Wednesday, July 25, 2012

Basi laua watu 3 Mlima Kitonga

WATU watatu wamekufa na wengine 17 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka katikati ya Mlima Kitonga, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
Aidha mkoani Pwani imetokea ajali nyingine ambayo abiria 11 waliokuwa wakisafiri kwa kutumia mabasi ya Dar Express na Simba Mtoto walijeruhiwa baada ya mabasi hayo yaliyokuwa yakisafiri kutoka Arusha na Dar es Salaam kugongana uso kwa uso eneo la Wami mkoani Pwani.
Kuhusu ajali iliyotokea mlima wa Kitonga, Iringa, mmoja wa majeruhi wanaohitaji msaada wa haraka ni Vedastus Benjamin (11), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Minazini, Kurasini Shimo la Udongo, Dar es Salaam.
Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisafiri peke yake kutoka Lusaka, Zambia alikokwenda kumsalimia baba yake mdogo, amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa sambamba na majeruhi wengine na anaomba wasamaria wafikishe taarifa hiyo kwa baba yake mzazi, Vedastus Benjamin.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alisema ajali hiyo ya gari aina ya Isuzu namba T 218 ACH mali ya Kampuni ya Mwashi Express ya Dar es Salaam ilitokea juzi saa 11.30 jioni.
Alisema basi hilo likitoka Tunduma kwenda Dar es Salaam liliacha njia na kugonga gema na kupinduka na kusababisha maafa hayo. Kakamba alitaja waliokufa kuwa ni Clara Dili (32) mfanyabiashara na mkazi wa Lusaka, Abel Nelson (32) mkazi wa Dar es Salaam na Danny Kawin (43), mfanyabiashara na mkazi wa Zambia.
Alisema dereva wa basi hilo, Benjamin Enock ambaye pia amelazwa katika hospitali hiyo yuko chini ya ulinzi wa Polisi akisubiriwa apate nafuu ili ahojiwe kwa sababu uchunguzi wa awali unaonesha ajali hiyo ilitokana na uzembe binafsi uliomfanya ashindwe kuchukua hadhari.
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita jana alifika katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kufariji majeruhi hao. Pamoja na kutoa pole, Guninita alitoa msaada wa fedha na vifaa vya tiba kwa baadhi ya majeruhi waliokosa ndugu wa kuwasaidia wakiwamo wa Zambia.
Katika ajali ya mkoani Pwani, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ernest Mangu alimwambia mwandishi kuwa ilitokea kati ya Wami na Msata jana saa 7 mchana wakati dereva wa basi la Dar Express akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake.
Kamanda Mangu alisema dereva wa Dar Express namba T316 ANS lililokuwa likitoka Arusha kwenda Dar es Salaam, Juma Lyimo alijaribu kulipita gari la mbele bila uangalifu na kukutana uso kwa uso na Simba Mtoto namba T901 ASL lililokuwa likiendeshwa na Khalifa Makame likienda Tanga kutoka Dar es Salaam.