Friday, August 31, 2012

Vituo vya ‘kuchimba dawa kwa abiria wa mabasi vyatangazwa



ABIRIA wa mabasi yaendayo mikoani kuanzia kesho watalazimika kuwa na fedha za ziada mifukoni kwa ajili ya kulipia huduma ya choo.

Fedha hizo zitatumiwa kulipia huduma hiyo baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), kutangaza rasmi kwamba utaratibu wa abiria kushuka maporini na kujisaidia imepigwa marufuku.

Katika Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri uliomalizika hivi karibuni Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kukataza ‘uchimbaji dawa’ porini ifikapo leo.

Baada ya agizo hilo, Mamlaka hiyo ilifanya kikao na wasafirishaji ili kuweka mikakati kwa pamoja juu ya utekelezaji wake ambapo maeneo ya kujisaidia yalibainishwa ili abiria wajulishwe.

Hivyo kwa mujibu wa tangazo la Sumatra kwenye vyombo vya habari jana, vituo kadhaa viliainishwa katika barabara tano kuu ambazo kwa upande wa barabara ya Dar es Salaam – Mbeya, vituo vilivyoainishwa ni vya mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na Njombe.

Vituo hivyo ni Ruvu iliko hoteli inayotoa huduma hiyo bure, Chalinze kuna hoteli inahudumia kwa Sh 200; stendi kuu ya mabasi ya Msamvu huduma inatolewa kwa Sh 200 na Ruaha Mbuyuni Hoteli ya Al Jazeera inatoa huduma bure.

Kitonga, Hoteli ya Confort inahudumia bure, stendi ya Ipogoro malipo ni kati ya Sh 100 na 200, Mafinga abiria watalazimika kulipia kiasi kama hicho na Makambako malipo yatakuwa kati ya Sh 200 na 300.

Katika njia ya Dar es Salaam - Mwanza; ambapo magari yanapitia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida,Tabora na Shinyanga, ‘dawa itachimbwa’ Msamvu, Gairo kuna hoteli ambayo inahudumia bure, Badueli umbali wa kilometa tatu kutoka Dodoma mjini pia huduma ni ya bure.

Singida mjini iliko stendi ya mabasi huduma hiyo pia itapatikana kwa malipo ya Sh 200, kituo cha mabasi Nzega mjini huduma italipiwa Sh 200 na katika stendi kuu mjini Tabora malipo ni Sh 200 pia.

Katika stendi kuu ya mabasi Shinyanga mjini, huduma hiyo italipiwa Sh 200 na kwa waendao Kagera kupitia Kahama huduma itapatikana stendi kuu ya mabasi kwa kati ya Sh 200 na 300 huku Mwanza mjini katika stendi kuu ya mabasi pia huduma italipiwa Sh 200.

Kwa waendao Kagera baada ya kutoka Kahama, huduma zitapatikana Ushirombo kwa Sh 100 na Sh 500 ambapo pia watapata fursa ya kuoga, Chato Sh 200, Muleba Sh 200 na Bukoba Sh 200.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa abiria watokao Kigoma kabla ya kufika Kahama watahudumiwa Kasulu kwa Sh 200, Kibondo kwa Sh 200 na Runzewe kwa Sh 200 pia.

Upande wa njia ya Dar es Salaam -Tanga, abiria watahudumiwa katika kituo cha mizani Msata bila gharama yoyote sawa na Segera.

Kwa njia ya Dar es Salaam - Moshi, Arusha na Manyara, huduma zitapatikana Korogwe katika hoteli mbili bila malipo na Mombo ambako pia kuna hoteli isiyotoza malipo. Lakini Same, Mwanga, Himo, Moshi Mjini na Boma Ng’ombe, huduma itatolewa kwa Sh 200 na Arusha huduma itapatikana stendi kuu kwa Sh 200 sawa na ilivyo kwa Manyara.

Njia ya Dar es Salaam-Lindi-Mtwara, eneo la Nangurukuru kuna hoteli iitwayo StarCom ambayo itatoa huduma bila malipo, ambapo Lindi huduma hiyo haitalipiwa huku Mtwara ikilipiwa Sh 200 ingawa haitoshelezi mahitaji.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema lolote kuhusu watoto na wale ambao wana matatizo ya kupata haja ndogo kila baada ya muda mfupi.