Tuesday, September 11, 2012
Chadema wamsusa Tendwa, wamtisha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kusitisha kufanya kazi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa na kumtishia kikisema kama ana wendawazimu, ajaribu kukifuta aone moto wake.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama hicho iliyokutana juzi kujadili masuala mbalimbali ya kisiasa nchini.
Mbowe alisema yuko tayari kuchukua maelekezo ya karani kuliko ya Msajili na kwamba hawatapokea maelekezo yake wala kumheshimu hadi atakapoondolewa katika nafasi hiyo na kuteuliwa mwingine.
“Hatutahudhuria kikao chochote cha Tendwa … na kama ana wendawazimu ajaribu kukifuta chama hiki aone moto wa nchi hii,” alisema Mbowe na kuongeza, kuwa labda Tendwa aombe radhi ndipo watamsikiliza.
Mbali na hilo, Mbowe alisema mkakati wa chama hicho wa vuguvugu la mabadiliko utaendelea nchi nzima kwa mujibu wa ratiba.
Alisema Kamati Kuu ilimtangaza Tendwa kuwa adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyo nayo ingawa itaendelea kuheshimu Sheria ya Vyama vya Siasa bila kushiriki shughuli zinazosimamiwa na Tendwa.
Mbowe alisema ni lazima viongozi wa Serikali wawe na staha na kutoa kauli zenye busara zisizokuwa na utata, huku akimtolea mfano Msajili kwa kauli alizozitoa hivi karibuni baada ya vurugu za Iringa.
Baada ya vurugu hizo, Tendwa alisema atakifuta chama chochote kinachofanya vurugu zinazosababisha mauaji, kauli ambayo Mbowe alidai kuwa imewafanya wamwone kama anafanya kazi kwa kushinikizwa au kujipendekeza.
“Kumwacha Tendwa aendelee ni kuiingiza nchi kwenye machafuko… Kamati Kuu imeona ni hatari kuendelea naye na imemtaka awajibike kwa kujiuzulu, la sivyo hatutafanya kazi naye wala kupokea amri zake,” alisema Mbowe.
Kuhusu mikutano ya vuguvugu la mabadiliko, alisema chama hicho kimepanga kurudi Iringa ambapo watafanya mikutano katika kila kata na hatimaye mkoani Singida hususani katika jimbo moja ambalo hakulitaja, lakini akasema mikutano hiyo wataifanya kitongoji kwa kitongoji.
Madiwani Mwanza watupwa Wakati huo huo, Chadema imewavua uanachama madiwani wake wawili wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kwa madai ya kukiuka maadili, kanuni na Katiba ya chama hicho kwa kuhusishwa na tuhuma za ufisadi.
Madiwani hao ni Adam Chagulani kutoka kata ya Igoma na Henry Matata wa kata ya Kitangiri ambao walikuwa chini ya uangalizi baada ya Meya wa Jiji hilo, Josephat Manyerere kuvuliwa madaraka na Baraza la Madiwani jijini humo. Kadhalika, chama hicho kimevunja Kamati ya Uongozi jijini humo na sasa kinatarajiwa kuchagua nyingine.
“Baada ya Meya kuvuliwa madaraka hivi karibuni, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa aliunda kamati ya kuchunguza misingi iliyotumika, iliyojadili na kuridhika na mwisho kuamua kuwawajibisha kwa kuwavua uanachama,” alisema Mbowe na kuongeza kuwa katika hilo, chama hakitaona aibu kwani makosa mengine hayavumiliki.
Alisema wahusika hao waliitwa na walishapewa nafasi ya kujieleza na uamuzi huo wa Kamati Kuu ni onyo kwa viongozi wote wa Chadema.
Alifafanua kuwa chama hicho hakiwezi kumvumilia mtu anayeonekana kukwamisha tumaini la Watanzania kufanikisha ukombozi wa mabadiliko ya kimfumo na kiutawala.
Meya alivuliwa madaraka kwa madai ya kutokuwa na imani naye tangu alipochaguliwa katika wadhifa huo ambapo madiwani 20 walitaka Meya huyo ang’oke na wengine wanane wakasema asiondoke na hivyo kufanya akose sifa.
Mimi si mjomba wa Chadema Akizungumza na gazeti hili kutoka Nairobi jana, Tendwa aliishangaa Chadema kwa kutoa kauli hiyo kana kwamba uhusiano uliopo kati ya chama hicho na yeye ni uhusiano binafsi.
“Mimi sina uhusiano wa ujomba na Chadema, wanakuwa na uhusiano na mimi wa kisheria na nikitoa maelekezo wasipofuata wamevunja sheria … uhusiano wetu si binafsi, kwa uhusiano binafsi hata mimi sina haja nao.
“Hawa wana wanasheria kibao, wameshindwa kuomba ushauri?” Alihoji Tendwa na kutaka vyombo vya habari kutokuwa vya kuchukua wanachosema Chadema, badala yake wawaulize maswali. Akisisitiza msimamo wake, Tendwa alisema kamwe hataiomba Chadema msamaha.