Monday, May 27, 2013
MASWALI NA MAJIBU JUU YA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA
Je ni kweli kuwa madhara ya uvutaji moshi wa sigara yako ni kidogo kuliko yale yatokanayo na kuvuta?
Kama nitasimama karibu na mvutaji na kuvuta moshi, kuna madhara ambayo siyo ya moja kwa moja. Kwa upande mwingine kama jirani wa mvutaji unaweza kuvuta sumu nyingi itokanayo na tumbaku kwa sababu hakuna kitu cha kuichuja.
Sigara za viwandani zina kishungi ambacho huchuja tindikali mbalimbali zenye sumu, kama vile kaboni na asidi ya magamba ya miti, ambazo zina madhara kwa mapafu.
Je gongo na sigara husaidia uyeyushaji wa chakula?
Ni imani na fikra potofu kwamba, ukinywa gongo au kuvuta sigara kwa kiasi kidogo baada ya chakula itasaidia kuyeyusha baadhi ya vyakula vya mafuta. Pombe inaweza hata kupunguza mtiririko wa kawaida wa kimiminika muhimu kwa uyeyushaji wa chakula (tindikali) na hivyo kuchelewesha kuliko kurahisisha uyeyushaji wa chakula.
Nikotini ya sigara kwa upande mwingine inaongeza kazi katika utumbo mpana na hivyo hurahisisha uyeyushaji wa chakula. Lakini kwa upande mwingine nikotini huchochea utengenezaji wa tindikali tumboni ambayo husababisha maumivu ya tumbo.
Je, ni kweli kwamba unywaji pombe na uvutaji sigara kupita kiasi husababisha vifo?
Unaweza kufa kutokana na kuvuta sigara au kunywa pombe, lakini ni pale tu utakapozidisha. Kama utavuta idadi kubwa ya sigara unaweza kupata kwa wingi sumu, iitwayo nikotini, iliyo katika tumbaku. Hii inaweza kusababisha kifo cha ghafla.
Unywaji wa pombe kupita kiasi husababisha kusimama kabisa kwa shughuli za ubongo.
Lakini pombe pia ni chanzo cha ajali nyingi za barabarani na kazini. Kumbuka kwamba pombe ni chanzo cha vifo vingi kuliko madawa mengine ya kulevya.
Kwa nini pombe na sigara bado zinatangazwa wakati zina madhara?
Serikali ina wakati mgumu katika kuamua kati ya kulinda afya za watu na shinikizo litokalo kwa wakulima pamoja na makampuni yanayotengeneza pombe na sigara. Wenye viwanda na wauzaji wanataka bidhaa hizi zitangazwe kibiashara.
Serikali yenyewe pia inapata faida kutokana na kutangazwa kwa tumbaku na pombe kutokana na ushuru kupitia ulipaji wa kodi.
Hata hivyo, Serikali imeamua kuwa matangazo hayo ya biashara yawe na onyo lisemalo Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako.
Hii inawajulisha wavutaji wa sigara kuhusu hatari za uvutaji sigara na kuacha kila mtu ajiamulie mwenyewe.
Ni kwa nini ni vigumu kuacha kuvuta sigara?
Hii ndiyo hatari kuu ya matumizi ya madawa ya kulevya ambayo unayazoea na kufikiri huwezi kufanya lolote bila kuyatumia. Kwa upande wa sigara unaweza kuzoea hali yake ya kukutuliza na hali ya kutamani kuvuta kila unapojisikia. Kwa wengi hamu hiyo hutokea wanapojifikiria kwamba wanahitaji kuvuta sigara baada ya kazi nzito, pamoja na pombe, au baada ya kula.
Kwa hiyo kama unataka kuacha uvutaji wa sigara inabidi ubadili tabia na kuepuka vishawishi na pia kupambana na nafsi na matamanio yako. Hii ni hatua kubwa inayohitaji msimamo mkali.
Vijana wafanye nini kujiepusha na madawa ya kulevya, pombe, sigara na bangi ?
Vijana wengi wanaanza kutumia madawa ya kulevya kwa sababu wenzi wao wanatumia madawa hayo, na hivyo kujisikia kulazimika kutumia madawa hayo.Wanafikiri ndiyo njia pekee ya kutatua matatizo yao. Fikiria kuhusu maisha yako na jinsi unavyotaka baadaye yawe.Utagundua haraka sana kuwa madawa ya kulevya hayatakusaidia kufikia malengo uliyokusudia.
