Prof. Tibaijuka asema wabunge wanahitaji maombezi
WAKATI mjadala wa Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma ukitawaliwa na vijembe, kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis Khalifa, amesema mhimili huo wa dola umeoza na una udhaifu mkubwa unaotokana na kiti cha Spika kukosa umakini na baadhi ya wabunge kukosa maadili wakati wakijadili hoja zinazolihusu taifa.
Aidha sheikh huyo amelishambulia Bunge baada ya juzi kushindwa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kutokana na utoro uliosababisha kushindwa kufikia idadi ya wabunge wanaopaswa kuwamo ukumbini wakati wa kupitisha bajeti kama kanuni inavyoelekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Khalifa alisema mwenendo wa Bunge hivi sasa unahuzunisha kutokana na tabia inayozidi kujengeka miongoni mwao ya kutumia uhuru wao vibaya.
Bila kutaja majina, sheikh huyo maarufu nchini alisema baadhi ya wabunge na hata viongozi wa mhimili huo wanaenda kinyume na maadili ya Kitanzania kwa kukosa staha na kutoa maneno ya dharau na kebehi hata matusi kwa wabunge wenzao.
“Wabunge wetu wakati mwingine wanaonyesha kutojali heshima kwani utashuhudia kijana mdogo anashindwa kuonyesha heshima kwa kiongozi wa serikali au mtu mzima anayelingana na mzazi wake na wabunge au viongozi wazee nao wanakosa staha kwa mbunge kijana na hivyo kulifanya Bunge lionekane kama kijiwe cha wahuni,” alisema Khalifa.
Kwa mujibu wa Khalifa, vurugu ndani ya Bunge zinatokana na wabunge wachache kutafuta umaarufu kwa njia ya mkato kwa kutotii kanuni za Bunge na kwa kutumia lugha chafu.
“Wabunge wajue wananchi wanawaangalia. Binafsi naona malumbano hayo ni jambo jema sana kwa sababu litawasaidia wananchi kuwa makini kuchagua wabunge, hivyo mwaka 2015 tunategemea wananchi watasahihisha makosa waliyofanya kuchagua baadhi ya wabunge ambao tabia zao zinakera na hawafai kuendelea kubaki Bungeni,” alisema Khalifa.
Hivi karibuni wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Mwenyekiti wa Bunge, Steven Mabumba, alishindwa kuongoza kikao na kusababisha vijembe, kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi.
Mvutano na malumbano hayo ya kisiasa vilimfanya Mbumba kuonyesha wazi upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani.
Mabumba alifikia hatua ya kutoa hata kauli chafu Bungeni dhidi ya Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, akisema mbunge huyo “anawashwawashwa” na kutaka kusimama mara kwa mara kuomba mwongozo.
Baadaye alimtoa nje Mbunge Kasulu Moses Machali (NCCR Mageuzi) akidai kuingilia mjadala huo na kuongeza kuwa alikuwa na ‘kiherehere’ cha kudandia mambo yasiyomhusu.
Malumbano hayo yaliyoendelea kwa siku mbili, yalitokana na hoja ya mgomo wa madaktari na jaribio la kutaka kuuawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, ambaye alitekwa nyara katika mazingira ambayo yanailazimisha serikali kuendelea kujitetea kwamba haikuhusika kumteka daktari huyo.
Aliyeanza kuchafua hali ya hewa juzi Bungeni ni Mbunge wa Viti Maalum na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, ambaye alitoa tuhuma dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisema kinahusika na mgomo wa madaktari na kwamba waliomteka walivaa magwanda yanayoelekeana na nguo wanazovaa wafuasi na wanachama wa CHADEMA.
Wakati Manyanya akiendelea kuzungumza, Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alisimama kupinga kauli hiyo na kumtaka msemaji athibitishe au afute kauli yake.
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Mwigulu Nchemba aliungana na Manyanya kwamba CHADEMA inahusika akitumia kauli kama za Manyanya.
Hoja hiyo ilimtibua Mnyika, akatumia kanuni mbalimbali kuwabana wasemaji (Manyanya na Mwigulu), na kuwataka wathibitishe au wafute kauli zao.
Hata hivyo kauli ya Manyanya imewasikitisha baadhi ya wabunge wa CCM kwa madai kuwa mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alipotoka.
Hadi sasa Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhoji uhali wa Mwenyekiti wa Bunge, Mabumba, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge hao, lakini hadi sasa kiti cha Spika hakijatolea uamuzi.
