Friday, June 29, 2012

Hatuhusiki na kipigo cha Ulimboka -Serikali


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali haihusiki na imeshtushwa, imesikitishwa na inalaani kitendo cha kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
“Serikali itafanya uchunguzi wa kumtafuta wahalifu waliofanya kitendo hicho na haitaangalia waliohusika …hakuna maelezo yoyote ya polisi kuhusika na jambo hili,” alisema Dk Nchimbi.
Ulimboka (35) anayeongoza mgomo huo wa madaktari nchini, alivamiwa na watu wasiojulikana, kutekwa na kujeruhiwa kwa kipigo usiku wa kuamkia jana.
Dk Ulimboka ambaye anaongoza mgomo huo ingawa yeye si mwajiriwa wa Serikali, alifikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbli, Dar es Salaam jana asubuhi baada ya kuokotwa eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni akiwa amejeruhiwa.
Wakati Dk Ulimboka alipofikishwa nje ya Kitengo cha Mifupa (MOI), madaktari wenzake ambao wamesusa kuhudumia wagonjwa, walifurika hospitalini hapo na kuanza kusukuma gari hilo huku wakiimba nyimbo za mshikamano na wengine wakilia.
Walipiza kisasi kwa polisi
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana ni kulipiza kisasi, madaktari hao ghafla walimgeukia mmoja wa askari Polisi aliyekuwa amevalia kiraia na kumshambulia kwa kipigo kwa madai kuwa aliwasiliana na wenzake na kuwataarifu kuwa Dk Ulimboka bado yuko hai.
Askari huyo pia alinyang’anywa simu na redio ya mawasiliano ambavyo vyote viliharibiwa vibaya na alionekana akiwa ameumizwa na kuvimba mwilini huku akiwa hajapatiwa huduma yoyote.
Kutokana na majeraha hayo, askari wenziwe walimuondoa eneo hilo; na mara moja Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewataka waliomshambulia askari huyo kujisalimisha.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwataka madaktari waliomshambulia askari huyo, wajisalimishe na kurudisha vifaa walivyomnyang’anya; simu na redio ya mawasiliano.
Kova aliyezungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, alikemea tabia ya wananchi kujichukulia hatua mkononi kwa kumshambulia askari huyo na kuongeza kuwa alikuwa kazini akichunguza tukio hilo.
MAT, Ulimboka wasimulia
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi, alidai Dk Ulimboka alitekwa juzi usiku na watu wasiojulikana na kupigwa na kung’olewa kucha na meno na hali yake ni mahututi.
Alidai Dk Ulimboka alizungumza kwa taabu alipofikishwa hospitalini ambapo alidai juzi jioni alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Abduel anayedaiwa kutoka Ikulu na alitaka kuzungumza naye kuhusu maendeleo ya madai ya madaktari.
“Alikubali kuonana na mtu huyo ambaye pia alikuwa akizungumza naye mara kwa mara na alikubaliana na wenzake asiende kuonana naye mwenyewe, aliongozana na rafiki yake Dk Deo hadi eneo walilopatana ambalo ni Kinondoni barabara ya Tunisia,” alisimulia Dk Mkopi.
Alidai Dk Ulimboka alisimulia kuwa akiwa katika eneo hilo pamoja na Abduel na Dk Deo, walitokea watu watatu; wawili wakiwa na silaha aina ya bastola na mmoja bunduki.
Kwa mujibu wa madai ya Dk Ulimboka, watu hao walianzisha vurugu na kuwataka wengine waondoke na kumchukua peke yake na kumuingiza kwenye gari nyeusi yenye namba zisizosajiliwa na kutokomea naye.
Kwa mujibu wa madai hayo, Dk Deo aliamua kuwasiliana na wenzake ambao walimtafuta kwenye vituo vyote vya Polisi bila mafanikio na kuishia kuandika maelezo ya tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Dk Deo pia aliwasiliana na wanaharakati akiwamo Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) Hellen Kijo-Bisimba. Anadai alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni msamaria kwamba amemuokota Dk Ulimboka akiwa hoi eneo la Mabwepande.
Inadaiwa Dk Deo aliwachukua wanaharakati hao hadi Kituo cha Polisi Bunju alikopelekwa Dk Ulimboka na kumchukua na kumkimbiza Muhimbili.
Taarifa ya Kova
Kova alisema Dk Ulimboka alikuwa na rafiki yake aitwaye Dk. Deogratius Michael na watu wengine katika Klabu ya Leaders Kinondoni ambapo ghafla saa 5:30 usiku, walitokea watu watano wasiofahamika wakavamia klabu hiyo na kuwatishia na kuwataka walale chini.
“Dk Ulimboka na wateja wengine walilala chini kwa kuhofia madhara kwa kuwa watu hao walikuwa na kitu wanachohisi ni silaha na hatimaye watu hao walimchukua Dk Ulimboka na kusema kwamba walikuwa wakimhitaji yeye na kumuingiza katika gari aina ya Suzuki Escudo nyeusi ambayo haikuwa na namba za usajili,” alidai Kova.
Alidai wakati wakiwa njiani, watu hao walianza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake na bila kusema wanataka nini kutoka kwake na walipofika maeneo ya Mwenge, walimvisha fulana nyeusi usoni na hakujua tena wanaelekea wapi huku wakiendelea kumpiga na mmoja wa watu hao akasema watamuua.
Kamanda Kova alidai ilipofika asubuhi, Dk Ulimboka alijikuta yupo msitu wa Mambwepande na alijivuta hadi barabarani na alikutwa na msamaria akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka alieleza kuwa gari yake aliiacha maeneo ya Leaders Club na watu hao waliuchukua ufunguo wake, nyaraka zake pamoja na fedha ambazo hakumbuki ni kiasi gani.
Kamanda Kova alisema ameunda jopo la wapelelezi wa fani mbalimbali chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mlalamikaji mwenyewe na mashahidi walioona tukio hilo, ili uchunguzi wa shauri hilo ufanyike na kuwaomba raia wema kutoa ushirikiano ili matukio ya aina hiyo yasijirudie.
“Naamini kwamba watu wengi watakuwa wameguswa na tukio hili ila nawasihi watuache polisi tufanye upelelezi na waachane na minong’ono kwa kuwa sisi hatukuwa na ugomvi wowote na Dk Ulimboka wala madaktari… upelelezi utafanyika kwa makini na taarifa rasmi zitatolewa baadaye.” alisema.
Serikali kutoa tamko
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema leo Serikali itatoa tamko bungeni juu ya hatua zitakazochukuliwa dhidi ya mgomo wa madaktari unaoendelea nchini na kusema litakalokuwa na liwe.
Pinda aliwataka madaktari hao kuheshimu amri ya Mahakama Kuu iliyokazia uamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ya kuwataka madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini pamoja na kuwatangazia umma kupitia vyombo vya habari kusitisha mgomo.
Maelezo ya Waziri Mkuu yamekuja baada ya Mbunge Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) kuomba Mwongozo wa Spika na kutaka Serikali iseme inachukua hatua gani za ziada kuhusu mgomo huo.
“Jana (juzi) baada ya madaktari kuendelea na mgomo, tulirudi Mahakama Kuu nayo iliagiza amri ya Juni 22, mwaka huu itekelezwe na madaktari waache mgomo na kutangaza kwenye vyombo vya habari.
“Ni kweli aliyosema Zambi nasi tulifikiri si vizuri kuingilia Mahakama, lakini kesho (leo) tutatoa taarifa bungeni juu ya hatua Serikali itakayochukua na kama Waswahili wanavyosema litakalokuwa na liwe,” alisema Pinda.