Njia mojawapo ya kujizuia kutumia madawa ya kulevya ni kujitenga na makundi au mtu anayetumia madawa hayo. Jitafutie shughuli za kufanya ili uondokane na mawazo potofu. Waweza kufanya mambo kama vile kujisomea, mazoezi ya viungo au kusaidia shughuli za nyumbani. Vijana wengine wanafarijika na kujihusisha na mambo ya dini kwa mfano kuimba kwaya au mikusanyiko ya vijana misikitini na makanisani.
Iwapo kuna anayetaka kukushauri kutumia madawa jaribu kupinga kwa nguvu kitendo hicho. Mweleze kwanini hutaki kutumia madawa ya kulevya. Mweleze kuwa madawa ya kulevya yanahatarisha maisha afya yako na kwamba kuyanunua madawa hayo kunagharimu fedha nyingi. Zaidi ya hayo kutumia madawa kutafanya usiweze kufikia malengo uliyojiwekea katika maisha. Iwapo ataridhika na uliyomweleza hatakusumbua tena.
Kama nimeshaanza kutumia madawa ya kulevya na sasa nataka kuachana nayo nifanyeje?
Kuna sababu nyingi zinazofanya watu watumie madawa ya kulevya. Njia nzuri ya kuacha ni lazima utambue sababu inayokufanya utumie madawa ya kulevya. Katika maeneo mengine kuna vituo vya ushauri kwa vijana juu ya madawa ya kulevya. Mara nyingi ni vigumu kuacha kutumia madawa hasa kwa wale wanaotumia madawa makali.Lakini inawezekana iwapo umedhamiria kuacha. Unaweza ukasaidiwa kwa ushauri na vituo maalumu vilivyopo kwenye baadhi ya maeneo ya jamii juu ya kuacha kutumia madawa ya kulevya.
Nimsaidiaje rafiki yangu aliyetopea kwenye madawa ya kulevya ili ayaache?
Iwapo utatambua kuwa rafiki yako anatumia madawa ya kulevya kuna mambo machache unaweza kujaribu kuyafanya. Zungumza na rafiki yako kabla hajalewa. Rafiki yako aelewe kwamba una wasiwasi naye. Jaribu kumsaidia kuepuka kwenda mahali ambapo anaona hawezi kujizuia kutumia madawa ya kulevya. Unaweza pia kumsaidia rafiki yako kwa kumtafutia msaada kutoka sehemu nyingine yoyote.Wakati mwingine watu wanaoathirika na madawa ya kulevya huwa hawapo tayari kukusikiliza na kupata msaada. Inaweza kutokea kwamba mwathirika akakukasirikia au urafiki wenu ukavunjika, lakini usijilaumu.Ulijaribu kusaidia na ulijitahidi kadri ya uwezo wako lakini, imeshindikana.Wakati mwingine inafaa kuvunja urafiki kwa usalama wako na wa rafiki yako pia. Pengine baada ya urafiki kuvunjika anaweza kuelewa kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa na akaamua kujishauri juu ya utumiaji wake wa madawa ya kulevya.
Madawa ya kulevya ni nini?
Tunaposema madawa ya kulevya ina maana ni matumizi mabaya ya madawa na hasa pale yatumikapo kinyume cha maelekezo ya tabibu na kuleta madhara kwa mtumiaji.
Madawa ya kulevya yanatoka wapi na yanafika vipi Tanzania?
Madawa ya kulevya yanatoka nchi mbalimbali duniani, na baadhi yanatoka hapahapa Tanzania.mfano kokain inatokea Amerika ya kusini, heroini hutoka Bara la Asia, nchi za India, Pakistan na Burma. Madawa yanayotengenezwa viwandani kama mandrax yanatoka nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania. Bangi na mirungi hulimwa Tanzania. Madawa yaliyothibitishwa na madaktari, pamoja na vimiminika vinavyogeuka hewa, kama petroli, yanatengenezwa hapahapa Tanzania.
