WATU watatu wanashikiliwa na Polisi kwa
tuhuma za mauaji ya mkazi wa Kijiji cha Inala One, Khalid Said na mkewe,
Amina Ali (50), akiwamo kaka wa mke huyo, Maganga Shakalambe (55).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Antony Rutta jana alitaja watuhumiwa wengine kuwa ni Jumanne Mohamed (30) na Mabula Masanja (33).
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kamanda Rutta alisema baada ya kuhoji watuhumiwa, walidai kuahidiwa Sh
milioni moja au ng’ombe wawili ili kufanya mauaji hayo na walikuwa
wapewe ng’ombe hao baada ya mauaji hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda Rutta, watumiwa hao walikiri kukodiwa na Maganga na mpango huo ulikuwapo tangu mwaka jana.
Mbali na watuhumiwa hao, Polisi pia
inashikilia watuhumiwa wengine 13 kwa tuhuma zingine za mauaji ya watu
wanane yaliyoripotiwa katika muda mfupi wa wiki mbili.
Kamanda Rutta alisema kukamatwa kwa
watuhumiwa hao kulitokana na jitihada za Polisi kwa kushirikiana na
Watanzania wema. Alisema Polisi wilayani Igunga ilikamata Sungusungu 11
kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu waliotuhumiwa kwa wizi wa simu aina
ya Nokia yenye thamani ya Sh 40,000 ulitokea Juni 13.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Rutta,
Sungusungu walipohojiwa walikiri kupeleka watuhumiwa wa wizi wa simu
porini kwa mahojiano na baada ya hapo waliwaua na kuwachoma moto.
Kamanda Rutta alitaja waliouawa kuwa ni Juma Shija, Paulo Tungu na Josia
Mashinji wakazi wa Nyandekwa.
Alisema baada ya Sungusungu hao kutoweka
baada ya mauaji, Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliwakamata juzi.
Kamanda Rutta pia alizungumzia tukio lingine la mauaji la Julai 9
katika Kijiji cha Ibutamisuzi, Igunga, ambapo inadaiwa Hamisi Ramadhani
(36) alimwua mkewe Perpetua Paul (46).
Alisema katika mauaji hayo, Ramadhani
alimfunga mkewe kitenge shingoni kwa nia ya kumning’iniza mtini ili
ionekane amejinyonga lakini alishindwa kufanya hivyo na badala yake
akamtelekeza barabarani.
Kamanda alisema asubuhi mwili wa
marehemu uliokotwa na wananchi na kumtilia shaka mumewe kwa kuwa siku ya
tukio walikuwa na ugomvi kwenye klabu cha pombe.
Kuhusu mauaji wa Ofisa Mifugo Severine
Tesha yaliyotokea Julai 6 mjini Tabora, Kamanda Rutta alisema watuhumiwa
wawili wanahojiwa.