Friday, August 10, 2012

Pinda- Kipengele cha dini katika sensa hakina tija


Waziri Mkuu Mizengo Pinda
SERIKALI imesisitiza kuwa, kipengele cha dini katika sensa hakina umuhimu kutokana na ukweli kwamba, si moja ya vigezo muhimu katika kuzingatia mipango ya maendeleo nchini.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyasema hayo leo bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema), akitaka ufafanuzi wa kuondolewa kwa kipengele cha dini katika sensa.

Lyimo aliuliza:“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na malumbano makali sana, kwa baadhi ya waumini wa dini moja wakihoji sababu ya kuondolewa kwa kipengele cha dini…sasa ni kwa nini Serikali imeondoa kipengele hicho?”

Lakini Waziri Mkuu aliyerejea jana asubuhi akitokea mkoani Arusha na kuingia moja kwa moja bungeni akitokea uwanja wa ndege mjini hapa, alisema Serikali haioni tija kuingiza kipengele cha dini katika sensa kwa kuwa maendeleo ya nchi hayapangwi kwa kuangalia kigezo cha dini.

“Tumekuwa na sensa kadhaa kuanzia miaka ya nyuma huko, hili suala halikuwahi kujitokeza. Hatukuhangaika na eneo hilo na sababu ni nyepesi, kwamba katika kupangilia mambo ya maendeleo, hatupangi kwa kuzingatia vipengele vya dini…

“Sisi Watanzania ni wamoja na unapanga mambo kwa kuangalia mambo ya msingi, mathalani jinsia ili kupangilia mambo, mfano wanawake ni jinsi gani ya kuwawezesha, au walemavu kwa ajili ya kuangalia jinsi ya kuwasaidia.

“Lakini ukishaanza kuingiza dini, kwa Serikali sisi tunadhani halina tija halina…hofu tuliyokuwa nayo na mimi ni mmoja wapo, jambo hili linaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima, tuzingatie mambo ya msingi tu…”

Sensa ya Watu na Makazi inatarajiwa kufanyika Agosti 26, kote nchini, lakini katika miezi ya hivi karibuni, makundi, hasa ya baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu yamekuwa yakipotosha na kuwataka waumini kususia kwa kuwa kipengele cha dini kimeondolewa.

Hata hivyo, Serikali, viongozi wa dini karibu zote nchini, wakiwamo wa Kikristo na Waislamu na wanaharakati, wamekuwa wakielimisha juu ya umuhimu wa kushiriki katika sensa ili kuiwezesha Serikali kupanga vipaumbele vyake kwa kuangalia mahitaji halisi ya nchi na idadi ya watu wake.

Wakati huohuo Waziri Mkuu amekiri kuwa, tatizo la watoto wasio na makazi ni kubwa, hivyo amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali na jamii kwa ujumla, kufahamu kila mmoja anashiriki kikamilifu katika kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema hiyo ni changamoto ya nchi, na lengo la kila upande liwe ni jinsi gani watoto hao watasaidiwa.

“Ni tatizo la kijamii, na linatugusa sisi wote, viongozi kwa ujumla wake, jamii kwa upande mwingine.

“Ndiyo maana tunafanya juhudi kuhakikisha vituo vya kulelea watoto, mashirika yasiyo ya kiserikali vinapewa ushirikiano kuhakikisha watoto wanakuwa salama.

“Lakini bado kuna changamoto, baadhi ya watoto pamoja na kulelewa, bado wanatoroka,” alisema.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), aliyetaka kujua hatua ambazo wakuu wa mikoa na wilaya wanazichukua katika kukabiliana na ongezeko la watoto wasio na makazi, alisema wametapakaa katika mikoa mingi inayokua nchini, na hata katika milango ya Bunge.

Alisema kitendo hicho, kinaifedhehesha nchi, na kutolea mfano kwa wageni wanaotoka nje ya nchi wanaowakuta watoto wakizurura hovyo, hata karibu na Bunge. Lakini kabla ya kumpa Waziri Mkuu nafasi ya kujibu, Spika Anna Makinda alisema;

“Lakini si ndani ya Bunge“. Ndipo Waziri Mkuu alirudia mwito kwa jamii kushiriki kwa namna moja ama nyingine kupata tiba ya kudumu na tatizo la watoto wa mitaani, huku akisisitiza hilo si jukumu la wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya pekee.

“Hata wabunge, hao ndio wapiga kura wetu. Tushirikiane kuona ni kwa namna gani tunakabiliana na changamoto hii,” alisema.