Friday, August 31, 2012

Wahadzabe walikula pundamilia 18 ili kushiriki sensa

 
Vijana wa Kihadzabe wakicheza ngoma.

HIVI karibuni kabila la Wahadzabe lililopo lilizua gumzo baada ya kutoa sharti la kupatiwa nyama ya tumbili ili liweze kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi.

Tofauti na matarajio ya watu kwamba viongozi wa kabila hilo wangekamatwa na Dola kwa kitendo cha kuipa Serikali masharti ambayo ni kinyume na sheria ya sensa, Serikali ilikubali kulipatia kabila hilo nyama ya pundamilia 18 badala ya tumbili jambo lililofanikisha kujenga mazingira rafiki yaliyowezesha Wahadzabe kuhesabiwa.

Ingawa Serikali ingeweza kukataa sharti hilo, viongozi walitumia busara kwa kuzingatia mambo mbalimbali hasa sifa za kipekee za kabila hilo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa makazi ya kudumu. Kabila hilo halina utaratibu wa kuhodhi mali kwa kuwa haliwekezi katika mifugo, biashara wala kilimo.

Ni dhahiri kuwa wasingetimiza masharti yao isingekuwa rahisi kuwapata na kuwahesabu kwa kuwa ni wachache na hawana makazi maalumu. Kabila la Wahadzabe ni miongoni mwa makabila madogo yaliyopo katika hatari ya kutoweka kwa kuwa watu wake hawaongezeki kwa kasi ikilinganishwa na makabila mengine.

Hadza au Wahadzabe ni kabila linaloishi Kaskazini ya Kati Tanzania wanoishi kuzunguka Ziwa Eyasi eneo la Karatu, Mkoa wa Manyara, pia wanapatikana Mbulu, Iramba, Meatu na Maswa. Kabila hilo ni jamii pekee nchini Tanzania inayoishi kwa kutumia mfumo wa binadamu wa kale ambapo wanaishi kwa kutegemea uwindaji pamoja na kukusanya mizizi na matunda ya pori kama chakula kikuu.

Tofauti na makabila mengine ambayo yanajihusisha na kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara na shughuli mbalimbali za kuingiza kipato, shughuli kubwa ya wanaume wa Kihadzabe huwinda kwa kutumia upinde na mshale. Wanawake wanajihusisha na ukusanyaji wa mboga, mizizi na matunda pori kisha kukusanyika pamoja na kula kisha kukaa kwa ajili ya kusubiri kesho.

Wanawake wa Kihadzabe wakishamaliza kukusanya mizizi na matunda kugonga na kusaga mbegu za ubuyu kisha kutumia unga wake kutengenezea uji. Wakati wanaume hutumia muda wao kutengeneza upinde na mishale.

Kwa kifupi kabila hilo halijui thamani wala karaha ya kukosa fedha kwa sababu linaishi maisha ya kipekee katika maeneo ya nyikani ambapo hakuna matumizi ya kujenga nyumba, samani za ndani, kununua nguo, chakula wala gharama za matibabu.

Mwandishi wa Kitabu cha utamaduni mila na desturi za makabila ya Kaskazini Mashariki ya Tanzania Gervase Mlola anasema mfumo wa maisha ya Wahadzabe unajenga imani kuwa kabila hilo ni masalia ya binadamu wa kwanza ambaye aliishi kwa kula nyama, mizizi na matunda.

Pia utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa masalia ya mifupa ya mwanadamu wa kwanza aliyeishi miaka milioni 4 iliyopita yalipatikana katika makazi ya Wahadzabe jambo linalothibitisha kuwa kizazi cha kabila hilo kina uhusiano wa moja kwa moja na binadamu wa kwanza.

Mlola anasema watu wa kabila hilo wana miili midogo, ni weusi na wana chale kwenye mashavu. Hata hivyo watu wa kabila hilo hawatogi masikio, hawavai wala hawaweki chochote masikioni kama ilivyo kwa makabila mengine yanayoishi maeneo ya jirani.

Utafiti uliyofanywa kuhusu kukua kwa jamii za Kiafrika zilizostaarabika unaonesha kuwa Wahadzabe ambao ni maarufu kwa jila na Watindiga waliishi katika ardhi ya Tanzania kwa miaka mingi kabla ya kuingia kwa kizazi cha watu jamii ya Wabantu ambao mfumo wao wa maisha ulikuwa tofauti kwa kuwa walistaarabika zaidi na kutumia zana za kisasa. Lugha ya Wahadzabe inaju

likana kama Khoisan ambayo ni sawa na watu jamii nyingine zinazozungumza lugha Afrika ya Kusini, Wasandawe wanaishi Kondoa katika Mkoa wa Dodoma ndio kabila pekee lenye uhusiano wa karibu na Wahadzabe. Inasemekana kuwa miaka ya nyuma Wasandawe waliishi kwa kuwinda na kukusanya matunda ila hivi sasa wamebadilika kulingana na mabadiliko ya mfumo wa maisha.