Madawa ya kulevya ambayo hayatengenezwi Tanzania yanaingizwwa nchini kinyume cha sheria kwa kupitia njia ya barabara, anga, au bahari. Kuna mtandao kabambe wa shughuli hizo za madawa ya kulevya.
Wauzaji hao wa madawa ya kulevya hutoa ahadi za pesa za haraka ili kuwapata vijana wa kuwashirikisha kama wasambazaji. Wengi wa vijana hao hawatambui madhara ya kumiliki, kutumia na pia kujihusisha na shughuli hizo haramu ambazo zinaweza kuwasababishia kifungo cha maisha. Kwa upande mwingine vijana hao wanachangia kuharibu maisha ya wenzao na hata maisha yao wenyewe. Mara nyingi madawa ya kulevya husambazwa na watu tunaowa fahamu miongoni mwa familia na marafiki.
Je, ni vijana wa kiume pekee ndio wanaotumia madawa ya kulevya? Na wanaanza kutumia katika umri gani?
Hapana! Madawa ya kulevya yanatumiwa na watu wa rika zote katika jamii; wanawake na wanaume, wazee na vijana, maskini na matajiri! Wanaume ndio wanaotumia zaidi madawa ya kulevya kuliko wanawake hapa Tanzania. Matumizi ya madawa ya kulevya kwa wanawake si ya wazi, na ni ya usiri zaidi. Lakini wanawake na wasichana, kwa bahati mbaya, wanakaribia kuwafikia wanaume kwa utumiaji wa madawa ya kulevya.
Watu wengine huanza kutumia madawa ya kulevya katika umri mdogo sana, hata katika umri wa kwenda shule ya msingi!
Mara nyingi vijana hawa huanza kufanyia majaribio madawa ya kulevya bila kujua chochote juu ya madhara na hatari zake. Wengine huweza hata kudhuru vibaya miili yao na akili au kuishia kutumia madawa kila mara, na wasiweze tana kuyaacha.
Je, madawa ya kulevya yanaathiri vipi mwili na ubongo wa binadamu?
Moja ya vitu vinavyotisha kuhusu madawa ya kulevya ni kwamba yanaathiri watu kwa njia mbalimbali na huwezi ukasema kwa uhakika jinsi yatakavyokuathiri. Madhara ya madawa ya kulevya yanategemea aina, kiwango na jinsi yatakavyotumika. Vilevile inategemea na umri, afya ya mwili na ukomavu wa akili, na pia mazoea ya matumizi ya madawa hayo.
Madhara ya muda hutokea mara tu baada ya madawa ya kulevya kutumika, wakati madhara ya muda mrefu huonekana baada ya muda kupita, na mara nyingi husababisha uharibifu wa kudumu kwenye mapafu na ubongo.
Kwa mfano, bangi, husababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo, matatizo ya kumbukumbu ya muda mfupi, pamoja na umakini kujifunza, kufikiri na kutatua matatizo. Pia inaweza ikasabisha kasoro kwenye utaratibu wa viungo vya mwili. Mara kwa mara wavuta bangi huwa na macho mekundu. Na vijana wengine hupata mihemko mbalimbali kama uoga na hofu baada ya matumizi ya bangi.
Madawa ya kulevya ya vichangamsho, kama mirungi na kokaini, inasemekana kuwa huwafanya watumiaji kuwa macho, kujiona wana nguvu na kujiamini. Vichangamsho vikitumika kwa wingi, humfanya mtumiaji kujihisi kuwa na wasiwasi au hofu. Matumizi mabaya ya madawa ya kulevya kwa muda mrefu huweza kusababisha matatizo ya akili na kifo iwapo yatatumika kwa kiwango cha juu.
Madawa ya kulevya yanayokufanya upooze. Kama heroini au madawa mengine yanayoagizwa na daktari, husababisha kujisikia umetulia, una amani na furaha. Ukizidisha vipimo husababisha usingizi, upungufu wa umakini na uwezo wa kuona, kizunguzungu, kutapika na kutokwa jasho. Vilevile kipimo kingi kinaweza kusababisha usingizi wa muda mrefu, kuzimia na hata kifo. Pombe za kienyeji kama gongo ni hatari kwa afya na zinaweza kusababisha upofu na hata kifo.
