Saturday, July 21, 2012

Watakaovaa 'kihasara’ Mwezi Mtukufu, kula mchana kukiona


WAZIRI wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari amesema, watu watakaoshindwa kuheshimu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwemo kuvaa nguo zisizo za staha na kula hadharani watachukuliwa hatua za kisheria.
Bakari ameyasema hayo wakati anatoa taarifa kuhusu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotazamiwa kuanza kesho Jumamosi ambapo waumini wa dini ya Kiislamu watafunga kwa muda wa mwezi mmoja.
Amesema, Serikali imechukua uamuzi huo kufuatia kuwepo kwa vitendo vya kudharau mwezi wa Ramadhani, ikiwa ni pamoja na watu kula hadharani pamoja na kuvaa mavazi yasiyokuwa na staha kwa wanawake yenye kusababisha matamanio.
“Ndugu wananchi kesho (leo) ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaanza ambapo wananchi wanatakiwa kuuheshimu ikiwemo kuacha kula hadharani na kuvaa mavazi ya stara,” alisema Bakari.
Aidha, aliwataka wamiliki wa migahawa na hoteli zote kuzifunga katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kuepuka malumbano kwa waumini wa dini tofauti.
Alisema hoteli zitakazofanya kazi ni zile zilizoruhusiwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wageni ikiwemo watalii ambazo zinafahamika zikiwa zimeorodheshwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri huyo alisema serikali imeamua kutoa taarifa hiyo kufuatia katika miaka iliyopita kuibuka kwa vitendo vya kudharau mwezi wa ramadhani ikiwemo wananchi kula hadharani.
Mapema Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk aliwataka wamiliki wa hoteli za kitalii kutunza mila na silka za wananchi wa Unguja katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani.
Aliwataka watalii kuhakikisha wanavaa nguo zenye heshima zinazokubalika katika kipindi cha Ramadhani.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria kuwapiga na kuwashambulia watu wanaovaa nguo fupi katika kipindi hiki.