Akamatwa na kichwa cha albino
na Abdallah Khamis
MFANYABIASHARA wa baa na nyumba ya kulala wageni ya Bongo Star Lodge
iliyopo Kawe Ukwamani, James Isame, maarufu kama Mzee Chacha (50),
anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa tuhuma ya kukutwa
na kichwa cha binadamu anayedhaniwa kuwa ni mlemavu wa ngozi (albino).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amethibitisha
kushikiliwa kwa mfanyabiashara huyo na kusema kuwa alikamatwa juzi saa
2:45 usiku baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa jeshi hilo juu ya
kuwepo kwa tukio lisilo la kawaida katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
Alieleza kuwa, baada ya taarifa hizo, polisi waliizingira nyumba hiyo
kisha wakamtafuta mjumbe wa eneo la Kawe kwa ajili ya kuthibitisha
upekuzi utakaofanyika na kwamba baada ya taratibu zote, walimtaarifu
muhusika ambaye alianza kuonesha upinzani juu ya kufanyiwa upekuzi.
Alisema jitihada za mtuhumiwa kuzuia upekuzi huo zilishindikana, ndipo
katika kufanya kazi hiyo maeneo yote ya ndani na nje ya nyumba hiyo
pamoja na baa, walifanikiwa kukuta kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa
juu ya ukuta wa choo.
“Kilikuwa kimevingirishwa katika mfuko wa
rambo na tuliweza kubaini kuwa ni kichwa cha binadamu baada ya kuona
nywele na meno, ila bado hatujajua ni wa jinsia gani au kama ni mlemavu
wa ngozi,” alisema Kenyela.
Akielezea tukio zima, Kamanda
Kenyela alisema baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kuwepo kitu
kisichoeleweka katika eneo la mfanyabiashara huyo, waliweka ulinzi
maeneo yote.
Aliongeza kuwa, kichwa hicho kilikuwa na mchanga
hali inayoonesha kuwa huenda kilikuwa kimefukiwa kabla ya kufikishwa
hapo au wakati wa kukatwa kilikuwa kimewekwa katika mchanga.
Kamanda Kenyela alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na baada ya
upelelezi kukamilika, watapeleka maoni ya Jeshi la Polisi kwa Mkurugenzi
wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.
Baada ya taarifa
hizo kuenea, Tanzania Daima ilifika hadi katika nyumba ya kulala wageni
ya Bongo Star Lodge iliyoko Kawe na kuangalia mazingira ya eneo zima na
kisha kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi na majirani.
Eneo la
nyumba hiyo limezungukwa na nyumba nyingine za makazi ya watu, huku eneo
la kuuzia vinywaji likiwa limepakana na vyoo vitatu ambavyo ukuta wake
ndiyo unaosadikiwa kuwekwa kichwa hicho.
Kuanzia mlango wa
kuingilia katika baa hiyo hadi vyumbani, kumesakafiwa na kuwekwa vigae
ambavyo si rahisi kwa mtu kuchimba pasipo kujulikana, huku vyooni kukiwa
na hali hiyo pia.
Mmoja wa wafanyakazi wa nyumba hiyo
aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema kuwa, walishuhudia askari
wakifika katika eneo hilo na kwenda moja kwa moja katika upande wa choo,
na baada ya muda wakaondoka na mmliliki wa nyumba hiyo.
“Hatukujua ni kitu gani kinaendelea mpaka meneja alipotuambia kuwa mzee
ameshikwa na kichwa cha binadamu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Majirani waeneo hilo walipoulizwa kama wanafahamu juu ya jirani yao
kukamatwa kwa tuhuma za kukutwa na kichwa cha binadamu, walishangaa na
kusema ndiyo kwanza wanapata habari hizo kutoka kwa mwandishi.
Kwa upande wake, mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo aliyefahamika kwa
jina moja la Mzee Kilambo, alisema aliitwa na polisi kwa ajili ya
kushuhudia upekuzi katika eneo hilo, na kwamba maelezo zaidi ya nini
kimetokea yanapaswa kuulizwa polisi.