Tuesday, September 24, 2013

Waathiriwa wa shambulizi la Westgate



Ruhila aliolewa mwaka jana
Takriban watu 62 wameuawa kwenye mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya dhidi ya jengo la kifahari lenye maduka zaidi ya themanini la Westgate.

Ruhila Adatia-Sood

Ruhila Adatia-Sood na mumewe Ketan Sood Ruhila Adatia-Sood walioana tu mwezi Januari mwaka jana.
Ruhila, alikuwa katika ghorofa ya juu ya duka la Westgate ambako alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wameandaa mashindano ya upishi kwa watoto.
Alikuwa ameolewa na Ketan Sood, aliyefanya kazi na shirika la USAid mjini Nairobi mwezi Januari mwaka 2012,na harusi yake ilitajwa kuwa harusi ya kiswahili ambayo ilisherehekewa kwa siku tatu.
Alikuwa mjamzito na mimba ya miezi sita alipofariki.
Kulingana na ripoti Adatia-Sood alikimbizwa hospitalini , lakini alifariki baada ya kuwasili kutokana na kuvuja damu nyingi.
Alisifika kote nchini kwa moyo wake mzuri wa kuwafanya watu kutabasamu daima.

Polisi wakikabiliana na wanamgambo hao waliokuwa wameteka jengo la Westgate
Kwenye ukurasa wake wa Twitter alijitaja kuwa mpenda chakula na mtu mwenye kufurahia michezo ya kusisimua.
Alisomea katika chuo kikuu cha Rhodes nchini Afrika Kusini , na dada zake watatu wamemtaja kama mtu mwenye ari kubwa maishani.
Pia alikuwa mtangazaji wa kituo cha redio cha East FM na pia alitangaza habari kwenye kituo cha televisheni ya Kiss.
Magaidi waliwarushia magurunedi Rahila na mtangazaji mwenzake pamoja na watoto waliokuwa ndani ya jengo hilo lakini Ruhila hakuponea. Mwenzake Kamal Kaur, pia mtangazaji wa redio alikuwa ameambatana na watoto wake ambao walifyatuliwa risasi ingawa ziliwakosa na kumgonga mtoto aliyekuwa karibu nao. Wao walijeruhiwa miguuni.
Kaur na wanawe walifanikiwa kukimbilia usalama wao.

Mbugua Mwangi and Rosemary Wahito

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pia aliwapoteza jamaa zake katika shambulizi hilo. Mbugua Mwangi ni mpwa wa Kenyatta na alikuwa na mchumba wake Rosemary Wahito wakati waliposhambuliwa kwa risasi na kuuawa papo hapo.
Akihutubia taifa, Kenyatta alisema kuwa, "ninamuomba Mungu awape utulivu wakati sote tukikumbwa na msiba huu na ninajua mnachokihisi hasa ikiwa umempoteza jamaa wako katiakshambulizi hili baya.''
Kulingana na taarifa ya jarida la nchini Ireland, mamake Mwangi, Catherine Muigai Mwangi, ndio alikuwa tu amerejea kutoka Dublin ambako alikuwa balozi wa Kenya kwa miaka sita .
Dadake mkubwa Rais Kenyatta Christine Wambui Pratt pia alikuwa katika jengo hilo lakini alifanikiwa kunusuru maisya yake.

Mitul Shah


Mitul Sha alipenda sana soka
Mitul Shah Mitul Shah alikuwa mkuu wa timu ya soka ya kampuni yake ambayo inacheza katika divisheni ya pili.
Afisaa mkuu mtendaji wa mauzo katika kampuni ya Bidco, ambayo hutengeza mafuta ya kupikia, Mitul Shah alikuwa katika ghorofa ya juu zaidi ya jengo hilo.
"Alifariki akijaribu kuwaokoa watoto waliokuwa wamekwama ndani ya jengo hilo. Kwa marafiki wa Mitul, alifariki kama shujaa .
Rafiki zake wamemtaja kama shabiki sugu wa Manchester United.
Pia alikuwa mwenyekiti wa timu ya soka ya Bidco.

Joyti Kharmes Vaya na Maltiben Ramesh Vaya ambao ni wifi


Mazishi ya Joyti Kahrmes Vaya na Maltiben Ramesh Vaya
Joyti Kharmes Vaya alikuwa na umri wa miaka 37 mwenye watoto watatu, ambaye mumewe alifanya kazi katika benki ya Victoria Commercial bank.
Maltiben Ramesh Vaya alikuwa na miaka 41 , mama wa watoto wawili aliyefanya kazi katika Benki ya Baroda.
Wawili hao walikufa kutokana na majeraha waliyopata, kutoka na risasi

Kofi Awoonor

Raia wa Ghana mwenye umri wa miaka 78 malenga anayesifika sana. Anasifika nyumbani kwao kama mwandishi ambaye vitabu vyake vinatumiwa katika shule nyingi nchini Ghana.
Alikuwa mjini Nairobi kushiriki hafla ya Storymoja na alitarajiwa kutumbuiza watu siku ya Jumamosi.
Alisifika kwa nyimbo na mashairi yake mapema miaka ya sitini.
Miaka ya sabini alifunza katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Marekani na kurejea Ghana mwaka 1975 kuchukua wadhifa wa mwalimu wa lugha ya kiingereza katika chuo kikuu cha Cape Coast.
Katika muda wa miezi kadhaa, alikamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya njama ya uhaini wakati wa utawala wa kijeshi wa Kanali Ignatius Acheampong.
Mwanawe Awoonor alikuwa naye wakati wa shambulii hilo mjini Nairobi na alipigwa risasi mkononi wakati wa shambulizi hilo.


