SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi kumuua kinyama mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, baadhi ya askari waaminifu wamefichua siri za mauaji yanayofaywa na jeshi hilo.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, askari hao walisema wakuu wao wanatumiwa kwa amri za watawala ili kuingilia kudhibiti matukio ambayo wakati mwingine husababisha vurugu zinazopoteza uhai wa wananchi.
Walisema tatizo kubwa ni wakuu wa polisi wilaya (OCD), makamanda wa mikoa (RPC) na maofisa upelelezi wa mikoa (RCO) ambao hulazimishwa kufanya kazi kwa amri ya wakuu wa wilaya na mikoa.
“Hawa wakuu wa wilaya na mikoa ni viongozi wa chama tawala, CCM. Hivyo, ili viongozi wetu wa polisi waweze kupanda vyeo ni lazima wajipendekeze kwao; yaani hata kipindi cha kampeni mkuu wa wilaya anampa amri OCD kudhibiti wapinzani,” alisema mmoja wa askari hao.
Walifafanua kuwa ili tatizo hilo liweze kuisha na jeshi hilo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na uhuru, ni lazima vyeo hivyo vya wakuu wa wilaya na mikoa vifutwe kwenye katiba mpya ijayo.
Katika tukio linaloshabihiana na madai ya askari hao, Tanzania Daima limedokezwa kuwa huko mkoani Pwani, hivi karibuni jeshi hilo limelazimishwa kupindisha sheria kwa lengo la kumlinda kigogo mmoja wa CCM aliyekuwa ametiwa mbaroni.
Chanzo hicho kinasema kuwa wiki mbili zilizopita mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilaya, alikamatwa na polisi kwa kosa la jinai na baada ya uchunguzi alifikishwa mahakamani, lakini alikosa sifa za kupewa dhamana na hivyo alitakiwa kupelekwa rumande.
Lakini katika hali ya kushangaza, mtuhumiwa huyo alirejeshwa kituo kikuu cha polisi na kuhifadhiwa hapo. Na alikuwa akitaka kuonana na mumewe, anakabidhiwa kwa askari polisi wa kike ambaye alikuwa anampeleka zaidi ya kilometa 25 kwenda kuonana naye.
Taarifa toka ndani ya jeshi hilo mkoani humo zinasema kuwa, yote hayo yalifanyika kwa amri ya kigogo mmoja wa CCM mkoa, na uongozi wa polisi ulifyata mkia hadi juzi mtuhumiwa huyo alipoachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Ni katika mfano wa tukio kama hilo, askari hao waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa matukio ya raia kupigwa na wakati mwingine kujeruhiwa na polisi hadi kufa, hayawezi kukoma ikiwa sheria hazifuatwi; na badala yake zinazingatiwa amri za viongozi wa kisiasa.
Mwangosi aliwashtukia askari
Naye Mkuu wa Operesheni ya M4C ya CHADEMA, Benson Kigaila, jana alifichua siri mjini Iringa, akisema kuwa Mwangosi aliwatilia shaka mapema polisi waliokuwa kwenye tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kigaila alisema kuwa muda mfupi kabla ya kuuawa kwake, Mwangosi alimweleza kuwa askari wengi anaowafahamu si wale waliokuwa eneo la tukio kudhibiti mkusanyiko wa CHADEMA.
“Marehemu aliniambia kuwa hapa nina shaka na hawa polisi kwa kuwa wengi ninawafahamu lakini ninaowaona si wale ninaowafahamu.Wanaofanya kazi za jeshi ni mamluki wasio na mafunzo,” alisema Kigaila.
Wakati siri hiyo ikifichuliwa, taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo mkoani Iringa zinadai baadhi ya askari wanaodaiwa kumuua Mwangosi wamekamatwa kwa siri na kuwekwa chini ya ulinzi.
Chanzo chetu kinasema kuwa jeshi hilo mkoani Iringa tangu juzi linahaha kuchukua hatua za dharura za kuwafundisha askari wake matumizi sahihi ya silaha wakati wa kutuliza ghasia.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa tayari askari watano kati ya saba walioonekana kwenye picha mbalimbali za magazeti na mitandao wakimpiga Mwangosi, wametiwa mbaroni.
