Tuesday, July 24, 2012

Wabunge watoro wakalia kuti kavu

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, ametangaza utaratibu mpya ambao utawabana vikali wabunge watoro wanaokwepa kuhudhuria vikao vya Bunge bila sababu.

Kwa mujibu wa utaratibu huo mpya, kuanzia sasa kila mbunge atawajibika kujisajili mara mbili kwa siku, wakati wa asubuhi na kipindi cha jioni.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Bunge kushindwa kupitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo mwishoni mwa wiki kutokana na idadi ya wabunge kutokidhi matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge.

Akihairisha Bunge jana kwa mapumziko ya mchana, Spika Makinda, aliwatangazia wabunge kuwa kuanzia sasa watapaswa kujaza fomu za kujisali mahuduria yao wakati wa mchana, na kudai kuwa sababu za kufanya zinaeleweka, hivyo hapaswi kuzitaja.

Hata hivyo, wakati akitangaza mkakati huo, idadi ya wabunge ukumbini ilikuwa imepungua sana kutokana na wengi wao kuondoka mara baada ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara ya kilimo.

Pamoja na utaratibu huo mpya, Spika Makinda hakusema adhabu gani itatolewa kwa mbunge atakayebainika kutoroka vikao vya Bunge. Aidha, Katibu wa Bunge, Thomas Kashililla, hakupatikana kutoa ufafanuzi wa hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakaopuuzia kutimiza sharti hilo hipya.

Wabunge wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutoroka vikao vya Bunge na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli zao binafsi.

Aidha, wabunge wengi wamekuwa wakidaiwa kutumia vikao vya Bunge kuendesha shughuli nyingine za kisiasa, ikiwemo kuendesha malumbano yenye mwelekeo wa kibinafsi kwa malengo ya kujiimarisha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hivi karibuni Spika Makinda alilazimika kutoa onyo kali kwa wabunge kufuatia kuongezeka kwa utoro huo, lakini haikusaidia lolote kudhibiti hali hiyo.