Chanzo: BBC SWAHILI

Vikosi vya Kenya 'vimedhibiti' Westgate


Moshi mkubwa ulioonekana ukifuka kutoka katika jengo la Westgate Jumatatu jioni Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.

Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.

Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.

Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia

Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota. Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.

Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.


Wanajeshi wa Kenya katika juhudi za kuokoa mateka na kukomboa jengo la Westgate Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo , lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.

Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.

Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.

"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku

Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.

Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.

Monday, September 23, 2013

FUATILIA MATUKIO YA KENYA LIVE HAPA





FUATILIA MATUKIO YANAYOENDELEA KENYA LIVE GONGA HAPA

Fuatilia zaidi hapa kuhusu yanayoendelea Kenya

Nairobi mall: Kenyan forces try to free final hostages>/a>

Fahamu zaidi kuhusu Al shabaab, ni nani hasa?


Wapiganaji wa Al Shabaab
Kundi la wapiganaji wa kisomali la al-Shabaab,limevamia jumba la kifahari lenye maduka na mikahawa nchini Kenya. Al Shabaab lenya mizizi yake nchini Somalia, limeweza kuondolewa kutoka miji mikubwa ya Somalia ikiwemo Mogadishu na sehemu zengine za Somalia , ingawa bado linasalia kuwa tisho kubwa kwa kanda nzima. 


Al Shabaab ni nani?
Jina Al-Shabab linamaanisha Kijana kwa lugha ya kiarabu. Kundi hilo liliibuka kama tawi la vijana la muungano wa mahakama za kiislmau ambao baadaye ulivunjika mwaka 2006, wakati ilipopigana na wanajeshi wa Ethiopia waliokuwa wameingia nchini Somalia kuunga mkono serikali iliyokuwa dhaifu.

Kuna taarifa chungu nzima kuhusu wapiganaji wa kiisilamu wanaokwenda Somalia kupigania Al Shabaab.

Kundi hilo limeweka sheria kali za kiisilamu katika maeneo ambayo linadhibiti ikiwemo kupigwa kwa mawe hadi kufa wanawake wanaodaiwa kufanya uasherati pamoja na kuwakata wezi mikono. 


Je Al Shabaab linadhibiti sehemu gani ya Somalia?
Ingawa kundi hilo limepoteza udhibiti, wa miji mikubwa, bado linakita mizizi katika maeneo ya mashinani.

Lililazimika kuondoka katika mji mkuu Mogadishu, mwezi Agosti mwaka 2011 na pia kuondoka katika mji wa bandarini wa Kismayo mwezi Septemba mwaka 2012.

Kismayo ulikuwa mji muhimu kwa kundi hilo, ambao ulikuwa unawezesha bidhaa kuwafikia wapiganaji wa kundi hilo pamoja na kuwatoza watu ushuru kwa shughuli zao.


Hizi ni silaha za Al Shabaab walizonasa wanajeshi wa AU

Muungano wa Afrika, ambao unaunga mkono juhudi za majeshi ya serikali, ulisherehekea ushindi huo ingawa al-Shabab hunfanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kujitoa mhanga mjini Mogadishu na kwingineko.

Wadadisi wanaamini kuwa al-Shabab limeanza kufanya mashambulizi ya kuvizia baada ya kushindwa na majeshi ya Muungano wa Afrika wanaotumia nguvu dhidi yao.

Lakini linakabiliwa na tisho kubwa kutoka kwa wanajeshi wa Kenya walianza hatarakti zao dhidi ya kundi hilo kuanzia mwaka 2011.

Kenya ilituhumu wapiganaji wa al-Shabab kwa kuwateka nyara wanajeshi wake pamoja na watalii na sasa wamekuwa katika msitari wa mbele kupambana na kundi hilo la kigaidi.

Wakati huo, wanajeshi wa Ethiopia waliweza kukabiliana na wapiganaji hao na kudhibiti miji ya Beledweyne na Baidoa.


Nani kiongozi wa al-Shabab?
Ahmed Abdi Godane ndiye kiongozi wa kundi hilo. Anajulikana kama Mukhtar Abu Zubair, na anatoka katika jimbo la Somaliland.

Kumekuwa na taarifa za mgawanyiko katika kundi hilo, ambazo hata hivyo zinapingwa vikali na kundi lenyewe. Inaarifiwa kuwa uongozi wake unapingwa, na wanachama wanaotoka maeneo ya Kusini na ambao ni wengi katika kundi hilo. Inakisiwa idadi yao ni kati ya wanajeshi 7,000 na 9,000.

Bwana Godane huwa haonekani hadharani . Mtangulizi wake Moalim Aden Hashi Ayro, aliuawa katika shambulizi lililofanywa na Marekani mwaka 2008. 


Nini uhusiano wa kimataifa wa kundi hilo?


Al Shabaab wakifanya mashambulizi mjini Mogadishu
Al-Shabab lilijiunga na al-Qaeda mwezi Februari mwaka 2012. Katika ujumbe wa Video, kiongozi wa al-Shabab Ahmed Abdi Godane alisema anaahidi kuunga mkono kingozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri.

Makundi hayo mawili yamekuwa yakifanya kazi kwa pamoja, na raia wa kigeni wamekuwa wakiunga mkono kundi hilo, na hata kuwasaidia katika harakati zao za mapigano.

Mwaka jana maafisa wa al-Shabab waliambatana na mtu aliyesema ni mwanachama wa al-Qaeda na kumtambua kuwa raia wa Marekani Abu Abdulla Almuhajir alipokuwa anatoa msaada wa chakula kwa waathiriwa wa njaa.