Matumizi ya madawa ya kulevya hupunguza uwezo wa vijana kuhimili na kutatua matatizo ya kijamii na kiakili. Hii husababisha vijana kuwa wepesi kujihusisha na ujambazi na mambo ya ngono na ugomvi, mabadiliko hayo ya tabia husababisha ugomvi katika familia na kuvunjika kwa urafiki. Matumizi ya madawa ya kulevya ndiyo sababu kubwa ya ajali za barabarani, kujiua na maambukizo mbalimbali.
Madawa gani ya kulevya ni hatari zaidi?
Kwa ujumla madawa yote ya kulevya yanaweza kuwa ni ya hatari. Kati ya madawa yaliyohalalishwa kisheria nikotini, ambayo ipo kwenye sigara, ndiyo hasa ya hatari. Inawezekana kuwa umeshakuwa tegemezi kwa sigara. Hii ina maana ubongo wako utaizoea nikotini na utahitaji nikotini zaidi na zaidi ili kuendelea kuwa na hali hii. Nikotini pia ni hatari zaidi kwa sababu vijana mara nyingi huanza kutumia madawa makali zaidi.
Miongoni mwa madawa yasiyoruhusiwa kisheria nchini Tanzania, heroini ndiyo labda yenye kusababisha utegemezi. Vilevile inahusishwa na makosa mengi ya jinai. Utumiaji wa heroini ni hatari hasa katika maambukizi ya UKIMWI. Watu wanaposhirikiana katika kutumia sindano za kujidungia heroini wanakuwa na uwezekano mkubwa sana wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Hili hutokea pia pale wtumiaji wa heroini wanapojiuza miili yao, itumike kwa ngono ili wapate madawa ya kulevya au fedha za kununulia madawa hayo.
Uvutaji bangi husaidia kuondoa aibu na vizuizi. Hii inamaanisha kuwa wavuta bangi wanaweza wakasahau kufanya mapenzi salama na hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kupata au kueneza UKIMWI. Matumizi mabaya ya madawa huweza kuwa hatari sana na pengine kusababisha kifo pale yatakapotumiwa kupita kipimo ama yatakapochanganywa na madawa mengine au pombe.
Je kuna tofauti yoyote ya athari za madawa ya kulevya kati ya vijana na wazee?
Athari za madawa ya kulevya ni sawa kwa rika zote. Hata hivyo vijana ndiyo walio katika hatari zaidi ya kuathirika na madawa ya kulevya, kwa sababu wako katika hatua ambayo mwili na akili, bado vinaendelea kukua. Mara nyingi vijana hupata maelezo potofu kuhusu madawa ya kulevya. Kama marafiki zao hawatakuwa mfano mzuri wa kuigwa wanaweza wakawashawishi kutumia madawa ya kulevya. Ni muhimu kupata maelezo sahihi kuhusu athari za madawa ya kulevya ili uwe na uwezo wa kujiamulia mwenyewe. Fikiri kwa makini! Ni mwili wako, ni maisha yako, na ni uamuzi wako.
Madhara ya madawa ya kulevya yanadumu kwa muda gani?
Ni vigumu sana kujibu swali hili kwa sababu mbalimbali kama vile aina za madawa ya kulevya, njia za utumiaji, hali ya mtu na mazingira anapoyatumia madawa hayo ya kulevya. Mtu anaweza kuanza kutumia madawa ya kulevya mara kwa mara ili kukidhi kile anachokihitaji. Kwa baadhi ya madawa ya kulevya, na baadhiya watu, matumizi ya mara kwa mara kwa kipindi cha zaidii ya wiki mbili ni kipimo tosha cha kumfanya aishi kwa kutegemea madawa ya kulevya.
Je, unaweza kufa ukitumia madawa ya kulevya?
Ndiyo, unaweza. Kifo kinaweza kuwa cha ghafla au kutokana na madhara ya muda mrefu katika viungo vya ndani ya mwili kwa matumizi ya madawa ya kulevya. Watu wengi hufa katika ajali pale wanapokuwa wana kiasi kikubwa cha kilevi katika damu, kwani wanashindwa kutambua mazingira ya hatari.
