Ni kwa viongozi kukataa kuhojiwa
*Yasisitiza kuchunguza tuhuma zao
*Yaonya haitakubali kuyumbishwa
JESHI
la Polisi limesema licha ya viongozi wa Chadema kukataa kuhojiwa,
litaendelea kuchunguza tuhuma za chama hicho dhidi ya baadhi ya maofisa
wa serikali na kuchukua hatua zaidi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jeshi hilo haliwezi
kuyumbishwa na mtu au kikundi cha watu katika kutekeleza majukumu yake
na litafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili.
Kauli hiyo
imetolewa siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kukataa baadhi ya
viongozi wake kuhojiwa ikisema haioni sababu ya kutii agizo la Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Dk. Nchimbi alitoa agizo
hilo baada ya viongozi watatu wa Chadema, Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa,
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema kudai baadhi ya maofisa usalama wa taifa wamekuwa
wakiwafuatilia wakiwatishia kuwaua.
“Jeshi la polisi ni chombo
cha umma kinachowajibika kulinda watu na mali zao, pia tunatekeleza kazi
zetu kwa haki, usawa na bila ubaguzi wowote. Hili la viongozi wa
Chadema kukataa kuhojiwa haliingii akilini hata kidogo.
“Kwa
akili ya kawaida, chukulia mtu amevamiwa nyumbani kwake na majambazi
akapiga kelele kuomba msaada na askari au watu wengine wakafika kumpatia
msaada, kweli atashindwa kuwaelezea kilichompata?
“Hawa Chadema
kukataa kwao hakutuzuii sisi kufanya kazi na hatuwezi kuyumbishwa na
kikundi au mtu yeyote bali tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na
maadili.
“…sitowaeleza sasa tunachokifanya ndani ya jeshi la
polisi lakini baada ya uchunguzi wetu kukamilika tutafanya uamuzi…
isitoshe katika malalamiko yao waliwataja watu kwa majina,”alisema
Senso.
Taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi hilo zilidai kuwa
hatua ya viongozi wa Chadema kukaidi kuhojiwa kunaweza kusababisha
wakamatwe.
Juzi Dk. Slaa alitangaza kwamba hakubaliani na agizo
la Dk Nchimbi kutaka kuwahoji kwa kuwa akisema kuwa yeye na wenzake
hawana tena imani na vyombo vya serikali ikiwamo polisi.
Dk. Slaa
alilitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wake lenyewe kuhusiana na
madai yao na kutoa tamko na sio kuwahoji wao ambao ndio walalamikaji.
Alisisitiza kwamba Chadema hakina imani na polisi kwa kuwa wamekuwa wakipuuza malalamiko wanayopelekwa na chama hicho.
Chadema
imekuwa ikiwasilisha madai yake mengi polisi yakiwamo ya wabunge wake
kupigwa mkoani Mwanza lakini hakuna hatua zilizochukuliwa, alisema.
Dk.
Slaa alisema kama Serikali isipokaa vizuri katika usalama wa raia wake
na kutimiza wajibu na ahadi zake kwa Watanzania, taifa litakwenda
pabaya.
Naye Msaidizi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka ambaye ni
mmoja wa maofisa usalama aliyetajwa kuhusika kuwatisha viongozi hao wa
Chadema amekwisha kutoa kauli akidai kuwa malalamiko ya viongozi wa
CHADEMA ni propaganda za siasa na zinapaswa kupuuzwa