Maafisa nchini Marekani wanaamini kuwa wapiganaji wa Al Qaeeda ambao hawajahusina sana na mashambulizi nchini Afghanistan na Pakistan kufuatia mauaji ya kiongozi wao,Osama bin Laden, wapiganaji wake wengi wanakwenda kutafuta hifadhi nchini Somalia.

Milio ya risasi yasikika ndani ya Westgate

Jeshi la Kenya linasema kuwa limedhibiti jengo hilo ingawa hali bado ni mbaya
Huku hali ya mshikemshike ikiendelea kushuhudiwa katika jengo la Westgate lenye maduka, ufyatulianaji risasi umesikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na mikahawa zaidi ya themanini.
Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia ambao idadi yao haijulikani. Walikuwemo ndani ya jengo wakiendelea na shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.
Inaarifiwa kuna maiti kumi katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.
Inaarifiwa wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wangali ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi umesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.
Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora.
Wakenya waliofanikiwa kuondoka katika jengo la Westgate kwa usaidizi wa polisi

Rais Kenyatta amesema kuwa jueshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.
Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ni ya ati ati katika eneo la shambulizi.
Awali jeshi la Kenya lilisema limeweza kudhibiti jengo hilo lote ingawa bado limetaja hali kuwa tete mno hasa katika kujaribu kuwaokoa mateka waliosalia ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa watu 69 wamefariki katika shambulizi hilo la Al Shabaab kufikia sasa huku 175 wakijeruhiwa. Baadhi wametibiwa na kuondoka hospitalini. Baadhi ya majeraha waliyopata ni majereha ya risasi na kutokana na guruneti ambalo Al shabaa waliwarushia wale waliokuwa ndani ya mikahawa siku ya Jumamosi.
Kundi hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo kutokana na hatua ya kenya kupelekeka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji hao.

Wakati huo huo makamu wa rais wa Kenya William Ruto amepewa ruhusa na mahakama ya ICC kurudi Kenya kuhudhuria shambulio la westgate

Chanzo: BBC-Swahili 

Thursday, September 19, 2013

Mwizi wa magari akamatwa jijini Dar es salaam

 
 Jengo ambalo linadaiwa ndiyo kiwanda hatari cha kubadilisha magari ya wizi, kimefumuliwa na mmiliki wake sasa hivi yupo nyuma ya nondo akingoja kufikishwa mahakamani.

Kigogo wa magari ya wizi, Benovilla Luhanga baada ya kunaswa.

Benovilla Luhanga, 43, ametajwa kuwa ndiye mmiliki wa kiwanda hicho na siku ananaswa, alikutwa na magari ya kihafari matano ambayo yote inadaiwa ni ya wizi.
Vilevile, Luhanga alikutwa na Bajaj moja ambayo imedaiwa nayo ni ya wizi na kwamba alikuwa tayari ameshaibadili rangi.
Luhanga alikamatwa akiwa na mkewe ambaye jina lake halikupatikana mara moja.


Moja ya gari alilokutwa nalo mtuhumiwa.

Kigogo huyo na mkewe, wanaishi ndani ya nyumba hiyo iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, kwa nje huonekana kama gereji lakini ndani ni makazi ya watu na shughuli za ubadilishaji magari, Bajaj na pikipiki hufanyika humo.
Luhanga na mkewe walikamatwa baada ya polisi kuvamia kiwanda hicho, saa 5 asubuhi lakini mchakato wa ukamataji ulikamilika saa 10 alasiri.
Mchakato wa kuwakamata uliwagharimu polisi jumla ya saa 5 kukamilika kwa sababu ilibidi kufanya upekuzi wa hali ya juu kwenye kiwanda hicho ili kubeba kila kitu kilichoonekana ni cha wizi.
Magari yote yaliyokutwa kwenye kiwanda hicho pamoja na Bajaj moja, ilidaiwa ni mali za wizi huku tayari yakiwa yameshabadilishwa rangi na kufungwa namba feki za usajili, isipokuwa gari moja.


Gari aina ya Nissan Navara lenye thamani ya shilingi milioni 45 alilokutwa nalo mtuhumiwa.

ZA MWIZI ZILIVYOTIMIA
Habari zinaeleza kuwa kuwa kiwanda hicho kiligundulika kutokana na kijana mmoja ambaye aliwahi kuibiwa gari aina ya Toyota Canter, Goba, Dar, hivi karibuni.
Imebainika kuwa kijana huyo baada ya kuporwa gari hilo ambalo yeye alikuwa ameajiriwa kama dereva, maisha yalimwendea kombo kabla ya kwenda kwa Luhanga kuomba kazi, akidhani ni gereji.
Chanzo chetu kilitamka kuwa akiwa ndani ya kiwanda hicho, kijana huyo aliliona hilo Toyota Canter ndani ya uzio wa kiwanda hicho, hivyo kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kawe, Kinondoni, Dar.
“Baada ya kuripoti, askari walifuatilia na kukuta kweli kuna gari aliloibiwa kijana huyo na walipofanya upekuzi wakayakuta magari mengine matano yaliyoripotiwa kuibwa,” kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema, polisi waliweza kubaini kuwa magari hayo baadhi yake yalibadilishwa rangi na kupakwa nyeusi huku namba za usajili nazo zikiwa zimebadilishwa.


Nyumba anayoishi kigogo huyo.