Mtumiaji wa madawa ya kulevya anaweza akafa ghafla kwa kile kinachoitwa kuzidisha madawa, pale mtu tu atakapotumia madawa ya kulevya zaidi ya uwezo wa mwili. Kifo cha ghafla kinaweza kutokea au kutokana na matumizi ya kokaini na vifukishi kama petroli bila hata ya kuzidisha kiwango. Watumiaji wa vifukishi kama petroli mara nyingi hutumia mifuko ya plastiki ili kuongeza kiwango cha mvuke wanaovuta. Katika mazingira haya ni rahisi kupoteza fahamu na kukoseshwa hewa na mifuko hiyo. Kuchanganya baadhi ya madawa ya kulevya kama vile heroini na madawa mengine hasa madawa ya kutuliza maumivu (mfano valium) au pombe pia huweza kusababisha kifo.
Je, watu huchanganyikiwa baada ya matumizi ya madawa ya kulevya?
Kuna imani potofu kwamba wote wenye matatizo ya akili wamekuwa hivyo kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya, hii sio kweli. Lakini, madawa ya kulevya mengine huleta ulemavu wa akili. Haya ni yale yaitwayo vichangamsho kama kokaini na mirungi. Pale yatumiwapo kwa viwango vikubwa mtu huchanganyikiwa kwa muda wa siku chache au wiki nzima. Hii hutokea pia kwa bhang.
Je, inawezekana kuwa ni hatari kutumia valium au Klorokwini au madawa mengine ambayo yanapatikana katika maduka ya dawa?
Ndiyo! dawa yoyote itakayotumiwa pasipo mahitaji sahihi au kwa kipimo zaidi ya kinachopendekezwa inaweza kuwa hatari na pengine kusababisha kifo. Mara zote sikiliza kwa makini maelezo yatolewayo na madaktari au wauzaji wa madawa. Usichanganye dawa na pombe au dawa nyingine kwani kwa hakika kufanya hivyo ni hatari.
Nini matokeo ya unusaji wa petroli kwa vijana?
Kama kijana akinusa au kuvuta petroli kupitia puani au mdomoni, petroli hiyo huingia kwenye mapafu na sehemu zote mwilini. Madhara ya unusaji au uvutaji petroli ni sawa kabisa na pombe. Baada ya kunusa/kuvuta petroli mtumiaji hujisikia kizunguzungu na hulewa.Wengine huhisi kama kwamba wanaota na kujisikia furaha. Lakini wengine hujisikia kuumwa na kusinzia.
Unusaji/uvutaji wa petroli ni hatari sana na hata huweza kusababisha vifo kwani petroli humfanya mtu apoteze fahamu, huharibu mapafu na wengine hufa kwenye ajali. Hii hutokana na kushindwa kutoa maamuzi yafaayo wanapokabiliwa na hali zinazoweza kusababisha ajali, hasa barabarani.
Matumizi ya muda mrefu ya petroli huweza kumsababishia madhara mtumiaji kama kutokwa na damu puani, kupoteza hamu ya kula, kuwa dhaifu, kupata matatizo ya mtindio wa ubongo, kupatwa na magonjwa ya figo, moyo, mapafu na kuharibika maini.
Je ni kweli kwamba uvutaji bangi hukufanya uwe na nguvu?
Si kweli kabisa. Baada ya kuvuta bangi mtu hujiona kama jasiri sana na mwenye nguvu.Lakini madhara ya bangi ni kinyume na matarajio ya mtumiaji kwani mishipa husinyaa na ubongo hushindwa kufanya kazi zake vyema za kutoa maamuzi sahihi ya utendaji sahihi wa kazi za mwili.
Je, ni kweli kwamba uvutaji bangi hupunguza mawazo?
Bangi hupunguza mawazo kwa muda mfupi kwani huleta hisia za furaha na utulivu. Lakini hata hivyo matatizo hubakia palepale na mara nyingi huongezeka hapo baadaye. Watu wanaovuta bangi huikimbia dunia halisi na huingia dunia ya ndoto kwa muda fupi. Mara hisia zilizoletwa na bangi zinapoondoka, aghalabu matatizo huwa mabaya zaidi kuliko mwanzo. Matumizi ya bangi huahirisha na kuchelewesha tu utatuzi wa matatizo.
