Thursday, July 12, 2012

Polisi yawatisha Chadema

Ni kwa viongozi kukataa kuhojiwa
*Yasisitiza kuchunguza tuhuma zao
*Yaonya haitakubali kuyumbishwa

JESHI la Polisi limesema licha ya viongozi wa Chadema kukataa kuhojiwa, litaendelea kuchunguza tuhuma za chama hicho dhidi ya baadhi ya maofisa wa serikali na kuchukua hatua zaidi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jeshi hilo haliwezi kuyumbishwa na mtu au kikundi cha watu katika kutekeleza majukumu yake na litafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kukataa baadhi ya viongozi wake kuhojiwa ikisema haioni sababu ya kutii agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Dk. Nchimbi alitoa agizo hilo baada ya viongozi watatu wa Chadema, Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kudai baadhi ya maofisa usalama wa taifa wamekuwa wakiwafuatilia wakiwatishia kuwaua.

“Jeshi la polisi ni chombo cha umma kinachowajibika kulinda watu na mali zao, pia tunatekeleza kazi zetu kwa haki, usawa na bila ubaguzi wowote. Hili la viongozi wa Chadema kukataa kuhojiwa haliingii akilini hata kidogo.

“Kwa akili ya kawaida, chukulia mtu amevamiwa nyumbani kwake na majambazi akapiga kelele kuomba msaada na askari au watu wengine wakafika kumpatia msaada, kweli atashindwa kuwaelezea kilichompata?

“Hawa Chadema kukataa kwao hakutuzuii sisi kufanya kazi na hatuwezi kuyumbishwa na kikundi au mtu yeyote bali tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na maadili.

“…sitowaeleza sasa tunachokifanya ndani ya jeshi la polisi lakini baada ya uchunguzi wetu kukamilika tutafanya uamuzi… isitoshe katika malalamiko yao waliwataja watu kwa majina,”alisema Senso.

Taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi hilo zilidai kuwa hatua ya viongozi wa Chadema kukaidi kuhojiwa kunaweza kusababisha wakamatwe.

Juzi Dk. Slaa alitangaza kwamba hakubaliani na agizo la Dk Nchimbi kutaka kuwahoji kwa kuwa akisema kuwa yeye na wenzake hawana tena imani na vyombo vya serikali ikiwamo polisi.

Dk. Slaa alilitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wake lenyewe kuhusiana na madai yao na kutoa tamko na sio kuwahoji wao ambao ndio walalamikaji.

Alisisitiza kwamba Chadema hakina imani na polisi kwa kuwa wamekuwa wakipuuza malalamiko wanayopelekwa na chama hicho.

Chadema imekuwa ikiwasilisha madai yake mengi polisi yakiwamo ya wabunge wake kupigwa mkoani Mwanza lakini hakuna hatua zilizochukuliwa, alisema.

Dk. Slaa alisema kama Serikali isipokaa vizuri katika usalama wa raia wake na kutimiza wajibu na ahadi zake kwa Watanzania, taifa litakwenda pabaya.

Naye Msaidizi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka ambaye ni mmoja wa maofisa usalama aliyetajwa kuhusika kuwatisha viongozi hao wa Chadema amekwisha kutoa kauli akidai kuwa malalamiko ya viongozi wa CHADEMA ni propaganda za siasa na zinapaswa kupuuzwa