Friday, August 10, 2012

Malawi yapuuuza tishio la Tanzania


SERIKALI ya Malawi imepuuuza tishio la Serikali ya Tanzania kuhusu mzozo wa mpaka katika Ziwa Nyasa na kusisitiza kuwa, ziwa hilo lote ni la Malawi hivyo utafiti wa mafuta utaendelea.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa ndani wa nchi hiyo, Uladi Mussa, amekaririwa akisema kuwa, Watanzania hawana mamlaka ya kuzuia utafiti wa mafuta uliokuwa ukifanywa katika Ziwa Nyasa, na shinikizo likiendelea Malawi watawasilisha suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa.

“Niwahakikishie watu wote nchini watulie. Tunazungumza na Serikali ya Tanzania na hakuna kitakachoharibika.Shinikizo likizidi tutapeleka suala hili kwenye mahakama ya kimataifa” amesema Waziri Mussa juzi wakati akizungumza na kituo cha redio cha Zodiak (ZBS).

Amesema, Serikali ya Malawi ina ushahidi kuthibitisha kwamba, Ziwa Nyasa ni la nchi hiyo, na kuna mikataba inayoonesha hivyo, hoja ya Tanzania haina mantiki.

Tanzania inasema mpaka wa kweli unapita katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la Kaskazini Mashariki ya Ziwa kati ya Latitudo digrii tisa na digrii 11 kuwa eneo la Tanzania.

“Hakuna kitu hapa. Wote tunajua ziwa hili ni letu. Kama haya madai yangetolewa na Msumbuji angalau ingeleta mantiki lakini si Tanzania.

Tuna ushahidi wote na mikataba ipo kuonyesha kwamba Ziwa Malawi ni la Malawi” alisema Mussa.

Amesema, hoja ya Tanzania kwamba, kuna mpaka wa Tanzania na Malawi katikati ya ziwa hilo inamantiki kama hakuna mikataba lakini kwa sasa mkataba upo tangu mwaka 1890 unaoitwa Heligoland Treaty.

Inadaiwa kuwa, mwaka 1963, uliokuwa Umoja wa Nchi huru za Africa (OAU) uliazimia kwamba, nchi wanachama zitambue na kukubali mipapa iliyorithiwa wakati nchi hizo zilipopata uhuru, na kwamba, maazimio kama hayo yaliridhiwa pia katika mikutano ya Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2002 na 2007 Serikali ya Tanzania imeitaka Malawi isitishe mara moja kufanya utafiti wa mafuta katika eneo husika na kusisitiza kuwa ipo tayari kulinda mipaka ya nchi yake kwa gharama yoyote.

Mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa tamko bungeni mjini Dodoma, na kubainisha kwamba, upo uwezekano mkubwa wa mgogoro huo mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya nchi husika.

Alisema, Serikali inathamini uhusiano mzuri uliopo na inathamini kudumisha ujirani mwema isipokuwa Malawi inatakiwa kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita ya kutakiwa kusitisha utafiti huo.

“Napenda kuyaonya makampuni yote yanayofanya utafiti kwenye eneo hilo kuanzia leo Jumatatu (jana) kuacha shughuli za utafiti katika maeneo hayo hadi makubaliano na majadiliano yatakapoisha.

“Tuachie diplomasia …Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi wote wa eneo la Ziwa Nyasa kuendelea na shughuli zao ziwani na nchi kavu kama kawaida na bila wasiwasi wowote kwa sababu Serikali yao ipo macho ikiwa imara na iko tayari kulinda mipaka ya nchi yetu kwa gharama yoyote,” alisema Waziri Membe.

Akielezea historia ya mgogoro huo, Waziri Membe alisema ni wa muda mrefu ambao ulishindikana kutatuliwa miaka ya 1960 na 1990 kwa kuwa mazingira ya wakati huo hayakuruhusu.

Alisema tatizo hilo lisingeweza kutatuliwa wakati wa utawala wa Rais Kamuzu Banda wa Malawi kwa kuwa katika kipindi hicho, alikuwa rafiki wa Serikali ya Makaburu ya Afrika Kusini na Tanzania ilikuwa rafiki wa wapigania ukombozi wa ANC.

Aidha, kutokana na Tanzania kuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi, Banda aliamini Tanzania ilikuwa kichaka cha maadui wa Serikali yake kiasi kwamba mazungumzo yasingewezekana.

Alisema marais waliofuata hususan Bingo Mutharika walitengeneza uhusiano mzuri uliokaribisha mazingira ya kuzungumzia suala hilo.

Alisema mwaka 2005, Rais Mutharika alimwandikia Rais Benjamin Mkapa, lakini kwa kuwa wakati huo kilikuwa kipindi cha uchaguzi, alimwachia Rais Jakaya Kikwete kushughulikia suala hilo ambaye alikutana mara mbili na rais huyo wakakubaliana waunde timu ya wataalamu kutafuta suluhu.

Alisema timu hizo zilianza kukutana tangu mwaka juzi, lakini wakati zikiendelea kukutana, eneo la mpaka likachukua sura mpya hali iliyoashiria kuhatarisha usalama kutokana na kuwepo taarifa za kampuni zinazotafiti mafuta hivi karibuni.

“Tulipata taarifa za kuaminika kutoka TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli) kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa Kaskazini mwa Msumbiji limegawanywa katika vitalu,” alisema Membe na kwamba kampuni husika ziliomba kibali cha ndege zake kufanya utafiti huo, lakini Jeshi la nchini likakataa.

Alisema kati ya Januari na Julai mwaka huu, ndege tano zenye uwezo wa kutua kwenye nchi kavu na majini, zilionekana zikivinjari na kutua kwenye Ziwa Nyasa katika ufukwe wa Tanzania hali ambayo Serikali iliwasiliana na Malawi kutaka wajadili mustakabali wake.

Iliomba ufanyike mkutano kati ya wataalamu na baadaye mawaziri. Mkutano wa wataalamu ulifanyika Julai 25 na 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.