Malumbano mengine yaliibuka wiki iliyopita baada ya baadhi ya wabunge kutaka kujadili chanzo cha ajali ya meli ya MV. Skagit iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 150.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), walitaka Bunge kujadili ajali ya meli hiyo kama dharura.
Mambo yalianza kwenda kombo baada ya Lissu kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kifungu cha 47 (1) kikiambatana na kifungu cha 47 (3) cha kutaka Bunge liahirishe shughuli zake na kujadili jambo la dharura la taifa.
Katika mwongozo wake, Lissu alisema katika kipindi cha maswali kulijitokeza swali linalohusu ajali za baharini, ambapo wabunge wengi walionyesha hisia zao hasa kutokana na ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea juzi na kuua Watanzania wengi.
“Mheshimiwa Naibu Spika huu ni muda muafaka wa kulijadili suala hili hasa ikizingatiwa kuwa ni muda mfupi tu tangu itokee ajali ya Spice Islander na kuua idadi kubwa ya Watanzania inatokea tena ajali ya meli kuzama na kupoteza maisha ya ndugu zetu, tujadili jambo hili kama dharura,” alisema.
Baada ya kauli ya Lissu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuliomba Bunge lisijadili jambo hilo kwa kuwa hivi sasa taifa linashughulikia na uokoaji pamoja na kuhifadhi miili ya marehemu.
Baadaye alisimama mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), akasema ipo haja kwa jambo hilo kujadiliwa bungeni kama suala la dharura.
Alisema kuwa katika ajali nyingi zilizotokea za meli ikiwemo ya Mv Bukoba na Mv Spice Islander kuliundwa tume kuchunguza ajali hizo lakini matokeo yake hayakutolewa.
Mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliomba mwongozo na kuishutumu serikali kuwa imezoea kutoa hoja kuwa jambo fulani linashughulikiwa na kusisitiza umuhimu ajali hiyo kujadiliwa bungeni hapo kama dharura.
Akitoa mwongozo dhidi ya hoja ya Lissu, Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, aliikataa hoja ya Lissu kwa madai hoja yake haikuungwa mkono na wabunge licha ya kuitumia vizuri kanuni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, aliingilia kati mabishano hayo na kufafanua kanuni hiyo kuwa inazungumza wazi kwamba baada ya maswali mbunge ataomba mwongozo na kutoa hoja ya Bunge kuahirishwa ili kujadili jambo la dharura kwa taifa.
“Waheshimiwa wabunge kwa hili Lissu alishatoa hoja, sisi binadamu tuna vichwa tuvitumie kufikiri na si kufugia nywele tu,” alisema Werema jambo lililoibua tafrani ambapo Lissu alidai ametukanwa na kutaka mwanasheria huyo afute kauli yake,”
Lissu na baadhi ya wabunge wa chama hicho waliondoka bungeni humo kwa hasira.
Ndugai naye wakati fulani aliwahi kumkejeli Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), kwamba wananchi wa jimbo hilo wamechagua kituko.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka amewataka Watanzania kuwaombea viongozi wa ngazi zote wakiwemo wabunge ili wapate hekima na busara kutoka kwa Mungu.
Akizungumza jana kwenye viwanja vya Jagwani wakati wa maombi maalum kwa ajili ya taifa yaliyoandaliwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki Jimbo Kuu jijini Dar es Salaam Tibaijuka alisema kuwa wabunge wanapaswa kisikilizana na kushindana kwa nguvu ya hoja na si vinginevyo.
Tibaijuka pia aliwataka waumini hao kuwaombea viongozi wa serikalini nao ili wapate hekima sawa na aliyokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“Waumini wa Karismatiki naomba tuliombee Bunge, taifa na viongozi kwa ujumla kwani wakifuata nyayo za Baba wa Taifa hakutakuwa na ufisadi wala migomo na mtu anayezungumzia udini, itikadi za vyama au kubaguana huyo ana matatizo ya akili,” alisema waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Mratibu wa Uinjilishaji Karismatiki Arbogasti Kanuti alisema wanafanya maombezi ya mara kwa mara kwa kuwa dini hutengeneza watu wenye maadili lakini wameamua kuliombea taifa kwa sababu sasa linapitia changamoto nyingi ikiwemo rushwa, mauaji, migomo na upatikanaji wa Katiba mpya.