VIGOGO watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); Mshauri
wa chama hicho Dk Kitila Mkumbo na madiwani wawili, wametiwa mbaroni
wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali.
Wakati Dk Mkumbo ambaye ni
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa amepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, akituhumiwa kutoa lugha ya
matusi kwa mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Mwigullu Nchemba,
Diwani wa Kata ya Mabogini Wilaya ya Moshi, Albert Msando na Alex
Umbella wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, wamehojiwa na polisi kwa
makosa ya jinai.
Dk Mkumbo amepandishwa kizimbani jana
akiunganishwa katika kesi inayomkabili Ofisa wa Sera na Utafiti wa chama
hicho kikuu cha upinzani, Mwita Waitara Mwikwabe (37).
Mwanasheria
wa Serikali, Maria Mudulugu alidai mbele ya Hakimu Ruth Massamu kuwa,
Julai 14 mwaka huu saa 10.00 jioni, mshtakiwa Dk Mkumbo alitoa lugha ya
matusi dhidi ya mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi.
Mwanasheria
aliiambia mahakama kuwa, Dk Mkumbo alitamka kuwa mbunge huyo ni malaya,
mzinzi na ni 'the comedy' (msanii), huku akijua wazi kuwa kitendo hicho
ni kinyume cha sheria.
Mwansheria Mudulugu alisema kuwa mshtakiwa
alitoa lugha hiyo ya matusi kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema
uliofanyika katika viwanja vya kituo cha mabasi cha Kijiji cha Nguvumali
Kata ya Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo na yupo nje baada ya kudhaminiwa wa watu wawili. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 30 mwaka huu.
Wakati
huo huo, vijana wawili wakazi wa Kata ya Ndago, Paulo Nashakigwa (27)
na Emmanuel Shilla (24) wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo
wakituhumiwa kushiriki kumuua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) Yohana Mpinga (30).
Mudulugu alidai mbele ya mahakama
hiyo kuwa Julai 14 mwaka huu, majira ya alasiri wakiwa katika Kijiji cha
Nguvumali Kata ya Ndago wote kwa pamoja wakitumia fimbo na mawe,
walimpiga Yohana na kusababisha afariki dunia.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Washtakiwa
hao wameunganishwa na wenzao 12 ambao wamesomewa shtaka hilo la mauaji
Julai 16 mwaka huu. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 30 mwaka huu.
Madiwani watiwa mbaroni
Katika
hatua nyingine, madiwani wawili wa Chadema wanahojiwa na polisi kwa
makosa mbalimbali likiwamo la kushusha bendera ya CCM na kupandisha
bendera ya taifa.
Diwani wa Kata ya Mabogini Wilaya ya Moshi,
Albert Msando alikamatwa Jumanne wiki hii na kuhojiwa kwa saa mbili kwa
tuhuma za kushusha bendera ya CCM.
Msando ambaye pia ni
mwanasheria, anadaiwa kushusha bendera hiyo ya CCM iliyokuwa
ikipeperushwa katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Chekereni kwa madai
kuwa ofisi hiyo ni mali ya wananchi na si ya CCM.
Diwani huyo
alilithibitishia gazeti hili jana kuhusu kuhojiwa na kusisitiza japokuwa
CCM wanadai ofisi hiyo ni mali yao waliyoijenga chini ya mfumo wa chama
kimoja, hawana mamlaka ya kuweka bendera yao.
“Tunakubali kuwa
ofisi hii ilijengwa chini ya mfumo wa chama kimoja wakati huo ni CCM,
lakini ilijengwa na wananchi wenyewe siyo CCM hivyo bendera inayostahili
kupepea ni ya taifa,” alisema.
Hata hivyo baada ya diwani huyo
kuhojiwa aliachiwa bila masharti na kuelezwa kuwa jalada lake
lingepelekwa kwa viongozi wa juu wa polisi kwa hatua zaidi.
Wakati
huohuo, Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Alex Umbella na
Mtendaji wa Kata hiyo, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuharibu
mazingira katika Shule ya Sekondari Kisomachi.
Viongozi hao wawili
walikamatwa juzi saa 4:00 asubuhi baada ya kukata miti na uzio wa shule
hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi ili kupisha
upanuzi wa barabara kijijini hapo.
Mkurugenzi wa Elimu wa Kanisa
Katoliki Jimbo la Moshi, Padri William Ruwaichi alidai kuwa ukataji huo
wa miti iliyo mbali na barabara, ulifanywa bila kushirikisha uongozi wa
kanisa.
“Sisi kama kanisa hatupingi maendeleo, lakini
tunacholalamikia ni ukiukwaji wa taratibu kwa sababu huwezi kuingia
kwenye taasisi yetu na kukata miti bila kutushirikisha. Tunalaani tukio
hili,” alilalamika.
Ingawa Diwani Umbela hakuweza kupatikana
kutokana na simu yake kuita bila kupokewa, Kamanda wa Polisi, Robert
Boaz amethibitisha kukamatwa kwao.
Kamanda Boaz alisema diwani
huyo na mtendaji huyo wa kata wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano
kuhusiana na tuhuma za kuharibu mazingira kwa kukata miti na uzio katika
shule hiyo.
Chadema chatoa tuhuma nzito
Siku
chache baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba kuwatuhumu
wabunge wa Chaderma kuwa wamemtumia ujumbe wa vitisho, chama hicho
kimeibuka na kusema ujumbe huo umetumwa na mtoto wa kigogo wa CCM
anayemiliki mtambo wa kuingilia mawasiliano ya watu kwa mbinu za
kijasusi hapa nchini.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere
Marando alisema jana kuwa mtoto huyo amenunua mtambo huo nchini Israel
na anautumia kuandaa ujumbe huo wa maneno na kuingilia mawasiliano ya
simu za wabunge hao.
“Tulipopata malalamiko ya mbunge huyo wa
Singida Magharibi wa kutumiwa ujumbe wa kutishiwa maisha na wabunge
wetu, Tundu Lissu na John Mnyika, mimi kama kiongozi wa Idara ya
Intelijensia ya Chadema nilifuatilia. Niliwahoji (wabunge hao)
wakakataa na nilipofuatilia nikagundua kuwa ujumbe huo umetumwa kwa
kutumia mtambo huo,”alisema Marando.
Marando ambaye alisita
kutaja jina la mtoto huyo, jina la baba yake na cheo chake kwa madai
kuwa si wakati mwafaka kwa sasa, alitaja majina ya kampuni mbili za
nchini Israel alizodai ndizo zilizogundua mtambo huo.
“Nchini
Israel kuna kampuni mbili ambazo ni (Verinty na Nice Systems), kampuni
hizi zimegundua mtambo wenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya watu
kwenye mitandao yao, iwe Intaneti au simu, unaweza kuandaa ujumbe mfupi
na hata mrefu na kwa kutumia namba za mawasiliano za watu wengine,
unaweza kuonyesha kuwa mtu mmoja amemtumia ujumbe mtu wa pili na
ikaeleweka hivyo,” alisema.
Alisema kutokana na tukio hilo Chadema kimejipanga kukabiliana na kesi inayotarajiwa kufunguliwa dhidi ya wabunge hao.
“Tayari
tunazo taarifa kuwa Serikali kupitia kwa Mwanasheria wake Mkuu imeanza
kuandaa kesi dhidi ya wabunge hao, lengo likiwa kudhoofisha chama na
juhudi za uwakilishi wao bungeni. Sisi kama chama na mimi kama
mwanasheria mwandamizi tumejipanga kukabiliana na kesi hiyo,”alisema.