JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto katika kukabiliana na vurugu za wananchi katika maeneo ya Madale wilayani Kinondoni na Kariakoo, wilayani Ilala.
Katika tukio la awali jana asubuhi wilayani Kinondoni, watu wanaodaiwa kuwa wavamizi wa ardhi katika eneo la Madale, Kata ya Wazo Hill walibomolewa nyumba zao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Tanzania Daima ilishuhudia nyumba hizo zaidi ya 200 zikibomolewa katika operesheni hiyo inayoelezwa kuwa itadumu kwa siku tatu mfulizo.
Hata hivyo operesheni hiyo ilikumbana na vikwazo kadhaa kwani wavamizi hao walikuwa wamejihami kwa silaha za jadi kama mawe, mikuki, mishale, mapanga na nyinginezo ili kukabiliana na wabomoaji, ndipo Jeshi la Polisi likaingilia kati na kuwasambaratisha kwa mabomu ya machozi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alielezea vurugu hizo akisema kuwa kwa muda mrefu maeneo hayo yalivamiwa na wavamizi hao huku wakiwapiga na kuwaumiza wamiliki halali wa maeneo hayo jambo lililosababisha kuvunjika kwa amani katika eneo hilo.
Aliwataka wavamizi wengine ambao hawajafikiwa na operesheni hiyo kuondoka wenyewe kwa hiari yao na kuyaacha maeneo la sivyo watatiwa katika mikono ya sheria.
Kenyela alisema kuwa katika vurugu hizo hakuna askari aliyejeruhiwa na kwamba wamefanikiwa kuwakamata wavamizi 15, ambao watawafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Nao wamiliki wa maeneo hayo yaliyovamiwa wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, waliipongeza serikali kuamua kuingilia kati sakata la uvamizi wa maeneo yao wakidai ilifikia hatua wavamizi hao wakaanza kutamba kwamba hakuna anayeweza kuwatoa.
Kipindi kifupi kilichopita Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, liliwahi kuwashikilia zaidi ya watu 13 akiwamo Mwenyekiti wa Mtaa wa Madale, Alex Mbuya, baada ya kudaiwa kuhusika na vitendo vya uvamizi wa mashamba ya watu katika maeneo hayo.
Kenyela alisema kuwa kushikiliwa kwa watu hao kulitokana na ofisi yake kupokea malalamiko mengi ya wamiliki wa mashamba yao kuvamiwa na watu wengine na kujenga au kuuza maeneo yao.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Jordan Rugimbana, alisema kuwa hatua hiyo imetokana na agizo la Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mweyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadick.
Aliongeza kuwa kutokana na Wilaya ya Kinondoni kuongoza katika uvamizi wa maeneo ya watu kinyume cha utaratibu, kamati hiyo imelazimika kuchukua hatua ya kutambua maeneo yote yaliyovamiwa katika wilaya zote za mkoa huo ili kuzuia uvamizi huo kujirudia.
Rugimbana alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha wavamizi hao kujihami kwa silaha za jadi kama mapanga, mishale na marungu, jambo alilodai si utamaduni wa Watanzania kupingana na serikali.
Kuhusu wamavizi hao kudaiwa kuwa si raia wa Tanzania, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa amezisikia tetesi hizo na tayari jambo hilo wamekwisha kulifikisha kwenye mamlaka husika ili kushughulikia uraia wa wavamizi hao.
Katika tukio la pili jana mchana katika eneo la Kariakoo, nako polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi za moto hewani ili kutuliza ghasia katika kutanzua mgogoro baina ya mmiliki wa nyumba na mpangaji wake.
Hatua hiyo ilitokana na hatua ya mmiliki wa nyumba hiyo, Samiri Said, kushinda kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, hivyo mpangaji Shaban Hassan, aliyekuwa akidai kumiliki nyumba hiyo kutakiwa kuondoka.
Akizungumza na Tanzania Daima, kiongozi wa Kampuni ya udalali ya Yono, iliyopewa kazi ya kumwondoa mpangaji huyo, Isaac Nguku, alisema walifika eneo hilo kwa amri ya mahakama, kwa lengo la kukabidhi nyumba hiyo kwa Said.
Alisema kuwa walipofika katika eneo hilo majira ya saa 5:00 asubuhi, walikuta kundi la vijana ambao inasadikika kuwa waliandaliwa na Hassan kwa ajili ya kukwamisha zoezi hilo.
Nguku alisema baada ya kuona hali hiyo waliamua kuomba msaada polisi ambao walifika na kuanza kuwatawanya vijana hao.
“Vijana hao hawakuridhika ndipo wakaanza kuturushia mawe kutoka kona zote walizokuwa wamejipanga, kitendo hicho kilisababisha askari kufyatua risasi za moto juu huku wakipiga mabomu ya machozi na kuwatawanya,” alisema.
Baada ya vijana hao kutawanyika, mitaa minne inayozunguka nyumba hiyo ya Kongo, Mkunguni, Tandamti na Mchichi ilifungwa kwa muda.
Naye mmiliki wa nyumba hiyo, Said alisema wavamizi hao walipanga katika nyumbani hiyo tangu mwaka 1972, ambapo baada ya hapo wakajitengenezea hati bandia kwa lengo la kumdhulumu mama yake mzazi.
Alisema kitendo hicho kiliwafanya wafikishe kesi hiyo mahakamani ambako waliwasilisha hati zao ambazo zimewafanya washinde kesi hiyo na mvamizi huyo kuamriwa aondoke, kitendo alichokipinga huku akikata rufaa mara kwa mara na kushindwa zote.
Nyumba hiyo inayogombewa iko Mtaa wa Karikoo, Kitalu namba 86, ambapo wakati vurugu hizo zikiendelea, mvamizi huyo yuko jela akitumikia kifungo cha siku 21.