Je, kwanini watu watumiao madawa ya kulevya hupenda kuendelea kuyatumia?
Hii sasa ndiyo hatari ya madawa ya kulevya! Mara unapoyazoea unakuwa na ugumu wa kuendesha maisha yako bila madawa ya kulevya. Kwa madawa mengi ya kulevya ubongo huzoea kuwepo kwake kwenye damu na madawa zaidi na zaidi huhitajika ili kuendeleza hali hiyo. Hii ina maana kadri muda unavyoenda ndivyo unavyoongeza kiasi cha madawa ya kulevya unachokihitaji.
Pale utakapojaribu kupunguza kiasi cha matumizi ya madawa ya kulevya au kuacha kabisa unaweza ukapata matatizo ya kimaumbile au kiakili kutokana na kuacha kitu ulichozoea. Hali hii inaweza isiwe ya kufurahisha, yenye kuumiza na pengine hatari kwa maisha yako. Mara mtu anapoyazoea madawa ya kulevya haiwi tu tabia bali ugonjwa. Watu wengi wanaotegemea madawa ya kulevya hawayatumii kwa kujifurahisha bali kuzuia maumivu yasababishwayo na kuacha kitu ulichozoea. Njia nzuri ya kuzuia hali hii ni rahisi; KUWA JASIRI na SEMA HAPANA. Usijaribu madawa ya kulevya.
Kwa nini watu hutaka kufanya mapenzi baada ya kutumia madawa ya kulevya?
Madawa ya kulevya huathiri ubongo jinsi unavyofanya kazi. Hubadili hisia na husaidia kuondoa aibu na vizuizi vingine. Mtu hujisikia jasiri na mwenye nguvu na hivyo ni rahisi zaidi kwake kushawishika kufanya mapenzi kuliko asipoyatumia madawa hayo.
Kwa nini watu wanaotumia madawa ya kulevya wanadanganya?
Wengi wa waathirika wa madawa ya kulevya hukataa matatizo yao. Hudanganya kwa sababu hawataki kukubali matatizo yao pia hutoa maelezo kujitetea au kulaumu wengine. Mara nyingi huanza kudanganya au kusaliti marafiki na ndugu pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya kununulia madawa ya kulevya.
Je, kuna wataalamu Tanzania wanaowasaidia watu wenye matatizo ya madawa ya kulevya?
Ndiyo. Kuna mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayotoa ushauri nasaha kwa watumiaji wa madawa ya kulevya. Katika NGOs hizi kuna wataalamu wenye kusikiliza na kujaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo yako. Kama mtu anategemea madawa ya kulevya au anahitaji msaada wa kitaalamu, basi kuna vituo vya kuwasaidia kwenye hospitali za serikali. (anwani zao ziko kwenye ukurasa wa HUDUMA KWA AJILI YAKO kwenye tovuti hii).
Ni madawa yapi yaliyopigwa marufuku Tanzania na nini hutokea pale unapokamatwa?
Hapa Tanzania matumizi, umiliki, usafirishaji na kuhusika katika madawa ya kulevya kama vile bangi, heroini, kokaini na mirungi yamepigwa marufuku. Hii ni pamoja na madawa ambayo yamethibitishwa na daktari kuwa yasitumike kwa matibabu. Kwa Tanzania gongo pia ni haramu.
Polisi akimkamata mtu anayekwenda kinyume na sheria, humpeleka mbele ya vyombo vya sheria na ikithibitika kuwa ana hatia atahukumiwa kwa mujibu wa sheria. Sheria inatoa adhabu kali kwa makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya. Faini ya shilingi milioni 10 za kitanzania au kifungo cha maisha au vyote kwa pamoja.
Kwanini madawa hutengenezwa na kutumika hospitalini wakati yana madhara?
Baadhi ya madawa ya kulevya pamoja na madawa ya kutibu, hutumika hospitali kuokoa maisha na kupunguza maumivu. Hii inamaanisha kwamba wataalamu kama madaktari na wauguzi hudhibiti matumizi ya madawa haya, kwani watahakikisha kwamba madawa sahihi yanatumika, itakiwavyo na kwa vipimo sahihi.
Ni hatua zipi zinazochukuliwa na serikali kuhusu matumizi na biashara haramu ya madawa ya kulevya?
