WAZIRI wa Katiba na Sheria wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari amesema, watu
watakaoshindwa kuheshimu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwemo kuvaa nguo
zisizo za staha na kula hadharani watachukuliwa hatua za kisheria.
Bakari ameyasema hayo wakati anatoa
taarifa kuhusu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotazamiwa kuanza kesho
Jumamosi ambapo waumini wa dini ya Kiislamu watafunga kwa muda wa mwezi
mmoja.
Amesema, Serikali imechukua uamuzi huo
kufuatia kuwepo kwa vitendo vya kudharau mwezi wa Ramadhani, ikiwa ni
pamoja na watu kula hadharani pamoja na kuvaa mavazi yasiyokuwa na staha
kwa wanawake yenye kusababisha matamanio.
“Ndugu wananchi kesho (leo) ni Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan unaanza ambapo wananchi wanatakiwa kuuheshimu
ikiwemo kuacha kula hadharani na kuvaa mavazi ya stara,” alisema Bakari.
Aidha, aliwataka wamiliki wa migahawa na
hoteli zote kuzifunga katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani ili kuepuka malumbano kwa waumini wa dini tofauti.
Alisema hoteli zitakazofanya kazi ni
zile zilizoruhusiwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wageni ikiwemo watalii
ambazo zinafahamika zikiwa zimeorodheshwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri huyo alisema serikali imeamua
kutoa taarifa hiyo kufuatia katika miaka iliyopita kuibuka kwa vitendo
vya kudharau mwezi wa ramadhani ikiwemo wananchi kula hadharani.
Mapema Waziri wa Habari, Utangazaji,
Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk aliwataka wamiliki wa hoteli za
kitalii kutunza mila na silka za wananchi wa Unguja katika kipindi cha
mwezi wa Ramadhani.
Aliwataka watalii kuhakikisha wanavaa nguo zenye heshima zinazokubalika katika kipindi cha Ramadhani.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka
wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria kuwapiga na kuwashambulia
watu wanaovaa nguo fupi katika kipindi hiki.