Thursday, July 12, 2012

'Waliowachinja' mke, mume wakamatwa

WATU watatu wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa Kijiji cha Inala One, Khalid Said na mkewe, Amina Ali (50), akiwamo kaka wa mke huyo, Maganga Shakalambe (55).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Antony Rutta jana alitaja watuhumiwa wengine kuwa ni Jumanne Mohamed (30) na Mabula Masanja (33).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Rutta alisema baada ya kuhoji watuhumiwa, walidai kuahidiwa Sh milioni moja au ng’ombe wawili ili kufanya mauaji hayo na walikuwa wapewe ng’ombe hao baada ya mauaji hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda Rutta, watumiwa hao walikiri kukodiwa na Maganga na mpango huo ulikuwapo tangu mwaka jana.
Mbali na watuhumiwa hao, Polisi pia inashikilia watuhumiwa wengine 13 kwa tuhuma zingine za mauaji ya watu wanane yaliyoripotiwa katika muda mfupi wa wiki mbili.
Kamanda Rutta alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na jitihada za Polisi kwa kushirikiana na Watanzania wema. Alisema Polisi wilayani Igunga ilikamata Sungusungu 11 kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu waliotuhumiwa kwa wizi wa simu aina ya Nokia yenye thamani ya Sh 40,000 ulitokea Juni 13.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Rutta, Sungusungu walipohojiwa walikiri kupeleka watuhumiwa wa wizi wa simu porini kwa mahojiano na baada ya hapo waliwaua na kuwachoma moto. Kamanda Rutta alitaja waliouawa kuwa ni Juma Shija, Paulo Tungu na Josia Mashinji wakazi wa Nyandekwa.
Alisema baada ya Sungusungu hao kutoweka baada ya mauaji, Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliwakamata juzi. Kamanda Rutta pia alizungumzia tukio lingine la mauaji la Julai 9 katika Kijiji cha Ibutamisuzi, Igunga, ambapo inadaiwa Hamisi Ramadhani (36) alimwua mkewe Perpetua Paul (46).
Alisema katika mauaji hayo, Ramadhani alimfunga mkewe kitenge shingoni kwa nia ya kumning’iniza mtini ili ionekane amejinyonga lakini alishindwa kufanya hivyo na badala yake akamtelekeza barabarani.
Kamanda alisema asubuhi mwili wa marehemu uliokotwa na wananchi na kumtilia shaka mumewe kwa kuwa siku ya tukio walikuwa na ugomvi kwenye klabu cha pombe.
Kuhusu mauaji wa Ofisa Mifugo Severine Tesha yaliyotokea Julai 6 mjini Tabora, Kamanda Rutta alisema watuhumiwa wawili wanahojiwa.