Serikali inatambua kukua kwa tatizo la madawa ya kulevya Tanzania, kwani madawa ya kulevya mengi yanayotumika yanapitishwa na kuingizwa kwa magendo nchini. Kutokana na hali hii serikali imepitisha sheria kuhusu tuhuma za madawa ya kulevya yaani sheria ya kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya ya mwaka 1995. Sheria hii inatoa maelekezo ya kumshughulikia mtuhumiwa wa madawa ya kulevya na hutoa adhabu kali kwa waliopatikana na hatia. Katika kusaidia vita dhidi ya madawa ya kulevya, Serikali ya Tanzania iliunda tume ya wataalamu mwaka 1996 iitwayo Tume ya Taifa ya kuzuia na kuratibu madawa ya kulevya ili kuendeleza vita hivyo.
Tume hii inawasaidia polisi, polisi wa mipakani na forodha ambao wanazuia usambazaji wa madawa ya kulevya kupitia ni mipakani na kuharibu mashamba ya bangi na mirungi. Wakala hawa kwa sasa wanafanya kazi bega kwa bega na nchi jirani ili kuzuia uingizaji wa madawa ya kulevya kupitia mipakani. Vile vile inaandaa wataalamu kwa kutumia NGO mbalimbali ambao kazi zao ni kuelimisha jamii kuhusu athari na hatari ya madawa ya kulevya na kuwasaidia waathirika.
Tume hii ya wataalamu vilevile inafikiria kuhusu kampeni za kitaifa zinazolenga kuelimisha kuhusu athari za madawa ya kulevya. Lakini kazi ya tume hii ni ngumu kutekelezwa kwani vita dhidi ya madawa ya kulevya ni jukumu la kila mtu na sio serikali peke yake. Inahitaji msaada kutoka kwa kila mtu na jamii kwa ujumla.
Nani wa kulaumiwa kuhusu madawa ya kulevya Tanzani: serikali, wasambazaji au watumiaji?
Hakuna mtu wa kulaumiwa, lakini inabidi kila mtu awajibike.Kila mtu inambidi afanye lolote lililo katika uwezo wake ili kupunguza madawa ya kulevya.
Serikali inabidi ihakikishe kwamba sheria zilizowekwa zinatekelezwa. Pia inatakiwa kuwasaidia walio na matatizo ya kimwili na kisaikolojia yaliyotokana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa kutoa vifaa na huduma za kiafya kwao.
Ni kweli kwamba watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya wanawasababishia watu wengine matatizo. Lakini kusingekuwa na usambazaji wake kama kusingekuwa na wahitaji. Hivyo basi mtumiaji anatakiwa awe na uamuzi wa kujali maisha na afya yake binafsi. Hii ndio sababu, watu hasa vijana wanatakiwa kuelimishwa kuhusu athari za madawa ya kulevya.
Kama nina rafiki au jamaa wa karibu ambaye ameathirika na utumiaji wa madawa ya kulevya je ninaweza kumbadili?
Endapo rafiki au jamaa anaomba msaada wa kuacha kutumia madawa ya kulevya unaweza kumsaidia kumpatia ushauri nasaha. Jitahidi kumpatia taarifa zote muhimu kuhusu madawa ya kulevya. Muhimu zaidi mweleze athari za matumizi ya madawa hayo. Hata wazazi unaweza kuwapatia ushauri endapo watatambua umuhimu wako wa kujali.
Wakati mwingine waathirika wa madawa ya kulevya hawako tayari kusikiliza ushauri na msaada wako. Inaweza kutokea muathirika akawa na hasira na hata kuvunja urafiki wenu. Usijilaumu!!! Kwa sababu ulijitahidi kumsaidia kadri ya uwezo wako na kwa faida ya rafiki yako. Rafiki huyo anaweza kugundua kuwa utumiaji wa madawa ya kulevya unamletea mwisho mbaya na hatimaye kuchukua uamuzi wa kueleza matatizo yake.
Kama itatokea rafiki au ndugu yako ambaye ni teja ameathirika sana kiafya usijaribu kumsaidia peke yako. Inaweza kuwa muhimu kumtafutia msaada wa kitaalamu kutoka kwa mtaalamu.