Tuesday, September 4, 2012

Mwandishi ameuawa na bomu la machozi

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limearifiwa kuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi ameuawa kwa bomu la machozi.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wahariri pamoja na mameneja wa vyombo vya habari yaliyoanza mkoani Morogoro jana.

Mukajanga alisema baada ya kupata taarifa za awali za kifo cha Mwangosi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa ( IPC), alilazimika kumtafuta kwa njia ya simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.

Alisema katika mazungumzo yao, Dk Nchimbi alimfahamisha kuwa yupo nje ya nchi, Afrika Kusini kikazi na kukiri kupata taarifa za kifo hicho.

Mukajanga alinukuu mazungumzo yake na Waziri huyo kwa kusema; “Nimepata taarifa za kifo hicho na taarifa za awali zimesema ni bomu la machozi halikulipuka kitaalamu na limemuua (Mwangosi) na kuwajeruhi watu wengine watatu.”

Alisema Dk Nchimbi alitoa rambirambi kwa waandishi wote wa habari nchini kutokana na kifo cha mwandishi mwenzao.

Kauli zakinzana
“Hapa tunaona kauli ya Waziri inapishana na Polisi ambao wanadai amekufa kwa kupigwa na kitu kilichorushwa, wakati Waziri anadai ni bomu la machozi ambalo halikulipuka kitaalamu na kusababisha kifo na majeruhi watatu,” alisema Mukajanga.

Alisema MCT imefedheheshwa kwa kuwa mwandishi aliyeuawa, alikuwa kazini akitekeleza wajibu wake wa kukusanya habari.

Mbali ya kufedheheshwa huko, Mukajanga alisema mauaji hayo yametoa picha mbaya kwa Tanzania wakati huu ambao wajumbe wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani wapo nchini kwa ajili ya mkutano ambao Tanzania ni mwenyeji.

“Mimi ni Makamu wa Rais wa Mabaraza ya Habari Duniani, nimefedheheka sana kwa tukio hili, limefanyika wakati wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani wa mabaraza ya habari wapo hapa nchini kuhudhuria mkutano… wanakutana na vichwa vya habari kwenye magazeti na televisheni kuhusu kuuawa kwa mwandishi wa habari akiwa kazini,” alisema Mukajanga.

MCT imewataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari ikiwemo kulindwa na Serikali wanapokuwa kazini. Alisema mauaji hayo yameandika historia mbaya na ya kwanza tangu kupata Uhuru.

“Kwa mara ya kwanza tangu Uhuru mwandishi wa habari anauawa akiwa kazini kutekeleza wajibu wake ... tukio hili limetoa sura kwamba waandishi wa habari wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya kuchukua tahadhari kwenye matukio ya hatari,“ alisema Mukajanga.

Timu ya uchunguzi
Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena, aliutaka uongozi wa Polisi kuwajibika kwa kuanzia na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema.

Alisema kwa kushirikiana na MCT, wameunda timu ya uchunguzi itakayokwenda mkoani Iringa kubaini ukweli wa tukio hilo.

“Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu,” alisema Meena.

Wajumbe wa timu hiyo ni pamoja na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte, Mhariri wa Gazeti la Mwananchi na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa, Simon Berege.

Kampuni ya Africa Media Group inayomiliki Kituo cha Channel Ten ambayo Mwangosi alikuwa akifanya kazi imelaani mauaji hayo ya mwakilishi wake na kutaka uchunguzi huru kubaini sababu na mazingira ya mauaji hayo.

Mhariri wa Habari wa Channel Ten, Dina Chahali alisema wanataka uchunguzi huru ili waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Alisema taarifa kutoka Polisi Makao Makuu zimeeleza kuwa wametuma maofisa wake mkoani Iringa kwa uchunguzi wakiwemo wataalamu wa mabomu kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Historia ya Mwangosi

Dinna alisema Mwangosi alizaliwa Tukuyu mkoani Mbeya mwaka 1972 na mazishi yake yanatarajia kufanyika katika Kijiji cha Busoka, Tukuyu katika Wilaya ya Rungwe mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Mwangosi alijiunga na Channel Ten kuwa mwakilishi wa wa Iringa Julai 27, 2006 na ameacha mjane na watoto wanne. Kampuni hiyo kwa kushirikiana na vyama vya waandishi wa habari Mkoa wa Iringa na Mbeya, wamekubaliana kushughulikia msiba kwa kushirikiana na familia mpaka atakapopumzishwa.

Wanaharakati
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya alisema taarifa hiyo ni ya kuhuzunisha haswa ikizingatiwa kuwa Polisi kazi yake ni kulinda raia.

“Tanzania ni nchi ambayo inajivunia kuwa na demokrasia kubwa, kitendo kile hakikubaliki kamwe kwani Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kazi yao ni kuwalinda raia,” alisema Ussu.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya alisema kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na wote kwa kuwa hakuna soko ambalo roho ama uhai wa binadamu unapatikana. “Ninataka kumuuliza IGP (Said Mwema) aliwahi kusema ataliunda Jeshi la Polisi na kuwa la kisasa na lenye ustaarabu…je kuua mtu ndio kuendesha jeshi hilo kwa njia ya ustaarabu,” alihoji Ananilea.