Friday, August 24, 2012

Mwakyembe awasimamisha kazi vigogo wa Bandari


Mwakyembe ang’ata tena

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameendeleza kasi yake ya kuisafisha wizara yake, ambapo amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na viongozi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazowakabili.

Mbali ya Mgawe, vigogo wengine waliosimamishwa kazi ni wasaidizi wake wawili, Julius Mfuko, Hamad Koshuma pamoja na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Casian Nghamilo.

Timua timua hiyo ya Waziri Mwakyembe inakuja zikiwa ni wiki chache tangu afanye uamuzi mgumu kama huo katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kumsimaisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Paul Chizi na wakurugenzi wanne kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe alisema kutokana na upungufu waliobaini, wameona ni vema viongozi hao wakakaa pembeni na kwamba ameunda kamati ya watu saba watakaochunguza masuala hayo.

Alisema nafasi ya Mgawe kwa sasa itakaimiwa na Mhandisi Madeni Kipande kutoka Wizara ya Ujenzi na kwa nafasi nyingine, wawekwe watu wenye uadilifu.

“Nimeamua kumchukua mtu nje ya bandari kukaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu ili kuondoa wasiwasi, maana angetoka ndani angeshindwa hata kuingia ofisini. Najua uamuzi huu utahojiwa, lakini tuendelee kuvumiliana, kwani ukweli haupingwi,” alieleza.

Pamoja na hatua hiyo, alisema ameunda kamati ya watu saba kuchunguza tuhuma mbalimbali bandarini hapo, lakini akagoma kuwataja wajumbe watakaounda kamati hiyo, kwa madai kuwa wanashughulika na watu wenye fedha, kwamba hadidu za rejea zitakuwa na maswali 50.

Dk. Mwakyembe aliongeza kuwa mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia ameiagiza bodi ya mamlaka hiyo kuwasimaisha kazi watumishi wa kituo cha kupokea mafuta cha Kurasini (KOJ) ambao ni meneja, meneja wa Jet na injinia wa mafuta wa kituo hicho.

Aidha, aliitaka Kampuni ya Singirimo iliyokuwa inaendelea na zabuni ya kuchukua mafuta machafu iache kufanya kazi hiyo mara moja, kwani inachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura).

“Kwanza muda wa kampuni hii kufanya kazi hiyo umekwisha, hivyo kampuni nyingine iliyoshinda zabuni imepewe nafasi ifanye kazi hiyo. Singirimo ikae pembeni kupisha uchunguzi.

“Haya ni maamuzi yangu, lazima yazingatiwe, na kampuni hii mwaka 2008 Ikulu iliagiza isipewe zabuni kwa kuwa haina sifa, lakini uongozi wa TPA umekaidi agizo hilo mpaka sasa,” alisema.

Alisema sababu nyingine ya kampuni hiyo kunyimwa zabuni ni kuwa na mgongano wa kimasilahi kutokana na viongozi wake kuwa na uhusiano nayo.

Kuhusu wizi wa makontena katika Kitengo cha Kimataifa cha Kupakia na Kupakua Makontena (Ticts), alisema kuwa amekiagiza kitengo cha sheria cha TPA kupitia upya mkataba wake na kuona kama unaheshimu makubaliano yaliyokuwapo na kumpatia ripoti Jumatano ijayo.

Akizungumzia wizi wa mafuta, alisema suala hilo limekuwa vita kubwa na kwamba kampuni inayochukua mafuta hayo hudai ni machafu, lakini mwisho wa siku wanayapeleka kwenye vituo vya mafuta.

“Pale hayatoki mafuta machafu, yanapakwa rangi yaonekane machafu…zabuni ya mafuta hayo inagombewa mno. Tumefuatilia tumegundua kuwa magari yanayochukua mafuta hayo huishia petrol station,” alisema.

Pamoja na hilo, alisema malori yanayochukua mafuta hayo hayafahamiki kiwango kilichochukuliwa na kuongeza kuwa, lori moja lililodai kubeba lita 9,000 za mafuta, lilipopimwa na Kamishna wa Vipimo lilibainika kubeba lita 26,000.

Kuhusu kukosekana kwa flow metres ambazo zinapima kiwango cha mafuta, Mwakyembe alisema ameuagiza uongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja zinapatikana.

“Nimeaagiza watumie single sorce katika kuangiza flow mitres, lakini pia wazingatie sheria ya manunuzi inasemaje,” alisema.

Pamoja na hayo, ameagiza mamlaka hiyo kuacha malipo ya fedha taslimu dirishani kuanzia Septemba mosi mwaka huu, na kwamba watumie benki ama njia nyingine za kisasa.

Alisema njia ya malipo kwa fedha taslimu inaruhusu michezo michafu, pia inapoteza muda mwingi kwa wateja, huku akisisitiza kuwa atakayeshindwa kutumia njia hiyo ampelekee barua kuwa kazi imemshinda.

Rada yatengamaa

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alifafanua kuwa rada ya kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JKN) iliyokuwa imeharibika, imeanza kufanya kazi juzi baada ya kutengemaa.

Alisema, kifaa kilichokuwa kinasumbua kimeshaondolewa na kuwekwa kingine na kwamba wameagiza vifaa vingine vya ziada.

Dk. Mwakyembe alisema kuwa rada ni mashine kama zilivyo nyingine na kwamba imekuwa ikifanyiwa marekebisho kila mwaka.

“Tumekuwa tukiiimarisha mara kwa mara, safari hii sijui mmechochewa na nani. Kusimamishwa rada kwa siku tano, imekuwa habari kubwa. Kenya wanafanya service vile vile … haya ni mashindano ya biashara,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa, imekuwa kawaida kuifanyia marekebisho mashine hiyo na kuwa walipoifungua waligundua kuwa chombo kimekwisha upande mmoja.

“Hii imekuwa ni routen na mwaka kesho tutaisimamisha tena…watu wanasema ndege zitaanguka. Rada haiendeshi ndege. Wale wataalamu waongoza ndege tumewafundisha njia mbili za kuongoza ndege. Moja kama rada inafanya kazi na pili, kama rada haifanyi kazi,” alisema.