Tuesday, July 17, 2012

Mtoto mchanga aliwa sehemu zake za siri

WATU sita wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mtoto wa siku moja mwili wake kuokotwa ukiwa umeliwa na mbwa sehemu za siri na mguu wa kulia, na tukio jingine la mwanamume kujinyonga baada ya kuugua kwa miaka tisa bila kupona.

Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema tukio la kwanza lilitokea Julai 15, mwaka huu, saa 10 jioni, katika eneo la Shule ya Msingi Mlambankata, Ifakara, wilayani Kilombero, likimuhusisha mtoto wa siku moja.

Alisema mwili wa mtoto huyo uliokotwa katika eneo hilo ambapo ulishindwa kufahamika jinsia baada ya sehemu zake za siri pamoja na mguu wa kulia kuliwa na mbwa na uchunguzi unaendelea kubaini wazazi wa mtoto huyo na sababu ya kifo chake.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kisumbi, Elias Albin (60), amekutwa amekufa baada ya kujinyonga katika mti nyumbani kwake, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuugua miaka tisa bila kupona.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa nane mchana, katika Kitongoji cha Kisumbi, Tarafa ya Luhembe wilayani Kilosa, ambako mwanamume huyo alijinyonga kwa kutumia kamba ya magamba ya miti, baada ya kuugua ugonjwa wa kichwa na kupooza miguu kwa muda mrefu.

Katika tukio jingine, alisema Rozalia Muhuhuvale (59), mkulima na mkazi wa Kilongo, Mngeta wilayani Kilombero, alikutwa amekufa baada ya kujinyonga katika mti ulipo pembezoni mwa nyumba yake.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa tisa alasiri mchana, katika eneo la Kilongo, ambapo mwanamke huyo alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila pamoja na kanga yake na chanzo bado hakijafahamika.

Katika tukio jingine, alisema wapanda pikipiki wawili, Dotto Selemani (23) na Mhira Berati (23), ambao ni wakazi wa Wami Dakawa, wilayani Mvomero, walifariki dunia papo hapo baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kugongwa na gari.

Alisema watu hao waligongwa Julai 15, mwaka huu, saa tisa usiku katika eneo la Kwamwarabu, Mvomero, Barabara ya Morogoro kwenda Dodoma na gari lenye namba za usajili T361 BPE Mistubishi Fuso, lililokuwa likiendeshwa na Mohamed Tore (30), ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.

Aliitaja pikipiki hiyo kuwa ina namba za usajili T539 ART, aina ya beta, iliyokuwa ikiendeshwa na Doto Selemani, ikitoka Morogoro mjini kuelekea Wami Dakawa na chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari hilo.

Katika tukio jingine, mpanda baiskeli, Faraji Nyato (28) ambaye ni mkazi wa Dumila, wilayani Kilosa, alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Dumila, baada ya kugongwa na pikipiki yenye namba za usajili T647 BVD.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 13, mwaka huu, saa moja usiku katika Mtaa wa Pointi Dumila na dereva wa pikipiki hiyo hajafahamika baada ya kukimbia.