Thursday, July 5, 2012
Kima cha chini 315,000/- kwa mshahara haiwezekani.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani amesema Serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha mshahara cha Sh 315,000 kilichopendekezwa, kwani kufanya hivyo kutailazimu kutumia asilimia 60 ya Bajeti yake kwa mishahara tu.
Alisema hayo jana bungeni wakati akitoa majumuisho ya makadirio ya matumizi ya Wizara yake, akiongeza kuwa jambo hilo halitekelezeki, bali Serikali itaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wa umma kadri fedha zitakavyopatikana.
Kuhusu motisha kwa wafanyakazi, Kombani alisema kila kada kwenye utumishi ipo inayofanya kazi kwenye mazingira magumu na kwamba motisha itaangaliwa na kutolewa kwa wote bila kuangalia watumishi wa maeneo ya pembezoni pekee.
Mbali na hayo, Kombani pia alitaka wabunge kuchunga ndimi zao wanapochangia mijadala na kutoa hoja bungeni ili wasimamie vizuri sheria, kwani kuendelea kushawishi watumishi kugoma si suluhu ya matatizo.
“Nakuombeni wabunge mkumbuke, kwamba wajibu wenu ni kusimamia sheria, pia chungeni ndimi zenu, mnaweza kutamka jambo likawa baya, si vyema kuwaambia watumishi waendelee kugoma, maana kufanya hivyo si suluhu,” alisema Kombani.
Kuhusu ukubwa wa Serikali, alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kupanga ukubwa wa Serikali yake na pia upangaji huo huzingatia vigezo zinavyohitajika, vikiwamo vya ukubwa wa nchi, idadi ya watu na kuangalia uwiano wa pato la nchi.
Alisema kuhusu pato, uwiano unaotakiwa ni asilimia 17 hadi 35 kutumika kulipa mishahara na kwa upande wa Serikali ni asilimia 27.1, hivyo bado nchi iko kwenye kiwango kizuri cha ukubwa wa Serikali.
“Tanzania haina Serikali kubwa, kiwango cha mapato na matumizi ya nchi ni asilimia 27.1, sasa utaona hata hatujazidi, kwani tunatakiwa kuwa kati ya asilimia 17 hadi 35, na sisi tuko 27.1, nchi nyingine za Afrika na hata Afrika Mashariki zimevuka kiwango chetu, ingawa pia wao wana idadi ndogo ya watu na eneo dogo,” alifafanua Kombani.
Akizungumzia suala la watumishi hewa, Kombani alisema hilo linatokana na watumishi halali walioondolewa kwenye orodha ya malipo kuendelea kulipwa isivyo halali.
Alisema Serikali imebaini kuwapo watumishi hewa na hadi sasa watumishi 12,000 wameondolewa kwenye orodha ya malipo na kwamba wengine 5,745 wamepewa adhabu ya nidhamu.
Hata hivyo, alisema watendaji waliohusika kwenye suala la watumishi hewa wamechukuliwa hatua, wakiwamo watuhumiwa sita ambao wamefikishwa mahakamani na pia majalada 86 ya watuhumiwa yako mahakamani kwa hatua za kisheria.
Akihitimisha mjadala wa Ofisi ya Rais Utawala Bora, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), haiwezi kulisafisha Bunge na tuhuma za rushwa, bali wenye jukumu la kufanya hivyo ni wabunge wenyewe.
“Wabunge wenyewe ndio wenye wajibu wa kujisafisha, kazi hiyo si ya Takukuru, tunapaswa kujisafisha tuhakikishe hakuna rushwa miongoni mwetu,“ alisema Mkuchika.