KAMATAKAMATA IKAANZA
Polisi baada ya kugundua wizi huo, kamanda aliyeendesha oparesheni hiyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, aliamuru Luhanga na mkewe wakamatwe na magari yaliyokuwa na uwezo wa kutembea yaliendeshwa, mengine yalikokotwa kwa ‘breakdown’ hadi Kituo cha Polisi Kawe.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa watuhumiwa hao tayari wamefunguliwa jalada katika kituo hicho kwa namba KW/RB/8194/2013 WIZI WA MAGARI.
Waandishi wetu walipofika kituoni Kawe Jumapili iliyopita, walikuta ndugu sita wa Luhanga wakihaha kutaka kuwawekea dhamana.

 

MAGARI YALIYOIBWA
Magari yaliyoibwa ni aina ya Nissan Navara lenye thamani ya shilingi milioni 45, lililokutwa na kibao cha usajili namba T519 BNP.
Lingine ni Toyota Harrier, ambalo thamani yake ni shilingi milioni 30. Hili lilikutwa na namba za usajili T 924 AXB, wakati kuna Toyota Rav4 new model, lenye thamani ya shilingi milioni 40 ambalo lilikutwa na namba T 581 BBL.
Gari lingine ni Toyota Canter, vilevile kulikuwa na Rav4 new model nyingine lenye rangi ya kijivu, hili lilikuwa limeng’olewa namba zake halisi bila kuwekewa nyingine.
Rav4 hilo ambayo halikufungwa namba, imeelezwa lilikuwa halijabadilishwa rangi, kwani kwa kawaida yale yanayoporwa na kuingizwa kiwandani humo, hupakwa rangi nyeusi. OFISINI KWA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, ACP Camillius Wambura, hakuweza kupatikana licha ya waandishi kufika ofisini kwake. Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa jeshi hilo, alithibitisha kutokea kwa tukio.
“Tukio hilo lipo na tunaendelea na uchunguzi,” alisema ofisa huyo huku akiomba asiandikwe jina lake gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo.

Padri aliyemwagiwa tindikali kusafirishwa nje kwa matibabu


Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Cheju Zanzibar, akisaidiwa na Frateri, Richard Haki kupumzika kitandani baada ya kuzungumza na waandishi katika katika Wodi ya Kibasila iliyopo katika Hosipitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijni Dar es Salaam .

Huenda Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae Zanzibar, Anselmo Mwang’amba aliyemwagiwa tindikali siku tano zilizopita, akasafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kutokana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako amelazwa, kudaiwa kushindwa kumtibu.

Akizungumza jana, padri huyo alisema anategemea kwenda nje ya nchi kwa matibabu japokuwa bado hajajua nchi atakayopelekwa kwa kuwa anasubiri ushauri wa madaktari.

Alisema pamoja na matibabu aliyoyapata lakini bado anasikia maumivu katika majeraha ya usoni, mikononi na kifuani.

Aliisihi Serikali kukomesha na kuwakamata wahusika wa vitendo hivyo vilivyokithiri vya kuwamwagiwa watu tindikali bila sababu visiwani humo.

Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka katika chanzo kilichopo ndani ya hospitali hiyo kimeeleza kuwa, padri huyo anatarajia kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu kwani inadaiwa majeraha yake yameshindikana kutibiwa nchini, japokuwa bado haijajulikana ni nchi gani atakayoenda kati ya mbili zinazotajwa na viongozi hao, Afrika Kusini na India.

Alisema madaktari wataalamu waliopo katika hospitali hiyo wana uwezo wa kumponya Padri huyo lakini tatizo lililopo ni ukosefu wa vifaa vya kisasa ndiyo maana wagonjwa wengi wanaomwagiwa tindikali hupelekwa kutibiwa nje ya nchi.

TFDA yakamata kilo 7,500 za samaki wabovu kutoka nje



Pichani:Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza akizungumza na mmiliki wa Kampuni ya Sais Boutique iliyopo Tabata Bima, Dar es Salaam, Sadick Mapolo wakati maofisa wa TDFA walipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maghala ya kampuni hiyo na kubaini samaki wabovu kilo 7,500 aina ya vibua kutoka nje ya nchi waliokutwa wameharibika.

Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imekamata kilo 7,500 za samaki aina ya vibua walioharibika ambao waliagizwa na Kampuni ya Sais Boutique kutoka China, Julai mwaka huu.

Taarifa ya kuwapo kwa samaki hao sokoni iliripotiwa na Gazeti la Mwananchi Jumapili, Jumapili iliyopita ikieleza kuwa walikuwa wakiuzwa kwa bei ya chini na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam.

Akizungumza jana Tabata Bima, Dar es Salaam ambako samaki hao wamehifadhiwa, Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema mamlaka hiyo ilianza kufanya uchunguzi baada ya kuona taarifa kwenye gazeti hili ikiwa ni pamoja na kwenda katika Soko la Feri ili kujua namna wanavyoingizwa nchini.


“Samaki hawa ni wabovu lakini walikuwa wanauzwa mitaani kwa bei ndogo na tulimkuta mmoja wa wasambazaji akiwa na maboksi 10 ya samaki walioharibika baada ya kumbana ndipo alituelekeza anapowanunua ikabidi tuje kwa ajili ya kuhakikisha na ndipo tukawakamata wahusika,” alisema Simwanza.


Alisema bei ya kawaida ya samaki aina ya vibua ni Sh30,000 mpaka Sh35,000 kwa boksi moja la kilo 10 lakini mfanyabiashara huyo alikuwa anawauza kwa Sh23,000.

Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.

Simwanza alisema Kampuni ya Sais Boutique ilipewa kibali cha kuingiza samaki Julai 8, mwaka huu na kwa mujibu wa taratibu za TFDA, kila mfanyabiashara mwenye kibali anapoingiza bidhaa anapaswa aipeleke ikaguliwe kabla ya kuiingiza sokoni ili kujiridhisha kama inafaa kwa matumizi ya binadamu.

