Tuesday, August 21, 2012
Aliyemrithi Rostam kung’olewa ubunge?
Dk Dalali Kafumu
BAADA ya aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), kujiuzulu wadhifa huo na kusababisha uchaguzi mdogo uliompa ushindi mgombea wa CCM, Dk Dalali Kafumu, leo kitendawili cha uhalali wake kitajulikana.
Hilo linatarajiwa kujulikana wakati hukumu ya kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye kupinga matokeo yaliyompa ushindi Dk Kafumu itakaposomwa katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Tabora kuanzia saa tatu asubuhi.
Hukumu hiyo ina mvuto wa pekee kwa kuwa inatarajiwa kuacha wapenzi na wanachama wa Chadema au CCM wakicheka au kulia.
Chadema wanatarajia hukumu hiyo iwe upande wao, yaani Dk Kafumu ashindwe ili uchaguzi wa jimbo hilo ambalo, Kashindye alitoa ushindani mkubwa kwa mgombea wa CCM urudiwe, wakati CCM wakitarajia ushindi.
Mbali na Dk Kafumu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi huo, Protace Magayane. Shauri hilo lilianza kusikilizwa rasmi Machi 26 na Jaji Mary Shangali.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Sylvester Kainda alisema Mahakama Kuu ilipanga hukumu hiyo isomwe jana lakini kwa kuwa ilikuwa Sikukuu ya Idd, sasa inasomwa leo.
Wakili wa mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari kwa njia ya simu yake ya mkononi alisema zaidi ya malalamiko 13 yaliwasilishwa katika Mahakama hiyo.
Profesa Safari alisema baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, waliiachia Mahakama itoe uamuzi, “tumeiachia Mahakama itatoa hukumu, kwani kila kitu tumekiwasilisha na mashitaka hayo yote yalisikilizwa.’’
Dk Kafumu katika kesi hiyo aliwakilishwa na mawakili wawili; Antony Kanyama na Kayaga Kamaliza. Moja ya malalamiko katika kesi hiyo ni pamoja na vitisho katika uchaguzi huo mdogo, ahadi za ujenzi wa daraja la Mbutu na kugawa mahindi.
Katika kesi hiyo baadhi ya mawaziri, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba walitoa ushahidi.
Wengine ni Mweka Hazina wa CCM, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage. Waziri Simba akiwa shahidi wa 16 kwa upande wa mshitakiwa alitoa ushahidi wa kula chakula na wanachama wa CCM katika Hospitali ya Nkinga Kata ya Inkiga.
Alikiri kula na watu zaidi ya 50 hali ambayo mawakili wa mlalamikaji waliendelea kumhoji wakihusisha maneno aliyotamka kuwa ‘msimchague Kashindye kwani hana mke pia ni masikini’, hata hivyo Waziri huyo alikanusha kutoa kauli hiyo.
Akiwa shahidi wa 15 upande wa washitakiwa, Rage alikiri kushiriki kampeni hizo za uchaguzi akipangiwa kata za tarafa ya Igulubi.
Wakili wa mlalamikaji alimhoji shahidi huyo juu ya umiliki wa bastola na kwa nini alikuwa nayo katika mikutano ya kampeni ambayo alishiriki. Rage alikiri kumiliki bastola na kuwa nayo katika shughuli nzima za kampeni wakati huo.
Hata hivyo, alisema upepo ulimponza ulipopeperusha shati lake na bastola hiyo kuonekana hadharani na vyombo vya habari kumpiga picha sawia.