Thursday, July 12, 2012

Walimu hawajatangaza mgogoro na serikali.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Kassim Majaliwa, aliliambia Bunge kuwa si kweli kwamba walimu wametangaza mgogoro na serikali.
Majaliwa alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), aliyeitaka serikali kutoa tamko ni lini itamaliza mgogoro wake na walimu ili kuepusha migogoro inayojirudia.
Alisema suala hilo ni la msingi ambalo kila mtumishi anahitaji kujua na hasa walimu na kwamba ili watumishi hao waingie katika mgogoro, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, itahakikisha kuwa inamaliza matatizo ya walimu.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Iramba Mashariki, Salome Mwambu (CCM), alitaka kujua serikali itamaliza lini matatizo ya walimu ili nao waishi kama wafanyakazi wengine wa serikali.
Pia alitaka kufahamu kuwa serikali itachukua hatua gani kwa wakurugenzi watendaji wanaochelewa kuwasilisha taarifa ‘Seniority list’ ambayo hutumika kupandisha vyeo vya watumishi.
Kuhusu hilo, Majaliwa alisema jumla ya sh bilioni 15.8 zilitengwa katika mwaka wa fedha 2011/12 kwa ajili ya kumaliza tatizo la madai ya walimu nchini na kati ya fedha hizo sh 131.5 zilipelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Alisema serikali inatambua umuhimu mkubwa katika kada ya walimu na kuthamini mchango wao katika kutoa elimu nchini na kwamba imekuwa ikiboresha huduma kwa watumishi wake wakiwamo walimu.