“Hili suala limetuweka katika wakati mbaya sana na hivi ninavyoongea na wewe tayari askari watano kati ya saba wanashikiliwa katika kituo cha polisi Mufindi, lakini habari hizi zinafanywa siri sana,” kilisema chanzo chetu.
Miongoni mwa askari watatu ambao hawajakamatwa kwa mujibu wa chanzo hicho, ni pamoja na yule anayeonekana katika picha mbalimbali akiwazuia wenzake waliomzunguka Mwangosi kwa kunyoosha mkono juu na na baadae akiwa amejeruhiwa.
Mbali na askari huyo anayetambulika kwa jina moja la Mwampamba, pia yule anayeonekana pichani akiwa ameshikilia silaha aina ya bastola anayetajwa kwa jina la Gabriel, naye hajakamatwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa askari wengi waliokuwa katika operesheni hiyo siku ya tukioa eneo la Nyololo, hawakuwa na mafunzo sahihi ya kutumia mabomu ya machozi.
“Kiutaalamu mabomu ya machozi yanatakiwa yalengwe juu na kuwe na umbali wa mita 60 mpaka 120, lakini ikitumika kinyume chake yanaweza kudhuru au kuua.
“Katika kutuliza ghasia kuna mabomu ya aina mbalimbali ambayo yanatakiwa kutumiwa kulingana na wakati, mabomu hayo ni yenye moshi mzito, mwepesi na rangi ambayo lengo lake ni kuwaweka alama watu watakaokuwa katika kundi linalotakiwa kudhibitiwa ili waweze kujulikana,” kilibainisha chanzo hicho.
Kwamba askari wengi wa usalama barabarani siku hiyo walikuwa ni wanawake kwani wale wa kiume wote walitakiwa kuvaa nguo za Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU).
Habari hizo zinaongeza kuwa, kutokana na hali hiyo maafisa wa jeshi hilo walilazimika kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda Iringa kutoa mafunzo kwa askari wa mkoa huo juu ya matumizi sahihi ya silaha.
Alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa askari hao wanaotuhumiwa kuua, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema limeshaundiwa tume.
“Hizo taarifa mimi sina na siwezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa limeshaundiwa tume. Tusubiri majibu yake, lakini hilo la kuja kwa maofisa kwa ajili ya kutupatia mafunzo mimi sijui, wewe umezipata wapi?” alisema Kamuhanda.
CHADEMA wasitisha M4C kwa muda
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kusitisha kwa muda Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mkoani Iringa na badala yake kimeitisha kikao cha Kamati Kuu cha dharura kujadili mfululizo wa mauaji yanayofanywa na polisi katika mikutano yao.
Mkuu wa oparesheni hiyo iliyopangwa kufanyika mikoa mitano, Benson Kigaila, jana aliwaambia waandishi wa habari mjini Iringa kuwa wamelazimika kukutana kujadili hatua zaidi za kuchukua.
Alisema kamati kuu itakutana jijini Dar es Salaam Jumapili hii na kutoa tamko juu ya nini kifanyike baada ya wao kuwasilisha taarifa nzima juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza ya operesheni hiyo.
“Tunahitaji kukaa na kutafakari juu ya matukio haya kwa kuwa si jambo la kawaida, polisi waue watu kwenye mikutano, nasi tukaendelea na mikutano yetu bila kuchukua hatua stahiki,” alisema.
Alisema wakati wote tangu kuanzia kutokea kwa msiba wa Mwangosi, kumekuwa na propaganda nyingi zilizojitokeza juu ya hali hiyo, huku serikali, polisi na CCM wakitaka kuhamishia lawama kwa CHADEMA.
Kigaila aliongeza kuwa Watanzania wanajua kuwa mikutano na maandamano ambayo polisi hawaingilii kuvunja haileti misukosuko wala vifo, kama ilivyokuwa kwenye mikoa mbalimbali, ikiwamo ya Lindi na Mtwara.
Alisema wananchi wanapaswa kutambua kwamba kuna kitu cha ziada ambacho serikali ya CCM na Jeshi la Polisi wanakifanya dhidi ya CHADEMA, na si shughuli ya sensa ambayo imegeuzwa sababu ya kusitisha mikutano yao, kwani wakati serikali inazuia CHADEMA kufanya kazi zake, CCM inaendelea na mikutano na mchakato wa uchaguzi.