Alisema kampuni hiyo ilikiuka taratibu hizo na kuanza kuuza samaki hao kabla hawajakaguliwa na kusema kwamba kufanya hivyo ni kosa kubwa.

Alisema kutokana na kosa hilo, mmiliki wa kampuni hiyo, Sadick Mapolo yuko chini ya ulinzi akisubiri kuchukuliwa hatua za kisheria kulingana na kosa alilofanya huku taratibu za kuteketeza bidhaa hiyo zikifanyika.

Alisema eneo ambalo linatumika kuhifadhia na kuuza samaki hao siyo rasmi kwani halikusajiliwa na TFDA.

“Hapo alipo ana kosa jingine kwani amehifadhi chakula hiki katika sehemu isiyo salama. Angalia kontena zilizowekwa samaki hawa zimezungukwa na gereji. Tulivyofika tulihisi kumehifadhiwa mizigo tu ya kawaida, hatukudhani kama kuna chakula,” alisema Simwanza.

Maofisa wa TFDA walichukua sampuli ya samaki aina ya Kolekole ambao wametokea Yemen waliopo katika kontena ambalo lilikuwa halijaanza kuuzwa lenye kilo 27,500 ili kuwapima.


Akizungumzia sakata hilo, Mapolo alisema samaki hao waliingia nchini kwa kufuata taratibu zote na kwamba kontena lililokamatwa awali, lilikuwa na kilo 22,500 na kilo 15,000 kati ya hizo zilishauzwa kwa watumiaji. “Samaki hawa waliingizwa Julai, mwaka huu wakiwa katika hali nzuri lakini kutokana na matatizo ya umeme na uhifadhi, samaki 500 kati ya 7,500 waliobaki waliharibika,” alisema Mapolo.

Alisema samaki hao walikuwa wanauzwa kwa wafanyabiashara wa Soko la Feri kwa bei ya jumla ya Sh23,000.

Mapolo alisema baada ya kuona baadhi ya samaki wameanza kuharibika alikuwa katika harakati za kuwaondoa lakini kabla ya kufanya hivyo maofisa wa TFDA wakatokea na kumkamata.

JK: Tutakabiliana na wauza ‘unga’ kwa nguvu zote


Rais Jakaya Kikwete

Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.

 California/Johannesburg. Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya dawa ya kukamatwa na dawa hizo.


Rais Kikwete alisema Serikali yake itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume na sheria za nchi.


Alisema hayo juzi usiku alipokutana na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani...“Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria za nchi yetu.”


Masogange na Melisa walikamatwa Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.


Aidha, amesema hayo siku chache baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).


Pia, Agosti 31, mwaka huu, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.


Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.


“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe,” alisema.


Masogange, Melisa wakwama dhamana
Masogange na mwenzake Melisa jana walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama tik).


Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.


Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.


Awahoji akina Masogange


Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema hawakumpa ushirikiano.


Kamanda huyo alisema imebainika kuwa mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.


Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.

Tuesday, September 17, 2013

Mh. Pinda aiomba mahakama kuu kufuta kesi dhidi yake

EA DRIVE (10:00 Alasiri)  Waziri Mkuu Bw.Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam , itupilie mbali kesi iliyofunguliwa dhidi yao na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kuwa kituo hicho hakina haki kuwafungulia kesi hiyo. Mh. Pinda amefunguliwa kesi hiyo kwa kauli yake ya kuruhusu polisi kuwapiga raia wakaidi.

Nini maoni yako? 
Waziri Mkuu Bw.Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam , itupilie mbali kesi iliyofunguliwa dhidi yao na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kuwa kituo hicho hakina haki kuwafungulia kesi hiyo. Mh. Pinda amefunguliwa kesi hiyo kwa kauli yake ya kuruhusu polisi kuwapiga raia wakaidi.

Nini maoni yako?

Friday, September 13, 2013

Kampuni ya Sule's Inc kuachia video ya Mwanambuzi hivi karibuni

Kampuni inayojishughulisha na mambo ya sanaa na uburudishaji ya Sule's Inc &Entertainment, iko mbioni kuachia video ya msaani anaekwenda kwa jina la Wyname, akizungumza na singida connection, Manager wa kampuni hiyo Bw. Suleiman Salum Lyeme, amesema wadau wa sanaa na wenye mapenzi mema na wenye kupenda vitu vya nyumbani wawe tayari kumpokea kijana kwa kuwa video yake ipo katika hatua za mwisho kabisa.
Zifuatazo ni picha za uandaaji wa Video hiyo.


Director, Sule Junior

Wynem akiwa na mrembo

Ass. Director, Alex Nyaganilwa (kulia) akielekeza jambo.

Bandago naye alikuwepo kushoo lav na Wynem.







UGONJWA WA KUOTA NYWELE MWILI MZIMA WAWATESA

 
Ndugu hawa watatu kati ya sita waliozaliwa katika familia moja wameathirika na ugonjwa uitwao kitaalamu werewolf syndrom au kwa jina lingine hypertrichosis. Ugonjwa huu huweza kumfanya mgonjwa kuweza kuota nywele karibu kila sehemu ya mwili wake hasa sehemu za usoni. ni mara chache sana kumpata gonjwa anayeumwa ugonjwa huu kwani wataalamu wanasema kua hutokea kwa mtu mmoja katika watu bilioni moja.

