WATU sita wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mtoto wa
siku moja mwili wake kuokotwa ukiwa umeliwa na mbwa sehemu za siri na
mguu wa kulia, na tukio jingine la mwanamume kujinyonga baada ya kuugua
kwa miaka tisa bila kupona.
Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile, alisema tukio la kwanza lilitokea Julai 15, mwaka
huu, saa 10 jioni, katika eneo la Shule ya Msingi Mlambankata, Ifakara,
wilayani Kilombero, likimuhusisha mtoto wa siku moja.
Alisema
mwili wa mtoto huyo uliokotwa katika eneo hilo ambapo ulishindwa
kufahamika jinsia baada ya sehemu zake za siri pamoja na mguu wa kulia
kuliwa na mbwa na uchunguzi unaendelea kubaini wazazi wa mtoto huyo na
sababu ya kifo chake.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kisumbi,
Elias Albin (60), amekutwa amekufa baada ya kujinyonga katika mti
nyumbani kwake, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuugua miaka tisa bila
kupona.
Alisema tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa
nane mchana, katika Kitongoji cha Kisumbi, Tarafa ya Luhembe wilayani
Kilosa, ambako mwanamume huyo alijinyonga kwa kutumia kamba ya magamba
ya miti, baada ya kuugua ugonjwa wa kichwa na kupooza miguu kwa muda
mrefu.
Katika tukio jingine, alisema Rozalia Muhuhuvale (59),
mkulima na mkazi wa Kilongo, Mngeta wilayani Kilombero, alikutwa amekufa
baada ya kujinyonga katika mti ulipo pembezoni mwa nyumba yake.
Alisema
tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa tisa alasiri mchana,
katika eneo la Kilongo, ambapo mwanamke huyo alijinyonga kwa kutumia
kamba ya manila pamoja na kanga yake na chanzo bado hakijafahamika.
Katika
tukio jingine, alisema wapanda pikipiki wawili, Dotto Selemani (23) na
Mhira Berati (23), ambao ni wakazi wa Wami Dakawa, wilayani Mvomero,
walifariki dunia papo hapo baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria
kugongwa na gari.
Alisema watu hao waligongwa Julai 15, mwaka
huu, saa tisa usiku katika eneo la Kwamwarabu, Mvomero, Barabara ya
Morogoro kwenda Dodoma na gari lenye namba za usajili T361 BPE
Mistubishi Fuso, lililokuwa likiendeshwa na Mohamed Tore (30), ambaye ni
mkazi wa Dar es Salaam.
Aliitaja pikipiki hiyo kuwa ina namba za
usajili T539 ART, aina ya beta, iliyokuwa ikiendeshwa na Doto Selemani,
ikitoka Morogoro mjini kuelekea Wami Dakawa na chanzo cha ajali hiyo ni
mwendo kasi wa dereva wa gari hilo.
Katika tukio jingine, mpanda
baiskeli, Faraji Nyato (28) ambaye ni mkazi wa Dumila, wilayani Kilosa,
alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Dumila,
baada ya kugongwa na pikipiki yenye namba za usajili T647 BVD.
Alisema
tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa moja usiku katika Mtaa wa
Pointi Dumila na dereva wa pikipiki hiyo hajafahamika baada ya
kukimbia.