Monday, September 24, 2012

Kinana ang'atuka CCM



MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Abraham Kinana, amesema hatogombea tena nafasi za vikao vya juu kwa kuwa muda wa miaka 25 aliyotumikia katika nafasi hizo unatosha.

Kinana aliyasema hayo mjini Dodoma wakati akizungumza na gazeti hili na kubainisha kuwa anaamini kitendo cha kung’atuka kwake ni kizuri na kitatoa nafasi kwa wanaCCM wengine wazuri nao watoe mchango wao kwa chama hicho.

“Sijagombea kwa kuwa miaka 25 ya kushiriki katika vikao vya juu inatosha na ni vizuri kung’atuka, naamini kuna wana CCM wengi wenye sifa na uwezo wa kuongoza chama,” alisema Kinana.

Alisema suala la uongozi ni la kupokezana vijiti hivyo kwa sasa ni wakati wake kukabidhi vijiti alivyo navyo kwa wengine. Wakati Kinana akitoa kauli hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alimsifu Kinana kwa uamuzi huo na kuuita kuwa ni uzalendo.

“Tunashukuru kwa uzalendo, ujuzi na uzoefu alioonesha katika kipindi chote alichoshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, hata hivyo, napenda nisisitize kutokana na sifa alizonazo bado chama chetu kinamhitaji,” alisema Nnauye.

Alisema kung’atuka kwake kuwania nafasi za vikao vya juu ndani ya chama hicho hakumaanishi kuwa chama hicho hakitoendelea kumtumia pale kitakapomhitaji, kwa kuwa uzoefu wake na utendaji wake ni mtaji ndani ya chama.

Alisema pamoja na kuamua kuachia ngazi, Kinana anaendelea kushika nyadhifa nyingine ndani ya chama hicho, ikiwamo ya Uenyekiti wa Bodi ya vyombo vya habari vya CCM vya Uhuru na Mzalendo.

Wakati huo huo, Nape amesema wagombea wa CCM wanaolalamika nje ya vikao na kutoa vitisho iwapo hawatapitishwa na vikao vya chama hicho, wanajiharibia sifa na kuonesha wazi kuwa hawawezi kuhimili vishindo vya uchaguzi.

Aidha, amesema mchujo wa wagombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaweza kuchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kutokana na idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hawatashughulikia malalamiko na vitisho vya wagombea yanayotolewa barabarani.

“Kama wanataka wafikishe malalamiko yao kwenye vikao halali tutashughulikia, lakini wakilalamika au kutoa vitisho inaonesha wazi uwezo wao wa kuhimili pressure ni mdogo, hasa ikizingatiwa kuwa siasa za sasa zimejaa pressure,” alisema Nnauye.

Alisema mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu nani apite na nani asipite ni vikao vya chama ambavyo ni Kamati ya Maadili, CC na NEC.

Hivi karibuni, Mbunge wa Musoma Vijijini, ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nimrod Mkono, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kama jina lake halitarejeshwa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa, atahakikisha inaeleweka.

Pia mbunge wa Kahama, James Lembeli aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisisitiza kwamba hatokubali kuenguliwa katika uchaguzi huo kwa visingizio vya misimamo yake bungeni.

Aidha, Nnauye aliweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna mgombea yeyote aliyeenguliwa na vikao vya chama hicho na kwamba kinachofanyika kwa sasa ni kwa kamati ya maadili kupitia majina na kutoa mapendekezo yatakayopitiwa na CC na uamuzi wa mwisho ya kuenguliwa mgombea utafanywa na NEC.

“Kazi ni kubwa kinachofanyika ni Kamati hii ya Maadili kupitia jina moja moja la kila mgombea na kisha kuwapatia alama ya A, B, C, D na E lakini katika vikao vingine alama hizo zinaweza kubadilika kulingana na vikao hivyo,” alisema.