Ndugu hawa wote wanatokea nchini india, wa kwanza anaitwa Savita (miaka 23), wa pili Monisha (miaka 18) na wa mwisho ni Savitri (miaka 18) ambao wote hawa katika maisha yao wamelazimika kutumia dawa ambazo huweza kuwasaidia kupunguza uwezo wa nywele zao kukua kwa kasi.
 
Mama mzazi wa watoto hao anasema chanzo cha ugonjwa huo ni kutoka kwa baba yao, akielezea historia ya maisha yake alisema kua aliolewa kwa kulazimishwa. Na alikuja kujua kua mumewe ni mwathirika wa ugonjwa huo siku ya ndoa yao. Katika kuongezea zaidi amesema kutokana na umaskini walionao wameshindwa kulipia kiasi cha fedha kwa ajili ya watoto wake hao kufanyawa upasuaji, kwani gharama ya upasuaji kwa mgonjwa mmoja ni zaidi ya $7,000 za kimarekani. Mama huyo aliimalizia kwa kuomba msaada ili watoto wake waweze pata msaada wa kufanyiwa upasuaji ili nao siku moja waweze pona na kuolewa.

Tuesday, September 10, 2013

SMZ: Kuifutia usajili meli iliyobeba bangi Italia


Meli ya Gold Star ikiungua moto baada ya watu waliokuwa wakisafirisha bangi kuichoma ili kupoteza ushahidi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekuja juu ikisema itawafungulia mashtaka wamiliki wa meli ya mizigo ya Kampuni ya Gold Star iliyokamatwa juzi ikiwa na tani 30 za bangi nchini Italia ikipeperusha bendera ya Tanzania na kuifutia leseni kwa kulichafua jina la Tanzania kimataifa.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar, alisema kuwa SMZ imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya meli hiyo kubeba dawa hizo za kulevya kinyume cha kibali cha usajili wake.

Omar alisema meli hiyo ilisajiliwa kwa madhumuni ya kubeba mizigo, lakini Kampuni hiyo imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa Mataifa zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa kitendo cha meli hiyo kubeba dawa hizo huku ikiwa na bendera ya Tanzania imeidhalilisha Tanzania hivyo lazima ichukuliwe hatua.

Hata hivyo, alisema ni mapema kuzungumzia lini wataanza mchakato wa kufungua mashtaka kwa kuwa tukio lenyewe lilitokea juzi, hivyo lazima kuwapo na vikao vya watendaji wakuu watakaozungumzia uamuzi huo.

Alisema meli hiyo ilisajiliwa Oktoba 15, mwaka 2011 nchini Dubai katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Meli za Kimataifa Zanzibar, hivyo kisheria ni mali ya Tanzania, lakini wamiliki wake siyo raia wa Tanzania.

Alisema wamiliki wakuu wa meli hiyo ni Marshal Irend waliopo visiwa vya Caribbean, lakini jina la mmiliki pekee halijaweza kufahamika.

Omar alisema katika meli hiyo kulikuwapo na mabaharia tisa, saba wakiwa ni raia wa Syria na wawili wa India.

Alifafanua kuwa mabaharia hao kwanza watashitakiwa nchini Italia na SMZ itapata muda wa kusikiliza utetezi wao ili kufahamu kama hao ndiyo waliopakia dawa hizo au mmiliki wa meli hiyo ndiye aliyepakia ili waweze kumpata mtu wa kumshitaki.

Alisema baada ya kupata ushahidi huo, SMZ itawafungulia mashitaka Mahakama Kuu ya Zanzibar. Alisema mzigo wa dawa hizo zilizokamatwa katika meli hiyo haukutokea Tanzania, na kwamba meli hiyo haifanyi kazi zake katika nchi za Afrika Mashariki bali katika Bahari ya Mediterranean.

“Ningependa Watanzania wajue kuwa ile meli siyo ya Tanzania, bali Tanzania inamiliki kisheria tu kwa kuwa ilisajiliwa katika moja ya ofisi za Tanzania zilizopo Dubai, sisi tunawafadhili tu,” alisema Omar.

Aliwataja mabaharia hao waliokuwa kwenye meli hiyo kuwa ni Ahmad Balkis, Hani Othman, Abdul Ramadhan Jalloul, Ahmad Dalileh, Bachar Alfran, Shadi Suleiman, Mustafa Jumaa, raia wa Syria na Anuj Chauhan na Munishwa wa India.

Katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka huu, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya biashara ya dawa za kulevya yanayowahusisha Watanzania.

Watanzania hao wamekuwa wakikamatwa kwa nyakati tofauti nje ya nchi wakiwa na dawa hizo zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Ilibainika kuwa baadhi yao walikuwa wakipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na dawa hizo na kuilazimu serikali kupitia Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuingilia kati.

Tukio la kwanza lilitokea Julai 5, mwaka huu baada ya wasichana wawili raia wa Tanzania kukamatwa nchini Afrika Kusini wakisafirisha dawa hizo zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8

Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa hizo aina ya Cocaine na Heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6, akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea jijini Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hongkong.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara hiyo haramu ndani na nje ya nchi na kwamba.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara hiyo ya dawa hizo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi katika duru za kimataifa.

Sakata la meli hii linaibuka baada ya lile la Julai mwaka jana ambalo meli za mafuta za Iran zilizua kizaazaa baada ya kubainika kuwa zilikuwa zikipeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kufanikisha biashara ya nishati hiyo.

Kwa mujibu wa sheria, upande wa Tanzania Bara serikali inaweza kutoa usajili wa meli inapobainika umiliki wake ni wa raia wa Tanzania kwa asilimia 50 tofauti na Zanzibar ambako hata Mtanzania akiwa na asilimia moja meli inaweza kusajiliwa na kupeperusha bendera ya Tanzania.