Mila na desturi za kabila la Wahadzabe zinarithiwa na kizazi kipya bila kufanya mabadiliko makubwa jambo linalosababisha
kabila kuwa na mfumo wa kizamani ambao ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo. Upinde na mshale ni jambo la muhimu na la lazima kurithiwa na vijana wa kiume katika jamii ya Wahadzabe.

Kila mwanamume ana upinde na mishale ya kutosha yenye sumu kwa ajili ya kuwinda wanyama wakubwa na isiyokuwa na sumu kwa ajili ya wanyama wadogo kama digidigi na swala. Wahadzabe wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu bila kutawaliwa.

Tofauti na makabila mengine, Wahadzabe hawana utawala unaotegemea kiongozi wa kisiasa, kimila wala mganga wa jadi kwa ajili ya kuita mvua wala kuponya watu. Wanaishi katika makundi ambayo yana msemaji mmoja au wawili. Wasemaji huchaguliwa kutoka rika lolole ila ni lazima awe na uwezo wa kujieleza.

Hata hivyo wakati wa majadiliano kila mtu anapata nafasi sawa na maamuzi yanatolewa kwa kuzingatia kundi kubwa pasipo na kiongozi wa kutoa ushawishi kwa kundi moja kuunga mkono kundi lingine. Ingawa hawana uongozi huishi kwa kuheshimiana na kila mtu anajua wajibu wake pasipo kusukumwa.

Wahadzabe wanaishi katika makambi ya muda mfupi ambapo kambi moja hukaa watu wazima takribani 30. Kambi hupewa jina la mtu maarufu katika kambi husika na mtu huyo huchukuliwa kama kiongozi ingawa hana sauti wala uwezo wa kutoa maamuzi dhidi ya wenzake.

Kabila hilo kutembea kwa makundi ili kuweza kukabiliana na hatari hasa wanyama wakali wakati wa kuwinda. Wakiwinda
wanyama wadogo watamchinja na kuwagawa nyama kwa uwiano sawa kisha kila mtu hupeleka nyama hiyo kwenye familia yake.

Endapo watafanikiwa kuua mnyama mkubwa kama nyati wataitana na kundi nzima litakaa eneo la tukio watu kwa ajili ya kuchinja na kula nyama kwa pamoja. Kwa Mhadzabe hakuna kinachotupwa, baada ya kula nyama hutumia ngozi kutengenezea mavazi pia husaga mifupa na kutoa mafuta na baadhi ya mifupa hutumia kutengeneza ncha za mishale ya kuwindia.

Baadhi ya ncha za mishale hupakazwa sumu kwa ajili ya kuwinda wanyama wakubwa. Utengenezaji wa mishale ya sumu
hufanyika kitaalamu na ujuzi huo unarithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Utafiti unaonesha kuwa kabila hilo halikuathiriwa na mfumo dume.

Wanawake na wanaume hushiriki katika shughuli za kijamii kisha hugawana chakula pasipo ubaguzi wa kijinsia. Katika jumuiya ya Wahadzabe hakuna anayepatwa na njaa. Wahadzabe wote huwa na tabia ya kuvuta tumbaku. Waume kwa wanawake, wazee kwa vijana, wote wanapokaa katika kikundi huwa na kawaida ya kushirikiana kuvuta mtemba maarufu kama kiko ambacho hutengenezwa kutokana na mawe laini.

Vijana wa kiume ndiyo huwa na jukumu la kuteka maji kisha kwenda kuwinda ndege kwa kutumia mishale. Ndege hao hunyonyolewa manyoya na kuchomwa. Manyoya hutumika kutengenezea mishale na kwa kawaida hakuna kinachotupwa kutokana na ndege au mnyama aliyewindwa.

Kwa kuwa Wahadzabe wanazingatia na kuthamini mfumo wa ikilojia hujenga makazi yao mbali na vyanzo vya maji ili kuepuka
kuharibu vyanzo vya maji, kutisha wanyama pia kujiepusha na wadudu wanaoeneza maradhi hususan malaria. Tofauti na makabila mengine, Wahadzabe hawana tabia ya kujiona wao ni bora kuliko wanyama.

Wao wanaamini katika ikolojia kwamba ardhi, wanyama na mimea ni vitu vinavyotegemeana na hakuna chenye ubora kuliko
kingine. Huishi kwa kushirikiana bila kubadili wala kuharibu mazingira. Kila kitu hutumiwa kwa faida ya wote.

