zinazotofautiana, Ripoti ya
Ufafanuzi wa madai/hoja ya Madaktari iliyotoka na Majadiliano sisi
tukiwa wajumbe haikutoa pendekezo (ofa) yoyote juu ya ongezeko la
mshahara.
HITIMISHO
Kwakuwa kuendelea kufanya kazi
katika mazingira haya ndugu zetu Watanzania wazalendo wengi wamepoteza
maisha kutokana na ukosefu wa vifaa tiba na madawa.
Na kwakuwa
tumefanya kazi kwa miaka mingi sana tukishuhudia haya tunadhani muda
umefika wa kubadilisha hali hii na kuwasaidia ndugu zetu Watanzania.
Na kwakuwa Serikali imeshindwa kuweka mazingira ya kazi kuwa bora na kuwezesha huduma bora kwa wananchi na watoa huduma.
Hivyo basi, Madaktari Bingwa tumeamua kuacha kufanya kazi ambayo
haiendani na kiapo cha Madaktari mpaka hapo Serikali itakapokubali
kurejesha interns wote na kufungua meza ya Majadiliano yenye nia ya
dhati ya kumaliza mgogoro.
Na Wawakilishi
Kamati ya Jumuiya ya Madaktari
Imesainiwa na
Katibu Jumuiya ya Madaktari.