Baada ya kuibuka kwa meli hizo za mafuta, SMZ iliibuka na kutoa taarifa kuwa sheria ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (Maritime Authority – ZMA) iliyoundwa kwa sheria Namba 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na kazi nyingine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa SMZ wa kipindi hicho, Hamad Masoud Hamad, aliwasilisha taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi Julai 2, mwaka jana akithibitisha kusajiliwa kwa meli 10 za Zanzibar ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania, lakini siyo za Iran ila zimetokea Malta na Syprus.


CHANZO: NIPASHE

Wanafunzi 868,030 kufanya mtihani darasa la saba kesho



Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam, wakibeba madawati shuleni hapo jana ikiwa ni maandalizi ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.

Jumla ya wanafunzi 868,030 wa Darasa la Saba nchini, wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu yao ya msingi kesho katika michepuo miwili, wa Kiswahili na Kiingereza.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa, mtihani huo utakaojumlisha masomo matano, utafanyika kwa siku mbili kuanzia kesho hadi kesho kutwa Alhamisi.

Kati ya idadi hiyo ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani huo, wavulana ni 412, 105 sawa na asilimia 47, na wasichana 455, 925 sawa na asilimia 52.52. Jumla ya masomo matano yanatarajiwa kutahiniwa na wanafunzi hao ambayo ni pamoja na Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

Kwa mujibu wa Mulugo, wanafunzi 844, 810 wanatarajia kufanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili, ambao kati yao wavulana ni 400, 335 na wasichana 444,575, huku 22, 535 watafanya kwa lugha ya Kiingereza, ambao wavulana ni 11, 430 ma wasichana 11, 105.

Mulugo alitaja kundi lingine la wanafunzi ambao wanakwenda kufanya mtihani kuwa ni pamoja na lile la wasioona ambao idadi yao ni 88, wavulana 56 na wasichana 32, huku wale wenye uoni hafifu na ambao wanahitaji maandishi makubwa ni 597.

Kati ya watahiniwa hao wenye uoni hafifu, wanaotarajia kufanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili ni 546, wavulana 263 na wasichana 283, na wale watakaofanya kwa Kiingereza ni 51, wavulana 21 na wasichana 30.

Alisema maandalizi yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa fomu maalumu za OMR za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu huku akiwaagiza maafisa elimu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha mazingira yanakuwa tulivu na kuzuia mianya yote ya udanganyifu wa mitihani.

Mulugo pia aliwataka wasimamizi kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

Sambamba na hilo, aliwaasa wanafunzi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watafutiwa matokeo yao yote ya mtihani.


CHANZO: NIPASHE

Job Ndugai ajitetea kuhusu sakata la Mbowe bungeni


NAIBU Spika, Job Ndugai ametetea uamuzi wake wa kuagiza kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akisema alikuwa sahihi.

Mabishano hayo ambayo yalisababisha kuibuka kwa vurugu bungeni yalitokea mwishoni mwa wiki, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo kiongozi huyo wa Bunge aliruhusu mjadala kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uendelee.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisimama kutaka kutoa ufafanuzi juu ya mjadala huo, lakini Ndugai alimzima na kumtaka kukaa chini, jambo ambalo halikumfurahisha Mbowe na kumfanya agomee agizo lake.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Ndugai alitumia muda mwingi kutetea uamuzi wake na kukosoa hoja za watu wanaompinga juu ya uamuzi wake huo.

Ndugai alisema katika kikao hicho, Mbowe alifanya jeuri kubishana na kiti na kueleza kuwa kanuni za Bunge zinasema hakuna mbunge yeyote atakayesimama kuzungumza bila kuruhusiwa na kwamba uamuzi wa kiti ndiyo wa mwisho.

Ndugai alisema wanaomtuhumu kwamba hakutenda haki kumuamuru Mbowe akae chini, wanafanya hivyo kwa vile hawajui kanuni za Bunge.

Ndugai alisema kwa mujibu wa kanuni, ni Rais wa Jamhuri pekee ndiye anayeruhusiwa kulihutubia Bunge kwa wakati anaoona yeye unafaa, lakini si mbunge.

“Hata rais mwenyewe ni lazima amwandikie barua spika, huu ndiyo utaratibu lakini si mbunge au waziri anayeruhusiwa kusimama kwa wakati anaoutaka yeye kuzungumza akaruhusiwa, ni lazima ataomba ruhusa kwa Spika na kama ipo nafasi ya kufanya hivyo Spika atamruhusu, kama haipo hataruhusiwa.

Alipoulizwa kwamba haoni kama alivunja kanuni kwa kumzuia Kiongozi wa Upinzani bungeni wakati kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinatoa upendeleo kwa kiongozi huyo na waziri mkuu ndani ya Bunge, Ndugai alisema:

“Katika vikao vya Bunge, uamuzi wowote wa Spika unakuwa wa mwisho na hauwezi kupingwa na mbunge au waziri yeyote.

“Mbowe nilimuomba kwa heshima sana atupishe kwanza, nilimuelekeza karibu mara tatu…lakini mtu mzima anavunja utaratibu.

“Huyu Mbowe amejivunjia heshima mwenyewe, hata kanisani anayeendesha ibada ni mtu mmoja tu, na wengine wanapaswa kufuata utaratibu.

“Kwanza Mbowe alijitoa mwenyewe kwenye orodha kwa maandishi na ninayo hapa.... yeye na Halima Mdee, sasa alisimama kufanya nini kama sio ujeuri?

