Tuesday, August 14, 2012

WAISLAMU MKOANI SINGIDA WAMEAHIDI KUSHIRIKI SENSA



Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone (wa kwanza kushoto) akizungumza na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Singida (hawapo kwenye picha) kwa lengo la kuwahimiza waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa sensa ya taifa ya watu na makazi ya mwaka huu ili waweze kushiriki.


Sheikh Issa Nassoro Issa akichangia mada ya sensa ya taifa inayotarajiwa kufanyika Agosti 26 mwaka huu.


Katibu wa BAKWATA mkoa wa Singida Juma Ngaa akichangia mada ya uhamasishaji wa sensa ya taifa ya mwaka huu.

Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini waliohudhuria mkutano ulioitishwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone kwa lengo la kuwahimiza viongozi wao waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa sensa ya taifa inayotarajiwa kufanyika agosti 26 mwaka huu.

Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone (kushoto) akishiriki dua iliyofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini kwa ajili ya kuombea sensa ya taifa ya mwaka huu iweze kufanikiwa.

Waislamu mkoani Singida, wameahidi kushiriki sensa ya taifa ya mwaka huu kikamilifu na kamwe, hawatakubali kupotoshwa na watu/kikundi kinachotaka kuvuruga sensa hiyo yenye lengo la kuendeleza Watanzania.

Ahadi hiyo nzito, imetolewa na viongozi wa ngazi mbali mbali wa dini ya kiislamu kwenye mkutano wa viongozi wa madhehebu dini ulioitishwa na mkuu wa mkoa Dk. Parseko Kone. Lengo la mkutano huo, ni kuhamasisha zoezi la sensa inayotarajiwa kufanyika agosti 26 mwaka huu kwa viongozi wa madhehebu ya dini.

Walisema vipeperushi vinavyosambazwa na baadhi ya waumini wa kiislamu vinavyotoa wito kwa waislam wasishiriki sensa, havina sababu za msingi zaidi ya kutaka kukwamisha sensa ambayo imehimizwa hata kwenye kitabu kitakatifu cha Quruan.

“Tujuavyo sisi viongozi wa dini ya kiislamu, kwanza ustawi wa dini ya kiislamu hauwezi kuwa na tija bila kufanya sensa ya kujua pamoja na mambo mengine,idadi ya waumini ili uweze kujipanga vizuri kuwahudumia. Mwenyezi Mungu aliisha amrisha sensa ifanyike, sasa mwanadamu ataizuiaje”, alihoji Sheikh Issa Nassoro Issa.

Sheikh Issa alisema vipeperushi hivyo ambavyo vimesambazwa mkoani hapa na sehemu mbalimbali nchini, vimeandaliwa na kusambazwa na kikundi kinachojiita wanaharakati wa dini ya kiislam (Hajakitaja).

“Sisi waumini wa kiislam na hasa wa mkoa wa Singida, hatuongozwi na vikundi vya wanaharakati, tunaongozwa na viongozi waliochaguliwa. Kwa hiyo, mkuu wa mkoa, usiwe na wasiwasi, waislam mkoani Singida, watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sensa ya mwaka huu, imefikia malengo”, alisema Sheikh Issa.

Mapema mkuu wa mkoa wa Dk. Kone aliwaomba viongozi hao wa madhehebu ya dini, kutenga muda mfupi baad aya kumalizika kwa ibada, kwa ajili ya kuwahamasisha waumini wao kushiriki sensa ya taifa ya mwaka huu.

“Ninyi ni viongozi wa umma na mnaaminika sana, kwa hali hiyo, mkiwahimiza kushiriki sensa ya mwaka huu, nina imani lengo linalotarajiwa la sensa, litafikiwa”,alisema.

Akifafanua zaidi,Dk. Kone alisema serikali inafanya sensa ili kupata taarifa zitakazoisaidia katika kupanga, kufanya maamuzi, kusimamia na kutathimini sera ya mipango ya maendeleo. Taarifa za sensa hutumiwa pia na sekta binafsi na jamii kwa ujumla katika shughuli zao za kila siku.

“Kushiriki sensa ni muhimu kwa sababu kutaipa nafasi serikali kufahamu mahitaji ya wananchi wa kila rika, mahali walipo na watu wenye mahitaji maalum”,alisema mkuu huyo wa mkoa.