Ingawa wana mila ngumu, vijana huweza kumudu changamoto za maisha bila taabu. Watoto wa Kihadzabe, wenye umri kuanzia miaka nane wanaweza kujitafutia maisha yao na hata familia zao kwa kuwa hujifunza kazi za wakubwa wangali na
umri mdogo.

Uwindaji ni sehemu ya starehe kwa vijana wa Kihadzabe. Pia wana ujuzi wa kutengeneza visu vya vyuma ambavyo vinafanana na zana za kale enzi za mawe. Jioni ni muda wa kupumzika. Vijana huwa na kazi ya kuwasha moto na kuchoma nyama. Wazee huota moto kwa kuuzunguka.

Pia wanapata muda wa kucheza pamoja na kufurahi. Wakati wa kucheza huweka mduara kisha kucheza na kuimba huku wakipiga makofi na kuzunguka duara. Pia wana ngoma ambazo hutumia vifaa mbalimbali vya muziki. Wanapokuwa na tatizo hushikamana na kushirikiana hasa kwa kusali nyakati za usiku ili Mungu aweze kusikia kilio chao na kuwaondolea tatizo.

Ingawa ni jamii iliyopo nyuma kimaendeleo zipo ishara zinazoonesha kuwa walikuwa na ujuzi fulani katika kufanya mawasiliano. Wakati wa kurina asali Wahadzabe wanawasha moto unaotoa moshi mzito ili kuwafukuza nyuki kisha kurina asali pasipo kushambuliwa na nyuki.

Kila wanapomaliza kurina asali hasa kwenye mibuyu walichonga vijiti mithili ya msumari kisha kuvipigilia kwenye mbuyu kama ishara kuwa Mhadzabe aliwahi kurina asali kwenye mti huo. Hadi miaka ya hivi karibuni Wahadzabe wamekuwa wakichora kwenye miamba, kama yanavyofanya makabila mengine yaishiyo jirani.

Ingawa hawana kiongozi wa kiimani, Wahadzabe wanamkusanyiko wa hadithi, zinazoelezea miiko na imani kuhusu maisha
yao. Kwa mujibu wa hadithi hizo kabila hilo linaongozwa na mungu anayefahamika kwa jina la Ishoko. Ishoko amekuwepo tangu mwanzo wa dahari na kusaidia kizazi kimoja kwenda kingine.

Ishoko ambaye ni rafiki wa ambaye amewezesha watu wote kukua vyema na kufahamu mambo mbalimbali hasa mema
na mabaya. Anafundisha watu kujua kazi na wajibu wa kila mtu kulingana na mila na desturi, pia anatunza mazingira kwa kuzingatia uwiano wa ikolojia.

Ishoko anafananishwa na malaika ambaye aliweza kuwatoa Wahadzabe kwenye umbo la awali lililokuwa sawa na la mnyama na kuwaweka katika hali ya ubinadamu. Ishoko aliwawezesha kuondokana na mateso ya kula nyama mbichi kwa kuwapatia moto.

Wanaamini kuwa hata bakuli na mkuki wa kwanza ulitengenezwa na malaika kisha kuwafundisha jinsi ya kutumia kwa lengo la kuboresha maisha. Ni rahisi kuwatambua Wahadzabe kwa mavazi yao. Bado wanavaa nguo zilizotengenezwa kwa vipande vya ngozi zinazotokana na wanyama mbalimbali.

Wanaume wanaokwenda mawindoni huvaa ngozi nene ya baboon. Wahadzabe walioendelea wanavaa kaptula na wanawake wanajifunga vipande vya khanga na vitenge. Ila wengi wao wanavaa vipande vya ngozi vilivyolainishwa vizuri kisha kunakishiwa na shanga za njano, nyeupe na bluu bahari.

Ingawa wana mila ngumu mabadiliko ya mfumo wa maisha hasa mpango wa Serikali wa kuendeleza watu wake unaathiri
mfumo, mila na desturi za maisha ya Wahadzabe. Athari hizo zinaonekana kupitia programu za elimu ambapo hivi sasa watoto wengi wanaandikishwa shule. Jambo hilo linasababisha wazazi wao kujihusisha na shughuli za kuwaingizia kipato ili waweze kununua sare na kulipa ada za shule. Vijana wachache wa Kihadzabe wanapopata elimu wanahama katika makazi duni na kuishi maeneo mengine yenye maendeleo kisha kuhawahamisha wazazi wao ili nao waweze kujionea dunia katika taswira tofauti na maisha ya kula nyama na mizizi.