“Kanuni anazijua mimi ningemruhusu tu, lakini kwa ujeuri hakufanya hivyo. Kuna taratibu za bunge, mbunge anakaa chini pale Spika anaposimama na wasome kanuni, sasa hapo mjeuri ni nani?

“Tujifunze kanuni haiwezekani mtu yeyote asimame saa yoyote, kila mmoja hawezi kufanya anavyotaka, kuna taratibu zake, kiti kikimuona atapewa nafasi kama ipo na iwapo kiti kikiridhika,” alisema Naibu Spika.

Awatetea askari wa Bunge
Akizungumzia hatua ya kuwaamuru askari wa bunge kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kumtoa Kiongozi wa Upinzani, iwapo kama amevunja kanuni, Ndugai alisema hakuvunja kanuni na kufafanua kila askari aliye kwenye viunga vya bunge yuko chini ya himaya ya kiti.

“Kila askari aliye kwenye eneo la bunge au viunga vya bunge kuanzia polisi, usalama wa taifa na wengine wote siwezi kuwataja hapa, hao wote wako chini ya bunge ni Sajent at Arms.

“Askari polisi wote unaowaona bungeni wanaletwa na RPC Dodoma na wanakuwa chini yetu, hakuna askari aliyetoka nje siku ile…. Ni uongo na hawajui kanuni.

“Uamuzi wa kuita wanausalama ndani ya ukumbi ulikuwa ni uamuzi sahihi, hakuna askari aliyetoka nje ya bunge,” alisisitiza Ndugai.

Msekwa amuunga mkono Ndugai
Naye Spika Mstaafu aliyeongoza Bunge la nane, Pius Msekwa alimtetea Ndugai akisema kuwa haoni kosa lolote lililofanywa na kiongozi huyo wa Bunge.

Msekwa ambaye alipata kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), alisema ni jambo la kawaida ndani ya Bunge, Spika kumuamuru mbunge au waziri kukaa chini pale anapoona inafaa.

“Spika ni sawa na mwenyekiti wa kikao chochote, anayo madaraka ya kuruhusu nani aseme, nani asiseme.

“Tuje bungeni sasa, Ndugai ndiye anayeamua nani aseme, ni sahihi ndiye mwenye mamlaka hayo na ni jambo la kawaida kabisa,” alisema Msekwa.

Akitoa uzoefu wake wa bunge alilokuwa akilisimamia, Msekwa alisema matukio yanayotokea bungeni sasa yamegubikwa na hisia za ujana zaidi na kusisitiza wazee walio nje ya bunge wanatafakari cha kufanya kabla hali haijaharibika.

“Sisi yetu macho… lakini kila zama na kitabu chake, hizi ndio zama za vijana, wakati wetu haya hayakuwapo…lakini ikifikia hatua ya kutaka kuliteketeza bunge lazima tutachukua hatua… lakini dalili sio nzuri,” alisema Msekwa.

Friday, September 6, 2013

UWANJA WA NAMFUA-SINGIDA UPO KATIKA HALI MBAYA MNO

Hii ndio hali halisi ilivyo katika uwanja mkongwe na wa kipekee ambao unafaa kuchezewa mechi za ligi wa Namfua uliopo mjini Singida.


Nje ya uwanja kulivyo

Hali ya mazingira ya uwanja ni mbaya sana - kuna uchafuzi wa mazingira wa hali ya juu




Uwanja huu kuta zote zipo katika hali mbaya ya kimazingira kutokana na kujaa vinyesi na mikojo

Monday, September 2, 2013

Syria yaitishia Marekani dhidi ya shambulizi

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema kuwa Syria ilitumia kemikali aina ya Sarin kushambulia wananchi

Hatua yoyote ya kijeshi itakayochukuliwa na Marekani dhidi ya Syria, huenda ikachochea usaidizi kwa wapiganaji waal-Qaeda na washirika wake kwa mujibu wa taarifa kutoka Damascus.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria, Faisal Mekdad pia aliambia BBC kuwa makundi ya wapiganaji waliojihami, yalitumia silaha za kemikali wala sio wanajeshi wa Syria.
Marekani awali ilisema kuwa ilikuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa serikali ya Assad ilitumia kemikali aina ya Sarin katika shambulizi baya sana wiki jana .
Rais Barack Obama ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya Syria lakini mwanzo anataka baraza la Senate kupigia kura hoja hiyo kabla ya kuchukua hatua zozote dhidi ya Syria.
Wabunge wa Marekani wanatarajiwa kukutana na maafisa wa ikulu ya White House huku maafisa hao wakiwa na imani kuwa wataunga mkono hoja ya Obama.
Hata hivyo hatua ya Obama mwanzo kutaka baraza la Senate kuunga mkono hatua ya serikali kutaka kushambulia Syria imewashangaza wengi hasa washauri wake wa karibu.
Sio wazi kuwa Obama ataungwa mkono hasa na wabunge wa bunge la waakilishi ambao wengi ni wa chama cha Republican.
Labda Pia kwenye Senate huenda asipate kuungwa mkono. Bila shaka hii itakuwa kura yenye wasiwasi kwa Obama.
Ikiwa Congress haitaunga mkono hoja ya Obama basi huenda, likawa jambo baya sana kwa utawala wake.
Tayari kamapeini imeanzishwa ya kuwashawishi watu nchini Marekani kuwa ni jambo jema kwa serikali ya Obama kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria.
Lakini kwa kukosa kuchukua hatua za mashambulizi na badala yake kuomba idhini ya baraza la Senate itakuwa mchezo wa pata potea kwa Obama.